Nov 01, 2016 07:06 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (30)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 30 ya mfululizo huu.

Kwa wafuatiliaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulianza kuzungumzia maudhui ya "kuwa na maana maisha" katika mtazamo wa Usekulari; na tukasema kuwa wanafikra wengi wanaitakidi kwamba sababu kuu ya kuzungumziwa suala la "maana ya maisha" ni kukabiliwa mwanadamu na kitu kiitwacho "kifo". Tukaeleza kwamba baadhi ya Wasekulari wanasema inatosha maisha ya mtu au sehemu ya maisha yake ihusishe mambo yanayogusa hisia, hamu na utashi au imani binafsi za mtu ili kuyafanya maisha yawe na maana maalumu.

Lakini baadhi ya wanafikra wengine wa Kisekulari, wao wameliangalia suala hili kwa umakini zaidi na wanaitakidi kuwa maisha ya mwanadamu yanatakiwa yajishughulishe ipasavyo na vitu na mambo yenye thamani ili yaweze kuwa na maana. Yaani vitu vyenye thamani ambavyo vitakuwa nje ya nafsi ya mtu; na yeye mtu avishughulikie vitu hivyo vyenye thamani ili maisha yake yaweze kuwa na thamani; kama kuwasaidia watu na kujishughulisha na kazi za sanaa. Lakini wakosoaji wa rai na fikra hii wanahoji, ni kipimo na kigezo gani kilichotumika kuvifanya vitu hivyo viwe vyenye thamani? Kuainisha kigezo na kipimo cha kutambua mambo yenye thamani ni suala ambalo linapojibiwa katika Usekulari husababisha mzunguko wa kurejea unapoanzia; yaani baadhi ya wakati amali na tendo fulani huwa la thamani kwa sababu linayafanya maisha yawe na maana; na maisha yenyewe nayo huhesabiwa kuwa ni yenye maana kwa sababu yanajishughulisha na amali yenye thamani.

 

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa katika mtazamo wa Usekulari ladha tamu za maisha ni usalama, utulivu wa kiakili, ushairi, muziki, sanaa, kusafiri na kufanya kazi; na mambo ya aina hii ndiyo yanayomfanya mtu awe na maisha ya furaha na fanaka. Wasekulari wanasema, sisi wanadamu inatupasa tufahamu kwamba hakuna chochote kikubwa zaidi, cha kutufanya watu wenye furaha, fanaka na saada. Makusudio na madhumuni ya maneno yao ni kwamba tunapaswa kuyafikia malengo, ya ndani ya maisha haya haya, wala tusitake kufuatilia lengo kubwa zaidi la uumbwaji. Baadhi ya Wasekulari wanasema, ikiwa Mwenyezi Mungu ameainisha lengo maalumu kwa ajili ya maisha ya mwanadamu, na anamuelekeza na kutaka kumfikisha kwenye lengo hilo kwa ahadi ya Pepo na ahadi ya Moto, kwa kweli atakuwa amemvunjia heshima kiumbe huyo. Baada ya hoja na maelezo hayo ya Wasekulari, hebu sasa na tuangalie nini mtazamo wa Uislamu juu ya masuala haya.

Uislamu unaichukulia dunia shamba la kulima mazao ambayo mtu atakwenda kuyavuna akhera. Kulingana na aya za Qur'ani tukufu na Hadithi, maisha ya mwanadamu katika dunia hii ya kimaada yana sura ya mtihani; na lengo kuu na la asili la maisha ni saada ya milele ya mwanadamu ambayo kwa hakika ni kufikia daraja ya kuwa karibu na Allah. Jitihada zake mwanadamu za kufikia lengo hilo aali na tukufu ndizo zinazoyafanya maisha yake yawe kitu chenye maana.  Dini ya Uislamu inatoa ufahamu na utambuzi wa kina kuhusu ulimwengu na mwanadamu; na kwa mtazamo wa dini hii tukufu, mwanadamu ni khalifa wa Mwenyezi Mungu hapa duniani. Imani juu ya suala hili linaifanya kila sekunde, dakika na saa ya maisha ya mwanadamu iwe na maana maalumu. Mtu ambaye ni Muislamu anayachukulia maisha ya hapa duniani kuwa ni fursa ambayo itamwezesha kuifikisha nafsi yake kwenye lengo lililotukuka na la umaanawi.

