Mar 15, 2020 23:02 UTC
  • Jumatatu tarehe 16 Machi 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 21 Rajab 1441 Hijria sawa na tarehe 16 Machi mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1193 iliyopita mwezi wa Rajab mwaka 284 Hijiria, alifariki dunia Abu Hatam, Sahal bin Muhammad Sajestani. Abu Hatam alikuwa ametabahari katika elimu ya Qur'ani, hadithi, fasihi na mashairi. Mbali na kuwa alikuwa akiisoma Qur'ani Tukufu na kuifundisha kwa mapenzi makubwa, Abu Hatam pia alijishughulisha na masuala ya kijamii. Msomi huyo ameacha vitabu vingi miongoni mwavyo ni I'irabul Qur'an', na Akhlaqul Insan.

Katika siku kama ya leo miaka 161 iliyopita Alexander Stepanovich Popov, mvumbuzi na mwanafizikia wa Russia alizaliwa. Baada ya kuhitimu masomo katika taaluma ya fizikia, alianza kujishughulisha na ufundishaji katika vyuo vikuu vya nchi hiyo. Mbali na shughuli hiyo, Popov aliendelea mbele na utafiti wake katika nyanja mbalimbali za kielimu ambapo baadaye alifanikiwa kuvumbua chombo cha kunasia sauti na kukipa jina la kinasia sauti. Aliaga dunia mwaka 1906.

Miaka 81 iliyopita katika siku kama ya leo, katika hali ambayo Vita vya Pili vya Dunia havikuwa vimeanza, nchi ya Czechoslovakia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Ujerumani ya Kinazi. Kwa utaratibu huu, Jamhuri ya Czechoslovakia ikawa nchi ya pili baada ya Austria kukaliwa kwa mabavu na Adolph Hitler. 

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi mwaka 1909.

Bi Selma Lagerlof

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, Kamal Fouad Jumblatt mwanasiasa mahiri wa Lebanon aliuawa.  Alizaliwa Disemba 6 mwaka 1917 huko Moukhtara kusini mwa Beirut. Mwaka 1952 na kuendelea, Kamal Fouad Jumblatt  alikuwa mwanasiasa wa mrengo wa upinzani na akafanikiwa kumuondoa madarakani Bechara El Khoury Rais wa muda wa wakati huo wa Lebanon. Hatimaye Kamal Fouad Jumblatt  aliuawa na wapinzani wake katika siku ma ya leo  akiwa na umri wa miaka 60. 

Kamal Fouad Jumblatt 

Katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsiya aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Sayyid Ahmad Khomeini