Feb 20, 2020 23:11 UTC
  • Ijumaa, Februari 21, 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 26 Mfunguo Tisa Jamadithani 1441 Hijria sawa na tarehe 21 Februari mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita vita vya Dhatus Salasil vilimalizika baada ya Waislamu kujipatia ushindi. Vita hivyo vilianza baada habari kusambaa kuwa kikundi cha washirikina kilitaka kushambulia mji wa Madina. Baada ya habari hiyo kumfikia Mtume Mtukufu (saw), aliwaamuru baadhi ya Waislamu waenda kukabiliana na washirikina hao wakiongozwa na kamanda mmoja aliyetoka upande wa Muhajirina. Hata hivyo baada ya kujua uwezo mkubwa waliokuwa nao maadui, kundi hilo la Waislamu lilirejea nyuma. Mtume alimtuma kamanda mwingine lakini naye pia alirejea na ndipo Mtume Mtukufu (s.a.w) alipomteua Ali bin Abi Twalib (a.s) aongoze Waislamu katika mapigano hayo. Imam Ali (as) aliwashambulia maadui kwa umahiri mkubwa na kurejea Madina na ushindi. Mtume (saw) alifurahishwa sana na ushindi huo kiasi kwamba alikwenda kuwapokea mashujaa hao pindi waliporejea Madina. Wafasiri wa Qur'ani na wanahistoria wengi wa Kiislamu wanasema kuwa Suratul A'diyat iliteremshwa kwa Mtume (saw) kuhusiana na vita hivi. 

Siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, alizaliwa Reinhart Dozy, mtaalamu wa masuala ya mashariki mwa dunia aliyekuwa raia wa Uholanzi. Dozy alizamili katika fani za historia na lugha huku akifikia daraja ya PHD katika fani ya fasihi akiwa na umri wa miaka 24. Reinhart Dozy alipendelea sana kusomea tamaduni za Kiislamu ambapo mbali na kuwa mahiri katika lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kijerumani, alikuwa pia mtaalamu katika lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Uholanzi alifanya utafiti mwingi wa tamaduni za Kiarabu na historia ya Kiislamu, hususan Waislamu wa Andalusia, kusini mwa Uhispania. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya kisiasa na tamaduni za Kiarabu katika Andalusia' 'Historia ya Uislamu kuanzia mwanzo wake hadi katikati ya karne ya 19' na 'Tamaduni za mavazi ya Kiislamu.' Reinhart Dozy alifariki dunia mwaka 1883.

Reinhart Dozy

Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia.

Vita vya Verdun

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.

Jamal Abdul-Nasser na rais wa wakati huo wa Syria wakisaini hati ya muungano wa Kiarabu

Na siku kama ya leo 55 iliyopita, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu.

Malcolm X