 

Kulingana na fikra za Kiislamu, kila mtu, katika kila hali na mazingira, awe na suhula nyingi au chache za kimaada, awe katika hali ya ugonjwa au afya na uzima, katika hali ya dhiki au raha na katika umri wa ujana au uzee ni mweza wa kupiga hatua kuelekea kwenye lengo aali na lililotukuka la kujikurubisha kwa Mola Muumba. Pamoja na kwamba Uislamu unamshajiisha na kumhimiza mwanadamu afanye jitihada za kujitengenezea maisha mazuri yeye mwenyewe na wanadamu wenzake, kujizalishia utajiri na hali bora ya suhula za kimaada, lakini unaziangalia neema zote hizo kama nyenzo za kufikia lengo kuu na la asili la maisha ya mwanadamu; na kutokuwepo au kukosekana suhula na neema hizo hakukwamishi wala kupunguza chochote katika kuyafanya maisha yawe kitu chenye maana. Mashaka na mateso ya maisha ya dunia katika mambo mengi ni kitu kisichoweza kuepukika; kama mtu kusibiwa na maradhi au pengine kuishi maisha ya kinyonge ya ukata. Lakini wakati mtu anapoyaangalia maisha kwa jicho la kidini, hata anapokuwa katika hali mbaya kabisa ya maisha ya kimaada huwa hayahisi maisha kuwa kitu cha upuuzi na kisicho na faida wala maana yoyote, kwa sababu anaitakidi kwa dhati kuwa amali na tendo dogo kabisa jema na la kheri atakalofanya katika hali na mazingira yoyote ya kimaisha, linamsogeza hatua moja mbele kuelekea kwenye saada na fanaka ya milele.

Tumesema kwamba baadhi ya wanafikra wa Usekulari wanaitakidi kwamba kuainishwa lengo la maisha ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu na kuwekewa malipo ya ujira na thawabu au adhabu na ikabu kwa sababu ya kufikia lengo hilo ni kumvunjia heshima mwanadamu. Jawabu ya madai haya ni nyepesi na rahisi mno kwa kuzingatia misingi ya fikra za Kiislamu. Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa mwanadamu na ulimwengu. Yeye ni mjuzi na mwelewa zaidi ya mwengine yeyote yule kuhusu kanuni za ulimwengu aliouumba; na kutokana na huruma na rehma zake amemjulisha mwanadamu kuhusu vipi yatakuwa matokeo ya amali na matendo yake, hapa duniani na huko akhera; na kisha baada ya kufanya hivyo ametupa uhuru na hiyari sisi wenyewe ya kuchagua njia ya kufuata, iwe ya kheri na uongofu au ya shari na upotofu. Watu wanaoona kwamba kuwepo ujira wa thawabu na adhabu ya akhera kunakinzana na hadhi ya mwanadamu wameghafilika na kutoelewa nukta hii, kwamba thawabu na adhabu si mambo ya kupangwa na kubuniwa bali ni dhihirisho la amali na matendo ya mtu mwenyewe; na kwa hivyo kitu pekee alichofanya Mwenyezi Mungu ni kututanabahisha kabisa kuhusu matokeo ya amali zetu.

 

Uislamu haukatai moja kwa moja ulazima wa malengo madogo madogo katika maisha, lakini unayachukulia malengo hayo kuwa yana thamani pale tu yanapokuwa kwenye mkondo wa kumfikisha mtu kwenye lengo lililotukuka la kuumbwa kwake. Katika hali hiyo, sanaa, kazi, kujifunza elimu, ubunifu na kuwasaidia watu yatakuwa mambo yenye thamani. Lakini kama mtu ataghafilika na lengo kuu la uumbaji, ambalo ni hilo la fanaka na saada yake ya milele na kujikurubisha kwa Mola wake, mambo hayo yatakuwa si chochote zaidi ya burudani ya kupitisha wakati ambayo humsaidia mtu asiyawaze mateso ya kuishi maisha yasiyo na lengo; na kwa hakika ni kumfanya asiing'amue hali ya upuuzi na kutokuwa na maana maisha ya aina hiyo. Kwa kweli fikra ya aina hii ni sawa na dawa ya kulevya ya kumlaza mtu. Ni kwa sababu hii, baadhi ya wanafikra wa Usekulari mwishowe wameyaona maisha kitu kisicho na maana yoyote na kuamua kujiua.  Wasekulari wanamtaka mwanadamu asifikirie kifo bali asubiri kukabiliana nacho tu na kukubali kwamba mauti ni kutoweka na ni mwisho usioweza kuepukika. Lakini kwa mtazamo wa Uislamu, kujighafilisha na kujisahaulisha si sifa anayolaiki kuwa nayo mwanadamu; na ndiyo maana unamtaka atafakari, asiidunishe nafsi yake yenye thamani na wala asiridhike na chochote isipokuwa kuifikia saada ya milele ambayo ndiyo daraja inayomstahiki mwanadamu.

 Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 30 ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi hiki. Basi hadi tutakapokutana tena inshallah juma lijalo katika sehemu nyengine nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags