Ijumaa tarehe 20 Machi mwaka 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 25 Rajab 1441 Hijria sawa na Machi 20 mwaka 2020.
Leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1399 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani maarufu kwa jina la Sikukuu ya Nowruz. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni pamoja na Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi tarehe Mosi Farvardin kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

Siku kama ya leo miaka 1258 iliyopita, Imam Musa Kadhim (as) mmoja wa wajukuu watoharifu wa Mtume Mtukufu (saw) aliuawa shahidi. Imam Kadhim (as) alizaliwa mwaka 128 Hijiria huko katika eneo la Ab'waa lililoko baina ya miji mitakatifu ya Madina na Makka. Mtukufu huyo kwa miaka 20 alipata malezi na elimu muhimu kutoka kwa baba yake ambaye ni Imam Jaafar as-Swadiq (as). Baada ya kuuawa baba yake huyo, Imam Kadhim (as) alipata fursa ya kuuongoza umma wa Kiislamu kwa muda wa miaka 35, ambapo alipata mateso na mashaka mengi katika njia hiyo. Katika zama zake ambazo zilisadifiana na ustawi mkubwa wa utamaduni na elimu ya Kiislamu pamoja na kuimarishwa uhusiano na mataifa ya kigeni, Imam alifanya juhudi kubwa za kueneza mafunzo ya Kiislamu katika mataifa hayo kupitia wanafunzi wake. Mbali na hayo, Imam pia aliendesha mapambano makali dhidi ya watawala dhalimu wa Bani Abbas. Hatimaye Haroun ar-Rashid kutoka ukoo wa Bani Abbas aliyehofia sana kuporomoka kwa utawala wake, alimfunga jela Imam Kadhim (as). Licha ya kufungwa jela lakini Imam (as) hakusimamisha shughuli zake za kuhubiri dini na kupambana na madhalimu bali alifundisha na kuwaelimisha watu waliokuwa pembeni yake hali halisi ya mambo iliyotawala katika zama hizo. Hatimaye Haroun ar-Rashid alifanya njama ya kumuua Imam kwa kumpa sumu. Huku tukitoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kuuawa shahidi Imam Kadhim (as), tunakunukulieni hapa moja ya semi zake zenye mafunzo na busara kubwa. Imam anasema: 'Njia bora zaidi ya kumkurubia Mwenyezi Mungu baada ya kumjua ni kusimamisha swala, kuwatendea wema wazazi wawili na kuachana na husuda na majivuno.'

Tarehe 20 Machi miaka 293 iliyopita, alifariki dunia Isaac Newton mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza akiwa na umri wa miaka 84. Alizaliwa mwaka 1643 na kusoma katika Chuo Kikuu cha Cambridge. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy.
Miaka 64 iliyopita katika siku kama ya leo muwafaka na tarehe 20 Machi 1956, nchi ya Tunisia iliyoko katika eneo la kaskazini mwa Afrika ilijipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ijapokuwa harakati za ukombozi nchini humo zilianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, lakini kutokea Vita vya Pili vya Dunia na kudhoofika Ufaransa kwenye vita hivyo, kuliandaa mazingira mazuri ya kujikomboa nchi hiyo. Baada ya kujipatia uhuru, Habib Bourguiba aliongoza nchi hiyo, kwa karibu miongo mitatu lakini kwa mabavu na ukandamizaji. Baada ya utawala wa Bourguiba, nchi hiyo ilitawaliwa na Zainul Abidin Ben Ali ambaye aliingia madarakani mwaka 1982. Kiongozi huyo naye alifuata mbinu na mwendo uleule wa Bourguiba wa kuwakandamiza wananchi na kupiga vita Uislamu, suala lililopelekea wananchi wa nchi hiyo kusimama kidete na kumng'oa madarakani mwezi Januari mwaka 2011.