Jumatano tarehe 19 Februari 2020
Leo ni Jumatano tarehe 24 Jamadithani 1441 Hijria sawa na tarehe 19 Februari 2020.
Siku kama ya leo miaka 897 iliyopita alifariki dunia Ahmad Bin Ali Baihaqi Sabzawari, mmoja wa maulama wakubwa wa elimu ya Qur’ani mjini Nishapur. Ali Baihaqi Sabzawari, alitabahari katika elimu ya nahaw na lugha kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake, huku akitafsiri aya za Qur’an Tukufu. Aidha alimu huyo alikuwa mahiri katika kisomo cha Qur’an Tukufu. Ali Baihaqi Sabzawari ameacha vitabu mbalimbali ikiwemo: ‘Taajul-Masaadir’ na ‘al-Muhit Bi’ilmil-Qur’an.’

Katika siku kama ya leo miaka 547 iliyopita alizaliwa mnajimu na mwanahesabati mashuhuri wa Poland, Nicolaus Copernicus. Awali alijifunza elimu ya nujumu na baadaye tiba, na baada ya kukamilisha masomo alianza kufundisha hesabati huko Roma. Hata hivyo Copernicus aliendelea kudurusu na kufanya utafiti wa elimu ya nujumu na mwaka 1503 alivumbua nadharia ya harakati ya dunia kuzunguka jua na vilevile dunia kujizunguka yenyewe katika kila baada ya masaa 24. Nicolaus Copernicus alifariki dunia tarehe 24 Mei 1543 siku chache tu baada ya kuchapisha kitabu cha On the Revolutions of the Celestial Spheres kinachofafanua nadharia zake.
Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, Ayatullahil Udhma Sayyid Muhammad Ridha Golpayegani, alimu, fakihi mkubwa na mmoja wa marajii wakubwa wa Kiislamu ulimwenguni alifariki dunia. Alizaliwa Golpayegan nchini Iran na kusoma masomo ya dini kwa maustadhi stadi na waliokuwa wametabahari kielimu katika zama hizo akiwemo Ayatullah Hairi. Ayatullah Golpayegani alianza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Qum-Iran baada ya kuasisiwa kwake. Mwanazuoni huyo mkubwa ameandika vitabu vingi katika nyuga mbalimbali.
Tarehe 19 Februari miaka 23 iliyopita alifariki dunia Deng Xiaoping, kiongozi wa zamani wa China na mhandisi wa mageuzi ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo. Katika kipindi cha uongozi wa Xiaoping China ilifanya mageuzi makubwa katika nyanja mbalimbali na alifanya marekebisho makubwa katika uchumi wa kisoshalisti wa wakati huo wa China na kuuelekeza kwenye uchumi wa soko. Wakati huo China ilifanikiwa kuingia katika nyanja mbalimbali za kimataifa na kutatua migogoro iliyokuwepo katika uhusiano wake na nchi kadhaa. Deng Xiaoping alijiuzulu mwaka 1990 kutokana na maradhi na umri wake mkubwa na hadi anafariki dunia alikuwa akihesabiwa kuwa shakhsia mkubwa zaidi wa China.
Miaka 10 iliopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 30 Bahman 1388 Hijiria Shamsia, manowari ya kwanza ya kivita ya Iran inayojulikana kwa jina la Jamaran ilianza kufanya kazi. Jamaran ni manowari ya kijeshi yenye uwezo wa kubeba aina kadhaa za makombora ya kuhujumu meli na kutungua makombora na ndege za adui. Pia ina rada za kisasa na uwezo wa kushiriki katika vita vya kielektroniki. Meli hiyo inayoenda kwa kasi kubwa pia ina eneo la kutua helikopta. Baadhi ya teknolojia iliyotumia kutengeneza manuwari hiyo inamilikiwa na nchi kadhaa tu dunia na wataalamu wa Jamhuri ya Kiislamu wamefanikia kuvunja mzingiro huo na kuiwezesha Iran kuwa miongoni mwa nchi zenye utaalamu wa kubuni na kuzalisha teknolojia hiyo.