Sep 21, 2016 08:41 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (24)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 24 ya mfululizo huu.

Kwa wale mnaofuatilia kwa karibu kipindi hiki mtakuwa mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita mazungumzo yetu yalikomea katika kubainisha nukta kwamba mtazamo wa kisekulari, ni wa kukwepa wajibu na uwajibikaji na unachojali ni mtu kuwa na “haki” tu basi. Hali ya kuwa hakika ya mambo ni kwamba “haki” na “wajibu” ni watoto pacha au ni pande mbili za sarafu moja. Tukasema, kwa mtazamo wa Uislamu mwanadamu ana wajibu na mas-ulia mbele ya Mwenyezi Mungu, mbele ya wanadamu wenzake na hata mbele ya ulimwengu wa maumbile na neema kadha wa kadha alizopewa na Mola. Na tukabainisha kuwa tunapomchukulia mtu kuwa na haki fulani, maana yake ni kwamba tumembebesha mtu mwengine mzigo wa wajibu kwa mtu huyo. Mathalani, tunapozungumzia haki ya mtoto ya kupata elimu huwa wakati huohuo tunazungumzia wajibu wa wazazi na jamii wa kumpatia elimu mtoto huyo. Kama tulivyotangulia kusema, katika haki za binadamu za Usekulari hakujazungumzwa chochote kuhusu ‘wajibu’. Kulingana na mtazamo huu haki na wajibu ni vitu vinavyogongana; kwa hivyo tunapompangia mtu wajibu wa kufanya, maana yake ni kukiuka haki zake na uhuru wake wa binafsi.

Lakini kwa mtazamo wa Uislamu, haki na wajibu haviwezi kuwa na maana bila ya kuwepo pamoja. Imam Ali (AS) anasema:" Haki yoyote ile haithibitiki kwa mtu isipokuwa mkabala wake kuna wajibu anaoebebeshwa, na halithibitiki jukumu na wajibu kwa mtu isipokuwa mkabala wake kuna haki inayothibiti juu yake".

 Katika mtazamo wa Kiislamu, mwanadamu si kiumbe aliyeachwa vivihivi awe yupo tu katika dunia hii. Mwanadamu siye mmiliki wa dunia hii ila ni mbora wa viumbe, ambaye anapaswa kufuata njia ya kufikia ukamilifu wake kwa kujenga maelewano na wanadamu wenzake na pia na maumbile na neema alizojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Katika mtazamo wa Kiislamu, mfalme na mmiliki halisi wa ulimwengu ni Mwenyezi Mungu; na mwanadamu ana majukumu na wajibu mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumba wake na Muumba wa ulimwengu; lakini pia ana wajibu mbele ya wanadamu wenzake pamoja na ulimwengu wa maumbile. Ni kwa kutegemea msingi huu ndipo tukaona katika haki za binadamu za Kiislamu mwanadamu hana haki ya kuamiliana nayo na kuyafanyia atakavyo hata mazingira ya maumbile na wanyama. Yaani hatakiwi kisheria kumfanyia maudhi mnyama au kumuua bila ya sababu. Hawezi kuharibu na kuangamiza maumbile, bali pia hana haki ya kuidhuru hata roho na kiwiliwili chake mwenyewe. Kwa mtazamo wa Uislamu, mwanadamu ana jukumu na wajibu kwa watoto wake, wazazi wake, majirani zake na watu wengine hata kama watakuwa si Waislamu.

 

Tafakuri ndogo tu inatosha ili kufahamu kuwa jukumu na wajibu huo ni ishara ya umuhimu ambao Uislamu umelipa suala la kuchunga na kuheshimu haki za wengine. Kulingana na mafundisho ya Kiislamu, hata mtu mhalifu na mtenda jinai ambaye amehukumiwa kuuawa, naye pia ana haki zake ambazo ni wajibu watu kuzichunga na kuziheshimu.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mwanadamu ana wajibu na majukumu mbalimbali mbele ya Muumba wake. Hakika ya majukumu na wajibu huo ni njia za kumpatia saada mwanadamu. Saada na fanaka ya milele ya mwandamu haiyumkiniki kupatikana bila ya kujikurubisha kwa Mola.  Kwa hakika majukumu na wajibu ambao Uislamu umemwekea mwanadamu, yote yanalenga kumwezesha kuifikia haki yake ya msingi kabisa, yaani "haki ya kufikia ukamilifu stahiki wa mtu". Kuyapuuza majukumu na wajibu na kutilia mkazo haki tu kunamfanya mwanadamu kiumbe mbinafsi anayejiona mmiliki wa ulimwengu na mwenye haki juu yake, ilhali Muumba na Mmiliki wa dunia ni Mwenyezi Mungu, na mwanadamu ni kiumbe na mahuluku wa Mwenyezi Mungu ambaye ameletwa hapa duniani kwa lengo kubwa. Kusahau uhusiano wa baina ya Muumba na muumbwa, yaani wa Mwenyezi Mungu na mwanadamu ni kizingiti na kizuizi kikubwa kwa mwanadamu kufikia kwenye haki yake kubwa kabisa, yaani saada ya milele.

*****

Tofauti nyengine muhimu na ya msingi baina ya haki za binadamu za Kiislamu na haki za binadamu za Usekulari ni katika chanzo na asili ya haki zenyewe. Yaani haki hizo chimbuliko lake ni lipi na itibari yake imetokana na nini? Kuna mitazamo mbalimbali kuhusu chimbuko na asili ya haki za binadamu. Kuna baadhi wanaoamini kuwa zinatokana na rai na kura za wananchi, na kuna kundi jengine la watu wakiwemo wanahekima na wasomi wanaoamini kuwa kanuni za maumbile na au fitra na maumbile ya mwanadamu mwenyewe ndio chanzo cha haki za binadamu. Ayatullah Javad Amoli, alimu na msomi Muislamu yeye anasema: "Katika fikra za Kiislamu, chanzo cha haki zote ni Mwenyezi Mungu, na hii ndio njia ya kulinda haki za watu. Kwa hakika ni Mwenyezi Mungu tu ndiye mwenye haki ya kuweka sharia. Naye ni mwenye hekima, asiyemili upande wowote na Mwenye kujua zaidi njia za saada na zenye hasara kwa watu". Kwa hivyo kulingana na mtazamo wa Uislamu asili ya kila haki katika ulimwengu wa maumbile ni Mwenyezi Mungu Mwenye hekima ambaye ndiye mwenye kuufanya ulimwengu uwepo.

 Haki, wapenzi wasikilizaji, asili yake inatokana na umiliki; kwa maana kwamba kama mtu si mmiliki wa kitu hawezi kuwa na haki juu ya kitu hicho isipokuwa kama atapata idhini hiyo kwa mmiliki halisi. Katika haki za binadamu za Usekulari mwanadamu amefanywa kuwa mmiliki wa nafsi na uwepo wake; hali ya kuwa hana uwezo wa kujidhaminia na kujihakikishia uwepo na kutokuwepo kwake katika ulimwengu huu. Kulingana na mafundisho ya Uislamu, Mwenyezi Mungu ndiye mmiliki halisi wa ulimwengu wa maumbile pamoja na mwanadamu; na ndiye mwenye haki juu ya vyote hivyo viwili. Kwa hivyo kuthibitisha kuwa na haki kiumbe chochote kile kunajuzu kupitia idhini ya Mwenyezi Mungu. Hivyo basi chimbuko na asili ya haki za binadamu ni Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye aliyemuumba mwanadamu na kumpa utukufu ili kutokana na utukufu huo awe na haki ambazo haziwezi kukanushika.

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 24 ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi hiki. Katika kipindi kijacho tutakuja kuzungumzia akhlaqi za kidini na tofauti iliyopo baina yake na akhlaqi katika nadharia ya Usekulari. Basi hadi wakati huo inshallah nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani…/

 

Tags