Alkhamisi tarehe 27 Februari 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Rajab 1441 Hijria inayosadifiana na Februari 27 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1187 iliyopita yaani mwaka 254 Hijria, Imam Ali Naqi al-Hadi AS mmoja wa wajukuu wa Mtume Muhammad SAW aliuawa shahidi. Alizaliwa mwaka 212 katika mji mtakatifu wa Madina. Alikua na kulelewa chini ya uangalizi wa baba yake, yaani Imam Jawad AS. Imam Ali al-Hadi alichukua jukumu la kuongoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi baba yake. Imam Ali al Hadi alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufundisha, kulea wanafunzi na kueneza mafunzo sahihi ya dini tukufu ya Uislamu. Mapenzi ya watu kwa Imam Hadi kwa upande mmoja na elimu aliyokuwa nayo kwa upande wa pili, ni mambo yaliyowafanya watawala wa wakati huo wa ukoo wa Bani Abbas waingiwe na husuda, na ndio maana wakapanga njama za kumuua shahidi mjukuu huyo wa Mtume (saw) na kuitekeleza katika siku kama ya leo.
Tarehe 27 Februari miaka 118 iliyopita alizaliwa mwandishi wa riwaya wa Kimarekani, John Steinbeck katika jimbo la California. Alijiunga na chuo kikuu akiwa na umri wa miaka 17 na kuacha masomo kabla ya kupata shahada yake. Katika kipindi cha ujana wake alijishughulisha na kazi mbalimbali kabla ya kuchagua kazi ya uandishi. Kitabu cha kwanza cha riwaya cha mwandishi huo ni Cup of Gold akichokiandika akiwa na umri wa miaka 27. Mashaka ya kimaisha yalimtayarishia John Steinbeck mazingira mazuri ya kueleza kwa ufasaha maisha ya watu dhaifu na maskini katika jamii ya Marekani. Alikuwa hodari mno katika kueleza mandhari tofauti, matukio na hali mbalimbali. Steinbech ameandika vitabu vingi kama Of Mice and Men, Bombs Away, Travels with Charley, East of Eden, A Russian Jornal na Burning Bright.
Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, alifariki dunia Waziri Mkuu wa zamani wa Uturuki Necmettin Erbakan (Najmuddin Erbakan) akiwa na umri wa miaka 84. Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Istanbul, Erbakan alijiunga na Chuo Kikuu cha Aachen nchini Ujerumani ambako alipata shahada ya uzamivu. Mwaka 1969 Erbakan aliingia katika uwanja wa siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge. Mwaka 1987 aliongoza chama chenye mielekeo ya Kiislamu cha Refah ambacho kilipata viti vingi vya bunge na kumteuwa kuwa Waziri Mkuu mwaka 1996. Tukio hilo liliwakasirisha mno wanasiasa wa kilaiki wa Uturuki, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Serikali ya Erbakan ilipigwa vita na jeshi la Uturuki na miezi 10 baadaye chama cha Refah kilivunjwa na wanajeshi, na mwanasiasa huyo akapigwa marufuku kujishughulisha na masuala ya kisiasa kwa kipindi cha miaka 5. Profesa Necmettin Erbakan anatambuliwa kuwa baba wa harakati ya Kiislamu ya Uturuki.
Katika siku kama hii ya leo miaka 4 iliyopita aliaga dunia mtengezaji filamu mashuhuri wa Iran, Farajullah Salahshur. Alizaliwa mwaka 1331 Hijria Shamsia katika mji wa Qazvin. Farajullah Salahshur, ametengeneza filamu nyingi maarufu kama ile ya kisa cha Maisha ya Nabii Yusuf (as), kisa cha As’habul Kahf na maisha ya Nabii Ayyub (as). Filamu hizo hasa ile ya kisa cha maisha ya Nabii Yusuf (as) zimewavutia watazamaji wengi duniani. Kabla ya kufariki dunia, Salahshur alikuwa ameshaandika kisa cha filamu ya maisha ya Nabii Musa AS. Uchukuaji filamu ya kisa hicho ulipangwa kuanza miezi michache kabla ya kifo chake, lakini hilo halikuwezekana kutokana na ugonjwa wa saratani ya mapafu ulioishia kwenye kifo chake.