Jumatatu tarehe 9 Machi mwaka 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 14 Rajab 1441 Hijria sawa na Machi 9 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 7 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sayyid Mujtaba Musavi Lari ambaye alikuwa miongoni mwa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1314 Hijria Shamsia katika eneo la Lar nchini Iran na kupata elimu ya msingi katika eneo hilo. Mwaka 1332 alielekea Qum kwa ajili ya elimu ya juu ya Kiislamu. Huko Qum, Ayatullah Musavi Lari aliasisi Kituo cha Kueneza Maarifa ya Kiislamu Duniani ambacho kilikuwa kikisambaza vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha hai za dunia. Mwaka 1372 Hijria Shamsia Academia ya Sayansi ya Jamhuri ya Azarbaijan ilimtunuku shahada ya uzamivu kutokana na taathira kubwa ya vitabu vyake vilivyotarjumiwa kwa lugha ya Kirusi. Ayatullah Mujtaba Lari aliaga dunia siku kama ya leo tarehe 19 Esfand katika Hospitali ya Imam Ridha (as) baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa kipindi kirefu.
Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sheikh Muhammad Ghazali mwanazuoni na mwanamageuzi mkubwa wa Misri. Alizaliwa mwaka 1917 huko nchini Misri. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, tayari Muhammad Ghazali alikuwa amehifadhi Qur'ani Tukufu yote. Muhammad Ghazali alihitimu Chuo Kikuu akiwa na umri wa miaka 24. Fikra zake zilijengeka juu ya msingi wa mageuzi ya maarifa ya kidini, kukurubisha baina ya madhehebu za Kiislamu na kupinga fikra za kikaumu. Muhammad Ghazali aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 79 kwa mshtuko wa moyo na kuuzikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina.
Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita Menachem Begin mmoja wa waasisi wa utawala haramu wa Kizayuni na chama cha mrengo wa kulia cha Likud aliangamia. Begin alizaliwa huko Russia mwaka 1913 na baba yake ambaye alikuwa Mzayuni mwenye misimamo mikali alikuwa na taathira na nafasi kubwa katika malezi yake. Akiwa na umri wa miaka 12, Menachem Begin aliasisi kikosi cha vijana wa Kizayuni na miaka miwili baadaye baada ya kuhajiri huko Palestina mwaka 1942 akachaguliwa kuwa kamanda wa Taasisi ya kigaidi yenye misimamo ya kufurutu ada. Taasisi hiyo ilikuwa moja kati ya makundi makuu ya kigaidi na yenye misimamo mikali ya Kizayuni iliyoshiriki kwa kiasi kikubwa katika kuwauwa raia wa Palestina na kuwafukuza katika ardhi zao.
Miaka 566 iliyopita sawa na tarehe 9 mwezi Machi mwaka 1454 alizaliwa mvumbuzi na baharia wa Kiitalia kwa jina la Americo Vespucci. Vespucci alijishughulisha na kazi za melini kutokana na hamu yake kubwa ya kupenda ubaharia aliyoionyesha tangu akiwa kijana na hivyo kupewa cheo cha unahodha. Baharia Americo Vespucci alisafiri mara nne katika nchi isiyojulikana ambayo hadi wakati huo ilikuwa haina jina na baadaye ikapatiwa jina la mvumbuzi huyo wa Kiitalia yaani Amerika.