Jumatano, tarehe 26 Februari, 2020
Leo ni Jumatano tarehe Pili Rajab 1441 Hijria sawa na tarehe 26 Februari 2020.
Siku kama ya leo miaka 1220 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Ibn Rumi, malenga mashuhuri wa Kiarabu mjini Baghdad, Iraq. Alianza kusoma elimu ya awali kwa baba yake akiwa kijana mdogo, na baadaye akasoma kwa walimu wakubwa wa enzi zake. Aidha alipata kujifunza elimu za zama zake kama vile fasihi na mashairi. Ibn Rumi alikuwa akisoma sana mashairi ya kumsifu Imam Hassan Askari, mmoja wa Ahlubaiti wa Mtume (saw) kutokana na mapenzi yake makubwa aliyokuwanayo kwa watu wa familia ya Mtume wa Allah (as). Malenga huyo alifariki dunia mwaka 283 Hijiria.
Katika siku kama ya leo miaka 1001 iliyopita, alifariki dunia Abu Raihan Biruni msomi, mnajimu na mwanahisabati mkubwa wa Kiirani huko katika mji wa Ghazne katikati mwa Afghnaistan ya sasa. Abu Raihan Biruni alikuwa hodari katika elimu za historia, jiografia na hisabati, tiba na utengenezaji wa dawa. Akiwa safarini nchini India, msomi huyo wa Kiirani alikutana na kufanya mijadala na maulama na watawala wa zama hizo. Abu Raihan alikusanya taarifa muhimu alizokuwa akizihitaji kwa ajili ya kuandika kitabu chake alichokiita 'Tahqiq Ma Lilhind' baada ya kujifunza lugha ya Sanskriti yaani lugha ya Kihindi ya kale. Katika kitabu hicho, Abu Raihan ameandika taarifa muhimu kuhusu sayansi, itikadi, mila na desturi za Wahindi. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingine vingi kuhusu elimu ya nujumu, mantiki na falsafa.
Tarehe 26 Februari miaka 218 iliyopita yaani mwaka 1802 alizaliwa mshairi na mwandishi mashuhuri Mfaransa, Victor Hugo. Alikuwa akitetea uhuru na usawa kwa ajili ya matabaka ya watu wote masikini. Hugo alikubaliwa kujiunga na chuo kikuu na wakati huo huo akawa mwanachama wa Baraza la Kutunga Sheria akiwa na umri wa miaka 25. Kutokana na upinzani wake dhidi ya utawala wa ukandamizaji wa Napoeleon wa Tatu alilazimika kuachana na masuala ya siasa na akaishi uhamishoni kwa kipindi cha miaka 20. Katika kipindi hicho Hugo aliandika vitabu muhimu na vya thamani. Miongoni mwa vitabu hivyo ni "Watu Masikini," "The Hunchback of Notre-Dame," " The Man Who Laughs" na "Toilers of the Sea". Victor Hugo alifariki dunia mwaka 1885.
Miaka 99 iliyopita siku kama ya leo kulisainiwa mkataba wa urafiki baina ya Iran na Russia ya zamani. Katika mkataba huo ambao ulisainiwa baada ya miaka minne ya mapinduzi ya Muungano wa Sovieti ya zamani, Moscow ilitangaza kwamba, haitaendelea na siasa za kikoloni dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa kifungu hicho muungano huo wa Sovieti uliacha kutekeleza mikataba ya huko nyuma iliyokuwa inaidhuru Iran. Katika mkataba huo wa urafiki, Moscow ilitangaza kuwa haiitambui mikataba yote iliyowekwa na utawala wa tatu wa Tzar dhidi ya Iran. Hata hivyo Urusi ya zamani haikuipatia Iran ardhi za Caucasia na Turkmenistan zilizopo Kaskazini Magharibi na Mashariki mwa Iran. Aidha katika mkataba huo Iran iliahidi kutoruhusu nchi nchi nyingine kutumia ardhi yake dhidi ya Urusi.
Na miaka 64 iliyopita siku kama ya leo mwaka 1334 Hijiria Shamsia, alifariki dunia mtaalamu wa fasihi na malenga mkubwa wa Iran, Allamah Ali-Akbar Dehkhoda. Alizaliwa mjini Tehran mwaka 1258 Hijiria Shamsia na akawa miongoni mwa wanafunzi wa awali wa chuo cha zamani cha siasa mjini Tehran. Baada ya kukamilisha masomo yake ya awali Dehkhoda alikwenda Ulaya na kufanya utafiti kwa miaka 5. Alirudi Iran katika kipindi cha kuchipua fikra za kupigania uhuru, kipindi ambacho alikitumia kufanya kazi za kishairi dhidi ya utawala wa wakati huo. Kazi kubwa zaidi ya msomi huyo ni kamusi maarufu ya Dehkhoda.