Feb 05, 2016 06:38 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo, ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya nane ya mfululizo huu.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa kuchagua viongozi wakubwa wa dini ya Ukristo maisha ya utawa ni ujumbe unaomaanisha kwamba, ni kwa kuipa mgongo dunia na utashi wa nafsi ndipo mtu ataweza kukwea na kufikia daraja za juu za imani na kupata saada na fanaka ya akhera. Kulingana na mafundisho ya Ukristo, dunia ni kitu kibaya; na kuwepo mwanadamu duniani kumetokana na dhambi ya asili ya Nabii Adam (AS); na kwa hivyo kuzipa mgongo starehe na raha za dunia ni jambo bora kwa ajili ya saada na uongofu wa mwanadamu. Mtazamo huo kwa maisha ya kidunia ndio uliosababisha kujitokeza kwa Uprotestanti katika karne ya 16 miladia. Martin Luther, mwasisi wa madhehebu ya Uprotestanti alikuwa hakubaliani na fikra hiyo na akiitakidi kwamba kufunga ndoa na kufaidika na neema za kidunia hakukinzani na kuongoka kwa mwanadamu. Luther alikuwa akisisitiza kuwa lazima makasisi waruhusiwe kuoa.

Japokuwa madhehebu ya Protestanti ilifanya marekebisho na mageuzi katika itikadi za kujitenga na dunia za viongozi wa Kikristo, hadi sasa Wakatoliki na Waorthodoksi wangali wanatilia mkazo juu ya ubora wa maisha ya utawa. Alaa kulli hali fikra hiyo iliendelea kutawala katika ulimwengu wa Kikristo mnamo karne ya 16 bila ya kuwa na mshindani. Ukweli ni kwamba mwenendo huo unakinzana na fitra na maumbile ya mwanadamu na ni kwa sababu hiyo ndio maana makanisa yamekumbwa na vitendo vingi vya utovu wa maadili na ufisadi wa kiuchumi. Vitendo hivyo vya utovu wa kiakhlaqi vingali vinaendelea kushuhudiwa hadi leo hii; na kutokana na kuwepo vyombo vya mawasiliano ya kijamii habari zinazohusiana na vitendo hivyo hata haziweki kufichika. Kiasi kwamba kila baada ya muda na katika hali ya aibu, hata Baba Mtakatifu, yaani Papa mwenyewe amekuwa akithibitisha kujiri kwa vitendo hivyo. Kutawala kwa mitazamo hiyo katika ulimwengu wa Kikristo ilikuwa ni sababu nyengine iliyopelekea kujitokeza kwa fikra ya kuitenganisha dini ya Ukristo na nyanja tofauti za maisha ya watu.

Wapenzi wasikilizaji, dini zote za tauhidi na Mitume wote wa Mwenyezi Mungu walikuwa wakiwalingania watu heri na uongofu; na ni wazi kwamba Mwenyezi Mungu, ambaye ni Muumba wa mwanadamu hajatoa amri yoyote inayokinzana na kupingana na fitra na maumbile ya kiumbe huyo. Kwa ushahidi wa historia, mafundisho ya Mitume wa kabla ya Mtume wa mwisho, Nabii Muhammad SAW yalibadilishwa na kupotoshwa. Kutokana na kushindwa mwanadamu kuyalinda mafundisho hayo ya mbinguni, Mitume wengine wapya walikuwa wakitumwa na Allah ili taa ya uongufu utokao kwa Mola isizimike. Uislamu, ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, ulidhihiri katika mazingira, ambapo jamii ya mwanadamu ilikuwa na uwezo wa kutunza turathi zake. Kwa ungamo la wanafikra na wanahistoria, kitabu cha mbinguni cha Waislamu, yaani Qur’ani, hakijawahi kupotoshwa na kubadilishwa tangu kuteremshwa kwake. Mafundisho ya Bwana Mtume SAW pia, kwa zaidi karne ya mbili baada ya kuaga dunia mtukufu huyo, kwa kiwango kikubwa yalibakia salama kutokana na kuwepo Maimamu maasumu wa kizazi chake. Kwa hivyo tunachotaka kujua sasa, ni Uislamu, ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu na iliyokamilika zaidi, ina mtazamo gani kuhusu dunia na juu ya kufaidika na neema za kidunia?

Katika fikra asili za Kiislamu, dunia na neema zake za kimaada sio tu kwa dhati yake si kitu kibaya, bali ni wenzo wa kutengenezea saada ya mwanadamu. Kile ambacho Uislamu unakitaja kuwa ni zuhdi au kujitenga na kuipa mgongo dunia ni kitu chenye tafsiri maalumu ambayo tutaibainisha katika maelezo yetu. Bwana Mtume SAW amesema:” Dunia ni shamba la (kuvunia) akhera”. Katika harakati za maisha haya ya dunia na katika maingiliano na wenzake, mwanadamu hupata fursa na suhula za kumwezesha kujichumia mengi ya kumfikisha kwenye ukamilifu wa kiutu. Aidha kujitenga na dunia, kwa maana ya kuacha kabisa raha za kidunia pamoja na mahusiano na maingiliano ya kijamii ni kitu kisicho na nafasi yoyote katika mafundisho ya Uislamu. Kuhusu wafuasi wa Nabii Isa Masih (AS) walioamua kuishi maisha ya utawa, Qur’ani tukufu imewazungumzia watu hao katika sehemu ya aya ya 27 ya Suratul Hadid kwa kusema:”Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao (wenyewe). Sisi hatukuwaandikia hayo”. Bwana Mtume SAW amesema:”Hakuwa utawa katika Uislamu”. Ndani ya Qur’ani tukufu, Mwenyezi Mungu amezitaja neema za kimaada na za kidunia, zikiwemo za mwenza wa ndoa, yaani mke au mume, watoto, mandhari za maumbile  na anuai za vilaji na vinywaji halali, na kuyaelezea yote hayo kuwa ni ishara na alama zake. Baadhi ya wakati Qur’ani tukufu imezitaja neema hizo kwa sura ya kiapo na kukuelezea kuzitumia na kuneemeka nazo katika mipaka ya fitra na maumbile halisi ya mwanadamu kuwa sio tu ni jambo linalojuzu bali ni la lazima.

Kwa mujibu wa aya za Qur’ani tukufu na hadithi zilizopokewa kutoka kwa Maimamu maasumu (AS), mwanadamu hana haki ya kujinyima na kujiharamishia moja kwa moja neema za kimaada za dunia. Imam Jaafar Sadiq (AS) amesema:”Kwa Muislamu mwenye busara inafaa asitafute ghairi ya vitu vitatu. Kujitengenezea maisha, kutafuta masurufu kwa ajili ya akhera na kustarehe kwa mambo yasiyo ya haramu.” Kinyume na watawa na wale wanaoipa mgongo dunia, Uislamu sio tu haukubali kuwa kubaki bila ya kufunga ndoa ni jambo tukufu bali umelikemea na kulikataza suala hilo. Bwana Mtume Muhammad SAW amesema:”Wakati mtu anapokuja kuposa na ikakuridhisheni tabia yake na dini yake, basi mkubalini; kwani msipofanya hivyo itaenea fitna na ufisadi katika ardhi”.  Katika aya ya 21 ya Suratu Rum, Mwenyezi Mungu anasema:” Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.”

Katika mafundisho ya Uislamu hata kuwa na hamu na kuzipenda neema hizo za kimaada hakulaumiwi wala hakukemewi. Hisia za mapenzi ya vitu mbalimbali ambazo Mwenyezi Mungu ameziweka ndani ya nafsi ya mwanadamu si kitu kilichofanywa bila ya lengo wala sababu. Kwa kufahamu hilo ndipo tutakapoelewa barabara madhumuni ya Qur'ani pale inapoyataja maisha ya dunia kuwa ni kitu chenye "kumpoteza", "kumhadaa" na "kumghafilisha" mtu. Shahidi Mutahhari anasema:" Kile ambacho Qur'ani inasema kuelezea dunia kama kitu kibaya, ni kutekwa nayo, kuikumbatia, kujifakharisha nayo pamoja na kutosheka na kuridhika na mambo yake ya kimaada. Kuifanya dunia ya kimaada kuwa ndio ghaya, lengo kuu na kusudio la ukamilifu wa mtu, ni jambo linalokemewa katika Uislamu na ni sababu ya kuikosa mwanadamu saada yake ya milele. Qur'ani tukufu inawaelezea watu wapenda dunia katika aya ya 7 ya Suratu Yunus kwa kusema:" Hakika wasio taraji kukutana nasi, na wakaridhia maisha ya dunia na wakatua nayo, na walio ghafilika na Ishara zetu". Katika aya hii, kilicholaumiwa na kukemewa ni kuridhika, kutosheka na kumakinika na vitu vya kimaada. Hivi ndivyo wanavyoelezewa wapenda dunia inayolaumiwa na kukemewa na Qur'ani.

Kwa maelezo hayo ni kwamba katika Uislamu, kuipa mgongo dunia, maana yake ni mtu kutoifanya dunia ya kimaada kuwa ndio ghaya na tarajio kamili wala kughariki kwenye vitu vya kimaada, bali kuitambua johari ya utu iliyojenga nafsi na ujudi wake. Aifanye saada yake ya akhera, ambayo ni kupata radhi za Mola wake Muumba kuwa ndio ghaya na tarajio lake kuu na azitumie neema za kimaada kulingana na fitra aliyoumbiwa na Mola kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Kufuata hukumu na mafundisho ya Uislamu humwezesha mtu kuyaongoza matamanio, ghariza na mahitaji yake ya kimaada katika muelekeo wa kufikia ukamilifu anaostahiki na kuipata saada na fanaka ya milele. Kutokana na Uislamu kutoa tafsiri tofauti kabisa ya zuhdi na kuipa mgongo dunia, ndiyo maana wafuasi wa dini hii hawana mtazamo hasi na wa kufunga mikono tu kuhusiana na dunia. Na ndiyo kusema kuwa mbele ya macho ya Waislamu, dunia si kitu chenye mgongano na dini hata iwe sababu ya wao kutafuta mwongozo mwengine wa nje ya mafundisho ya dini ili kuishi maisha yatakayowiyana na fitra na maumbile waliyojaaliwa na Mola wao.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo nikiwa na matumaini kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika sehemu hii ya nane ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu. Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo kwa majaaliwa ya Mola katika sehemu ya tisa ya kipindi hiki nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani