Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (6)
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki huwatambulisha Maulamaa wakubwa wa Kishia na kuzbainisha mchango wao ka
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki ambacho huwatambulisha Maulamaa wakubwa wa Kishia na kubainisha mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao. Vipindi vyetu viwili vilivyotangulia vilimzungumzia Sheikh Abu Ja'far Ali bin Babawayh al-Qummi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikh Saduq, mmoja wa maulama wakubwa katika historia ya Ushia katika karne ya nne Hijria. Mafakihi na wasomi wakubwa wa Kiislamu walikuwa wakimuita Sheikh Saduq kwa lakabu ya Rais al-Muhadithin (Kiongozi wa Wapokezi wa Hadithi), kwani alikuwa na mahiri na stadi katika kuzitambua hadithi pamoja na vyanzo vyake kama ambavyo alifanya hima na juhudi kubwa katika kuzikusanya hadithi na kuziweka katika mafungu na mpangilio kwa mujibuu wa maudhui zake. Sehemu hii ya sita ya mfululizo huu wa Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu juma hili itaendelea kumzungumzia Sheikh Saduq. Kuweni name hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio yale niliyokuandalieni kwa leo.
Kwa hakika Sheikh Saduq hakuwa alimu na mtaalamu wa hadithi tu, bali alikuwa msomi na mwanachuoni aliyekuwa amebobea pia katika fani na elimu mbalimbali kama fikihi, teolojia na tafsiri. Licha ya kuwa jina la Sheikh Saduq daima hukumbusha kitabu cha hadithi chenye thamani kubwa cha Man Laa Yahdhuruh al-Faqih, lakini mwanazuoni huyu mkubwa wa Kishia amesanifu na kuandika vitabu takribani 300 vingine vya kidini ambavyo vinazungumzia maudhui tofauti kama masuala ya kiitikadi, teolojia, tafsiri na kadhalika. Aidha midahalo ya Sheikkh Saduq na wanazuoni wakubwa wa madhehebu nyingine ni mambo yanayoonyesha ni jinsi gani mwanazuoni huyu alikuwa ametabahari na kubobea katika elimu ya teolojia na itikadi.
Wanazuoni wengi wakubwa wanamtambua Sheikh Saduq kama mutakallim yaani mwanateolojia mahiri na stadi ambapo kutokana na mahitaji ya zama zake aliweza kuchukuua hatua ya kukusanya hadithi. Katika kipindi hicho Sheikh Saduq alifanya hima ya kujibu shubha na utata kuhusiana na itikadi ya Imam Mahdi (atfs) katika kitabu chake cha Kamaaluddin wa Tamaamun Ni'mah kupitia hadithi. Sheikh Saduq ameandika katika utangulizi wa kitabu hicho kama ifuatavyo:
Mimi ninashuhudia kukithiri shubha na utata kuhusiana na Imam wa Zama al-Mahdi (atfs) na ninataka kutoa majibu ya utata huu.
Hata hivyo Sheikh Saduq anatoa majibu ya shubha na utata huo kupitia hadithi mbalimbali. Kwa msingi huo basi, Sheikh Saduq hata katika vitabu ambavyo kidhahiri ni vya kunukuu hadithi anazungumzia maudhui ya teolojia na kutoa mtazamo kwa njia na hoja ya kiakili na nakili kwa ajili ya kuthibitisha itikadi sahihi. Hivyo anatoa hoja za kubatilisha shubha na utata na hatimaye anabainisha mtazamo wake sahihi. Katika uga wa fikihi pia, Sheikh Saduq ametumia njia hii hii.
Maktaba ya fikihi ya Sheikh Saduq inatambulika kama maktaba ya watu wa hadithi. Hata hivyo maktaba ya hadithi kwa Mashia ina tofauti na maktaba ya hadithi kwa Waislamu wa Kisuni na katu hailingani. Hii ni kutokana na kuwa, watu wa hadithi kwa Mashia kinyume na ilivyo kwa Masuni, wao wanaliona suala la Ijtihad katika masuala ya fikihi kuwa ni jambo la dharura na la lazima. Baada ya Sheikh Saduq, mwanafunzi wake yaani Sheikh Mufid alikuja na kuasisi mbinu mpya katika Ijtihad ambayo ilileta uhai na harakati maalumu kwa fikihi ya Kishia.
