Ulimwengu wa Michezo, Machi 16
SPOTI, MACHI 16
Hujambo mpenzi msikilizaji wa RT na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri kitaifa na kimataifa ndani ya siku saba zilizopita….nakusihi tuandame sote hadi tamati ya kipindi…….karibu……
Corona yazidi kuvuruga ratiba za spoti
Zimwi la Corona limeendelea kuusakama ulimwengu wa michezo huku virusi hivyo vikiendelea kusambaa kama moto wa kichaka na kuua. Ratiba za ligi, michezo na mechi mbali mbali duniani zimefutwa kabisa au kuakhirishwa kutokana na virusi hivyo. Hapa nchini Iran, ligi na michezo yote imesimamishwa ili kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa huo wa Covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo. Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, Masoud Soultanifar amesema michezo na michuano yote hapa nchini imeakhirishwa hadi Aprili 20. Awali wizara hiyo ilikuwa imesimamisha shughuli za michezo hapa nchini hadi Aprili 2.

Wakati huohuo, uchaguzi wa Baraza Kuu la Shirikisho la Soka la Iran FFIRI umeakhirishwa. Uchaguzi huo ambao ulikuwa ufanyike Jumapili hii ya Machi 15 sasa utafanyika katika terehe mpya itakayotangazwa na Bodi Kuu ya Uongozi wa shirikisho hilo. Tayari Shirikisho la Soka Duniani FIFA, lilikuwa limeliagiza Shirikisho la Soka la Iran kuakhirishwa uchaguzi huo hadi pale Bodi Kuu ya Uongozi wa shirikisho hilo itakapoangalia upya sheria zake za sasa. FIFA imesema sheria za sasa zina kasoro kadha wa kadha, ikiwemo hatua ya serikali ya kuingilia uchaguzi wa shirikisho hilo. Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran amesema anatumai FIFA itaridhia kufanyika uchaguzi huo hapo baadaye, kwa kuwa hivi sasa Iran inakabiliana na mripuko wa virusi vya Corona.
Kwengineko, Waziri Mkuu nchini Italia Giuseppe Conte amesaini pendekezo la kamati ya Olimpiki nchini Italia la kutaka michezo yote Italia ikiwemo ligi ya Serie A kusimama kwa muda kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona. Ligi Kuu ya Italia Serie A imesimamishwa hadi April 3 2020. Huku hayo yakijiri, Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) imepata pigo kubwa baada ya kubainika kuwa Kocha wa klabu ya Arsenal Mikel Arteta na mchezaji wa Chelsea Callum Hudson Odoi wameambukizwa virusi vya Corona. Kocha wa Arsenal Alkhamisi alipimwa na kubainika kuwa ameambukizwa virusi hivyo na kwa msingi huo mechi kati ya timu yake na Brighton iliyotarajiwa kuchezwa wikiendi iliakhirishwa. Arteta ametuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na kusema ''Hii kwa kweli inasikitisha.'' Niliamua kupimwa baada ya kujihisi vibaya lakini nitarudi kazini mara tu nitakaporuhusiwa kufanya hivyo''. Klabu za Arsenal, Bournemouth, Chelsea, Everton, Leicester, Manchester City, Watford na West Ham United zimeshuhudia angalau mchezaji ama afisa akitengwa ili kudhibiti uenezaji wa ugonjwa huo wa COVID-19.

Mechi zote za Ligi Kuu sasa zimeahirishwa hadi Aprili 4. Mkutano wa dharura uliandaliwa Ijumaa ambapo klabu zote za EPL ziliamua kwamba mechi zisukumwe mbele kwa majuma matatu, baada ya vikosi vya Arsenal, Chelsea na Everton kuwekwa katika karantini ili kuzuia maambukizi. Wakati huohuo, klabu ya Juventus imetangaza kuwa mchezaji wake, Daniele Rugani amekutwa na maambukizi ya virusi vya Corona. Klabu hiyo ya ligi ya Serie A imesema kwamba imechukua hatua zote za kumtenga mchezaji huyo zinazohitajika kisheria ikiwemo kuwashirikisha wale ambao waligusana naye.
Kadhalika Shirikisho la Mpira wa Vikapu (NBA) nchini Marekani limesitisha mashindano yake msimu huu baada ya mchezaji wa timu ya Uttah Jazz kukutwa na maambukizi ya virusi vya korona. NBA imesema itatumia muda huu kutathmini hatua za kufuata kuhusuana na mlipuko wa virusi hivyo.
Japan yaendelea na maandalizi ya Olimpiki
Wakati dunia ikiwa katika juhudi za kupambana na virusi hatari vya Corona, Tokyo yaendelea na mandalizi ya mashindano ya Olimpiki, licha ya Shirikisho la Afya Duniani WHO kutangaza rasmi kuwa virusi vya Corona ni janga la kimataifa. Japan imesema itaendelea na maandalizi yake ya michezo ya olimpiki na ile ya michezo ya Olimpiki kwa walemavu kama ilivyopangwa hapo awali hata baada ya WHO kutangaza rasmi kuwa virusi vya corona ni janga la kimataifa. Wajumbe wa kamati ya mandalizi ya Tokyo pia wamesema kuwa mashindano ya Olimpiki yatafanyika kama ilivyopangwa. Takribani wanariadha 11,000 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo yanayotazamiwa kufanyika katikati ya mwaka.
Rwanda yaandika barua ya kujiondoa Afcon
Serikali ya Rwanda imeamua kuchukua tahadhari mapema kuhusiana na mlipuko wa virusi vya Corona ambavyo vimeingia katika baadhi ya nchi. Rwanda imeamua na kufikia maamuzi ya kutangaza kutoshiriki fainali za michuano ya CHAN mwaka huu 2020 nchini Cameroon zinazotarajiwa kuanza April 4, lakini pia na mechi za kuwania kufuzu michuano ya AFCON mwaka ujao 2021. Fainali hizo za Cameroon zinatia hofu kutokana na nchi hiyo kuthibitisha kuwa na wagonjwa kadhaa wa corona.
Soka U-16, Tanzania yaibanjua Liberia
Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 16 imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Liberia katika mchezo wa fainali wa michuano maalumu ya kimataifa ya vijana yaliyofanyika nchini Tanzania. Katika mchezo huo wa fainali ambao ulipigwa katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Tanzania iliibanjua Liberia mabao 3-2. Mashindano hayo yamejumuisha washiriki watatu ambao ni Tanzania (mwenyeji), Liberia na Malawi.
Timu hiyo ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 16 ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Liberia katika mchuano wa awali wa mashindano hayo maalumu mataifa matatu yaliyoandaliwa na Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF. Kocha mkuu wa timu hiyo alisema alitarajia matokeo hayo kwa kuwa aliwaandaa vijana wake vya kutosha. Timu ya vijana chini ya umri wa miaka 16 inaandaliwa kwa ajili ya kushiriki fainali za Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zitakazofanyika mwaka ujao 2021, nchini Morocco.
Huku hayo yakijiri, timu ya taifa ya wasichana chini ya umri wa miaka 17 ya Tanzania wikendi ilikubali kichapo cha mabao 5-0 na wenyeji, Uganda kwenye mchezo wa marudiano kufuzu Fainali za Kombe la Dunia Uwanja wa Lugogo Jijini Kampala hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 6-2 kufuatia kushinda 2-1 kwenye mechi ya kwanza Machi 1 nyumbani, Dar es Salaam. Kocha wa timu ya taifa ya wanawake (U17) Bakari Shime, amekubali matokeo lakini ametilia shaka umri wa baadhi ya wachezaji wa Uganda waliocheza kwenye mchezo huo. Katika mchezo wa awali, timu hiyo ya taifa ya soka ya Tanzania ya wanawake wenye chini ya miaka 17, iliichabanga Uganda kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Sasa Uganda imefuzu moja kwa moja fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kuanzia Novemba 2 hadi 21 nchini India.
Cecafa yapata bosi mpya
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limemtangaza Auko Gacheo kuwa Afisa Mkuu Mtandaji wa baraza hilo, kurithi mikoba ya Nicolas Musonye wa Kenya aliyemaliza muda wake.

Cecafa inaundwa na nchi wanachama 12 ambao ni Uganda, Somalia, Kenya, Rwanda, Burundi, Djibout, Eritrea, Ethiopia, Tanzania Bara, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar. Mwenyekiti wa Cecafa, Wallace Karia amesema Gacheo amekidhi vigezo vinavyohitajika vya kuvaa viatu vya Musonye.
Dondoo za Hapa na Pale
Klabu ya Liverpool ingali inawaza na kukuna kichwa baada ya kubanduliwa kwenye kipute cha Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA Champions League). Hii ni baada ya timu hiyo kuchabangwa mabao 3-2 uwanjani Anfield usiku wa Jumatano, na kuyaaga mashindano hayo ya kifahari kwa kushindwa kwa jumla ya mabao 4-2. Mabingwa hao watetezi walikuwa wamepoteza 1-0 katika mkondo wa kwanza mjini Madrid, mnamo Februari 18. Liverpool sasa wameshuhudia ndoto yao ya kutetea taji la UEFA na pia kuwania makombe ya FA na Carabao ikizimwa ndani ya siku 12. Wamesalia katika shindano moja pekee msimu huu, Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza (EPL), ambako wanaselelea kileleni wakiwa na nafasi kubwa kutawazwa mabingwa kwa mara ya kwanza katika miaka 30.
Mbali na hayo, mchezaji nyota wa klabu ya soka ya Barcelona ya Hispania Lionel Messi ametoa mamilioni ya yuro ili kumtoa rumande mchezaji nyota wa zamani wa Brazil na Barcelona Ronaldinho Gaucho. Nyota huyo wa soka wa zamani wa Brazil, alihukumiwa kifungo cha miezi 6 jela alichohukumiwa nchini Paraguay kwa makosa ya kujaribu kuingia nchini humo na paspoti bandia. Mahakama nchini Paraguay ilifanya uamuzi wa kumshikia Ronaldinho na kaka yake Roberto de Assis Moreira kutokana na wawili hao kujaribu kuingia nchini humo wakiwa na hati bandia za kusafiria. Lionel Messi amejitolea kumsaidia Ronaldinho ambaye ni rafiki yake na mnasihi wake.

Nyota wa Arjentina amejitolea kulipa madeni yote ya Ronaldinho na kisha kumtoa gerezani. Kwa mujibu wa habari iliyotolewa na vyombo vya habari vya Uhispania, Messi amelipa kiasi cha yuro milioni 4 kulipia gharama za timu ya mawakili watakaosaidia kumtoa rafiki yake waliokuwa wakicheza timu moja katika gereza analoshikiliwa. Ronaldinho anadaiwa takribani Euro milioni 9 nchini Brazil, kiasi ambacho inasemekana Messi pia atakilipa. Ronaldinho na kakaye walikamatwa na Polisi nchini Paraguay Machi 6 kwa kosa la kutumia paspoti feki kuingia nchini humo. Mchezaji huyo alikwenda Paraguay kwa ajili ya uzinduzi wa kitabu na kampeni kuhusu watoto wanaoishi kwenye mazingira duni.
………………….TAMATI……………..