Apr 06, 2020 07:36 UTC
  • Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (5)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu.

 

Katika kipindi chetu kilichopita tulianza kumzungumzia alimu  na msomi mtajika Abu Ja'far Muhammad ibn 'Ali ibn Babawayh al-Qummi ambaye ni maarufu kwa lakabu ya Sheikh Saduq kutokana na utunzaji wake mkubwa wa amana na uaminifu katika kunakili hadithi. Tulibainisha hima na juhudi kubwa ialiyoifanywa kwa ajili kukusanya hadithi kuanzia mashariki hadi magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu na hivyo kupelekea kupatikana sehemu muhimu na isiyo na mithili ya dafina ya maarifa ya Ahlul-Baiti (as).

Pia tulisema kuwa, Sheikh Saduq alifanikiwa kualifu vitabu 300 katika maudhui mbalimbali ambapo kitabu chake cha Man La Yahdhuruh al-Faqihi kina nafasi maalumu na ni moja ya vitabu vinne vya hadithi vya Waislamu wa Kishia vinavyojulikana kama Kutub al-Arba'a. Sehemuu ya tano ya mfululizo huu juma hili itaendelea kumzungumzia mwanazuoni huyu mtajika. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.

 

Katika utamaduni wa Kiislamu maneno yanayonukuliwa kutoka kwa Mtume (saw) na Maimamu Maasumu (as) kutoka katika kizazi chake huitwa 'hadithi'. Baada ya Qur'ani Tukufu, daima hadithi zimekuwa na nafasi kubwa kwa Waislamu kuifahamu dini yao na hadithi zimekuwa ndizo zinazofasiri Kitabu cha Mwenyezi Mungu yaani Qur'ani Tukufu. Katika Aya zake nyingi, Qur'ani Tukufu imebainisha mambo kwa sura jumla ambapo ubainishaji wa kina na wa ndani ameachiwa Bwana Mtume (saw) na Mawasii wake baada yake. Katika Aya ya 44 ya Surat Nahal Mwenyezi Mungu anasema:

بِالْبَیِّنَاتِ وَالزُّبُرِ وَأَنزَلْنَا إِلَیْکَ الذِّکْرَ لِتُبَیِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَیْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ یَتَفَکَّرُونَ

Kwa Ishara wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, wapate kufikiri.

Mtume (saw) na Maimamu Maasumu (as) walikuwa wakiwashajiisha Waislamu kujifunza, kuhifadhi, kukumbuka na kueneza hadithi. Ni kwa msingi huo ndio maana inafahamika zaidi nafasi ya hadithi sahihi na umuhimu wake. Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq (as) amenukuu kutoka kwa baba yake yaani Imam Muhammad Baqir (as) ya kwamba amemwambia: Mwanangu! Ijue daraja ya Mashia kupitia kiwango cha kunukuuu na kufahamu kwao hadithi, kwani ukweli, utambuzi na maarifa yapo katika kufahamu na kudiriki hadithi. Ni kwa udiriki huu ambapo Muumini hufikia daraja ya juu kabisa ya imani (ufahamu wa kiitikadi na kivitendo).

 

Kitabu cha Man La Yahdhur al-Faqih (من لایحضره الفقیه) ndicho kitabu mashuhuri zaidi na kikubwa zaidi miongoni mwa vitabu vya Sheikh Saduq baada ya kitabu cha Madinat al-Ilm. Kitabu cha Madinat al-Ilm kina thamani kubwa. Hata hivyo inasikitisha kuwa, kitabu hiki kilipotea karne kadhaa zilizopita. Pamoja na hayo wasifu wa kitabu cha Madinat al-Ilm cha Sheikh Saduq umekuja katika baadhi ya vitabu mashuhuri na Maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu wamenufaika na matilaba pamoja na maudhui za kitabu hicho katika vitabu vyao.

Katika kipindi cha karne 12 kitabu cha Man La Yahdhuruh al-Faqih kimekuwa moja ya vitabu vinne vikuu vya hadithi kwa Waislamu wa Kishia. Kitabu hiki kina majmui ya hadithi 6,000 ambazo zimegawanywa mafungu mafungu na kwa mujibu wa mas'ala mbalimbali ya kifiqihi.

Sheikh Saduq anasema kuhusiana na kitabu hiki kwamba: Kitabu hiki kimeandikwa kwa ajili yya Fiqihi, masuala ya halali na haramu, sheria na kanuni za Mwenyezi Muungu, kiasi kwamba, nimeandika mambo yote yanayohusiana na masuala mbalimbali ya Kifiqihi kama kuanzia tohara hadi dia (hukumu za fidia), na kitabu hiki cha Man La Yahdhuru al-Faqif ni kwa ajili ya mtu ambaye mbele yake au karibu yake hakuna fakihi (hana msomi wa elimu ya fiqihi karibu yake ili amuulize)…. Makusudio ya kuuandika kitabu hiki ni kuwa, nilitaka kuleta zile hadithi ambazo zinatoa fatuwa na ambazo nina uhakika na ukweli wake kwamba, zimetoka kwa Maasumina (as).

 

 

Wapenzi wasikilizaji hadi sasa kumeandika vitabu 23 vya kusherehesha na kubainisha kitabu hiki cha Sheikh Saduq, ingawa la kusikitisha ni kuwa, kuna nakala moja tu tena ya maandishi ya mkono. Miongoni mwa vitabu mashuhudi vilivyoandikwa kusherehesha kitabu cha Man La Yahdhuruh al-Faqih ni Rawdhat al-Mutaqin cha Allama Majlsi. Kitabu cha Man La Yahdhuruh al-Faqih kimejumuisha masuala mengi kama aina za maji, tohara na najisi, mambo ya wajibu kwa Swala, mambo ambayo ni utangulizi wa ibada ya Swala kama, udhu, kuoga, kutayamamu, hukumu za maiti, hukumu za Swala, hukumu za utoaji hukumu, hukumu za machumo, hukumu za ndoa, hukumu za mirathi na mambo mengine ya kifiqihi.

Mbinu ya uandishi wa kitabu cha Man La Yahdhuruh al-Faqih ni mtindo ambao ulikuwa umeenea katika karne za kwanza za Uislamu ambapo mafaqihi na wanazuoni wa fiqihi walikuwa wakitosheka tu na kunukuu hadithi na maneno ya Maimamu (as).

Baada ya kipindi hicho, yaani kuanzia zama za Sheikh Mufid ambaye ni mwanafunzi bora kabisa miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Saduq, taratibu mtindo huu ukaanza kubadilika.

Kitabu cha Rawdhat al-Mutaqiin ambacho ni sherehe ya Kitabu cha Man Laa Yahdhuruh al-Faqih

 

Hilo lilitokana na kubadilika mahitaji ya zama katika upande mmoja na kuibuka hujuma na ukosoaji wa wapinzani na maadui wa Uislamu sambamba na kuingia falsafa ya Kigiriki katika ulimwengu wa Kiislamu kwa upande wa pili. Kuibuka masuala mapya ya kiitikadi ilikuwa ni lazima kwa Maulamaa wa Kiislamu kujitokeza na kutoa majibu ya maswali.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati. Kipindi chetu kijacho kitabainisha maktaba ya Kifiqihi ya Sheikh Saduq. Hadi tutakapokutana hiyo wiki ijayo, ninakuageni nikikutakieni usikilizaji mzuri wa vipindi vyetu vingine.

Wasslaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.