Sifa nyingine maalumu ya Sheikh Saduq ni juhudi zake kubwa zilizokuwa zimejaa ikhlasi kwa ajili ya kukurubisha madhehebu mbalimbali ya Kiislamu na kuondoa hali ya mtazamo mbaya wa dhehebu fulani kwa dhehebu jingine na ufahamu mbaya wa dhehebu hili kwa dhehebu lile. Licha ya kuwa, Sheikh Saduq alifanya juhudi kubwa zisizochoka kwa ajili ya kutetea itikadi za Kishia na akafanya midahalo mingi sambamba na kualifu vitabu vingi pia katika uga huo, lakini aliyafanya hayo kwa weledi mkubwa ulio mbali na chokochoko na ukufurishaji kiasi kwamba, hakuwa akizijeruhi hisia za madhehebu mengine. Mbali na kuhudhuria masomo kwa walimu wa Kishia, Sheikh Saduq alinufaika pia na walimu wa Kishia kiasi kwamba, kulikuweko na watu waliokuwa wakimpenda ambao hawakuwa wafuasi wa madhehebu ya Shia.

Kwa hakika hatua ya Sheikh Saduq ya kuheshimu madhehebu mengine sambamba na kuyakosoa kielimu na kuona imara itikadi za baadhi ya madhehebu, iliwafanya Maulama wa Kiislamu wa kila madhehebu waisifu shakhsia yake kubwa na aali aliyokuwa nayo. Mbinu hii nzuri inaweza kuwa funzo na somo kwetu sote.
Hatimaye baada ya miaka mingi ya juhudi zisizochoka na hima na idili kubwa katika njia ya kubainisha maarifa na mafundisho ya Kiislamu, Sheikh Saduq msomi mtajika wa Kishia aliaga dunia mwaka 381 Hijria akiwa na umri wa miaka 75 na kuzikwa katika mji wa Rey nchini Iran.
Kunasimuliwa kisa chenye mafunzo baada ya kupita miaka 800 tangu kufariki dunia Sheikh Saduq ya kwamba: Katika zama za utawala wa Fat'h Ali Shah Qajar nchini Iran takribani mwaka 1238 Hijria, kaburi la Sheikh Saduq lililopo katika mji wa Rey, liliharibika kutokana na kunyesha mvua kubwa na likaonyesha tundu. Wakati watu walipokuwa wakilijenga tena kaburi hilo, ghafla wakauona mwili wa Sheikh Saduq ukiwa mzima kabisa kana kwamba, ndio kwanza umetoka kuoshwa.
Baada ya mtawala Fat'h Ali Shah kupata habari hiyo aliondoka haraka na kuelekea katika mji wa Rey na baada ya kushuhudia kiwiliwili cha Sheikh Saduq kilichokuwa kizima kabisa kana kwamba hakikuzikwa kwa mamia ya miaka, alitoa amri kaburi hilo lijengewe kuba. Shakhsia 20 wakubwa wa zama hizo walishuhudia tukio hilo wakiwemo Ayatullah Mullah Rustamabadi na Haj Sayyid Mahmoid Mar'ashi ambaye ni baba wa Ayatullah Mar'ashi Najafi. Kwa hakika tukio hilo lilionyesha adhama na utukufu wa Sheikh Saduq na kulifanya kaburi lake lililopo jirani na Haram ya Shah Abdul Adhim al-Hassan katika mji wa Rey kuwa eneo linalotembelewa na mazuwwar wa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia.
Mpenzi msikilizaji, muda wa kipindi hiki nao naona umenipa mkono, hivyo nalazimika kukomea hapa kwa leo. Hadi tutakapokutana tena wiki ijayo katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachowatambulisha Maulamaa wakubwa wa Kishia pamoja na mchango wao katika Uislamu, ninakuegeni nikikutakieni kila la kheri.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh