Nov 01, 2016 07:03 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (29)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 29 ya mfululizo huu.

Usekulari kama tulivyotangulia kusema, kwa maana ya kutenganisha dini na uga wa maisha ya mtu, leo hii umegubika nyuga tofauti za kifikra katika Ulimwengu wa Magharibi. Tulitangulia kueleza pia ilikuwa kuwaje misingi ya fikra ya Usekulari ikajengwa kutokana na Ukristo na utamaduni wa Magharibi.  Humanism (Umwanadamu), Liberalism (Uliberali), Scientism (Usayansi) na Rationalism (Urazini) inahesabiwa kuwa miongoni mwa misingi muhimu ya Usekulari. Tab'an kila moja kati ya misingi hii ina wakosoaji wakubwa katika nchi zenyewe za Ulimwengu wa Magharibi. Aidha mazingira ya kihistoria na kiutamaduni ya zama za Enzi za Kati (Middle Ages) yaliyosababisha kuibuka kwa Mvuvumko wa Sanaa na Utamaduni barani Ulaya, kwa kimombo Renaissance, nayo pia yalikuwa na taathira muhimu katika kuchipua na kuenea fikra ya kutenganisha dini na maisha. Kwa hakika kushindwa Ukristo uliopotoshwa kuendesha jamii na ubutu wa muhtawa wa mafundisho yake katika kuyapatia majibu mahitaji ya watu viliwafanya baadhi ya wanafikra waichukulie dini kuwa ni kitu cha mtu binafsi kinachohusiana na hisia za mtu mwenyewe.

Wanafikra wengi wa Kiislamu wanaitakidi kuwa Usekulari hauna nafasi katika jamii zenye sifa tofauti na za Ulimwengu wa Magharibi. Kutokana na Uislamu kuwa na sifa maalumu ikiwemo mafundisho yaliyokamilika, ratiba na miongozo maalumu kwa ajili ya nyanja tofauti za maisha, kuendana na mabadiliko ya mazingira ya zama na kuwa na Kitabu cha mbinguni ambacho hakijatiwa mkono na kupotoshwa, dini hiyo ni tofauti kabisa na Ukristo uliojenga mazingira ya kujitokeza Usekulari.

Hii ni sawa na kusema kwamba katika jamii za Kiislamu, kinyume na jamii za Magharibi, dini haisimami kukabiliana na elimu, akili na dunia, bali inaichukulia akili na elimu ya mwanadamu kuwa ni neema za Mwenyezi Mungu alizomtunuku kiumbe mwanadamu ili aweze kuwa na maisha bora yeye mwenyewe na wanadamu wenzake katika dunia hii na vilevile kwa kutumia akili yake kwa njia sahihi aweze kubainikiwa na ukweli wa wahyi utokao kwa Mola wake. Kwa hivyo kwa ujumla Waislamu wanaichukulia dini kuwa ni ratiba kamili ya mwongozo kwa ajili ya maisha ya duniani na akhera. Na ndiyo maana, kwao wao, kutenganisha dini na maisha ni jambo lisiloleta maana yoyote. Katika mifululizo kadhaa ya kipindi hiki tumezungumzia kwa muhtasari kuhusu taathira za fikra na nadharia ya Usekulari katika nyuga mbalimbali zikiwemo za haki za binadamu na akhlaqi.

 

 

Tukiendelea na kipindi chetu tutupie jicho sasa maudhui nyengine muhimu ambayo ni moja ya madukuduku makubwa ya mwanadamu wa leo. Ni kuhusu "maana ya maisha" ili tuweze kujua kuna tofauti gani baina ya mtazamo wa kidini na kisekulari juu ya maana ya maisha.

Katika vitabu vya falsafa na akhlaqi vya zama zilizopita "kuwa na maana maisha" hakujazungumziwa kama maudhui peke yake yenye kujitegemea. Inavyoonyesha, kwa mtazamo wa wanafalsafa na wataalamu hao wa huko nyuma, 'maisha yenye maana' ni jambo la wazi kabisa na ni utangulizi wa maudhui na mijadala mingine; lakini katika ulimwengu mpya suala hilo limezishughulisha akili za wanafikra wengi. Albert Camus, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa wa karne ya 20 anasema "maana ya maisha" ni suala muhimu zaidi na la kujadiliwa haraka zaidi.

Katika dunia ya sasa matatizo mbalimbali ya kifikra na kinafsi kama wasiwasi, msongo wa mawazo, huzuni, kupoteza matumaini, kukata tamaa na kuyaona maisha kitu cha upuuzi yana uhusiano wa moja kwa moja na maudhui ya "maana ya maisha". Wanafikra wengi wanaitakidi kuwa sababu kuu ya kuzungumziwa suala la "maana ya maisha" ni kukabiliwa mwanadamu na kitu kiitwacho "kifo". Kifo au mauti ni mwisho wa maisha ya hapa duniani na pengine tunaweza kusema ndiyo awamu ya maisha ya mtu yenye siri kubwa na nzito zaidi. Kutokana na mtazamo wa kidini juu ya dunia, wafuasi wa dini za mbinguni wanajua kwamba mauti sio mwisho wa maisha na wanaitakidi kuwa Muumba wa ulimwengu alikuwa na lengo aali na tukufu la kuumba dunia na mwanadamu.

 

Imani na itikadi hii ndio mzizi na msingi mkuu wa tafsiri ya kidini ya maana ya maisha. Lakini kwa sababu Wasekulari hawakubali kuwa wahyi ni moja ya vyanzo vya utambuzi, hawana uelewa wa kuwakubalisha kuhusu mauti. Kwa sababu hiyo ima wanakanusha ma'adi na maisha baada ya kifo au hawalijali wala kulitilia maanani suala hilo.

Kiujumla Wasekulari wanaitakidi kuwa ili kuwa na maisha yenye maana hakuna ulazima wa sisi kuwa na imani juu ya Mungu, ulimwengu baada ya kifo na lengo aali na tukufu la uumbaji; na wanadai kwamba katika dunia isiyo na imani ya Mungu pia inawezekana kuwa na malengo juu ya maisha na kuyafanya maisha yawe kitu chenye maana na hivyo kumwokoa mwanadamu na hali ya kuyaona maisha kitu cha upuuzi na badala yake kumfanya ayahisi maisha yake kuwa ni kitu chenye maana. Tab'an kuna baadhi ya Wasekulari kama Jean-Paul Sartre na Franz Kafka, wanafalsafa wa Ulaya wa karne ya 20 wanaoitakidi kuwa kimsingi, maisha ya mwanadamu ni upuuzi na kitu kisicho na maana. Lakini kundi jengine la Wasekulari linaitakidi kwamba masuala madogo madogo na yanayoweza kupatikana katika maisha haya haya ya dunia yanaweza kuyafanya maisha yawe na maana.

Kai Nielsen, mwanafalsafa mlahidi wa Kimarekani, yaani asiyeamini kuwepo kwa Mungu anaitakidi kuwa machaguo mbalimbali anayofanya mtu kwa uelewa katika maisha yanayafanya maisha yawe na maana maalumu. Baadhi ya Wasekulari wanasema inatosha maisha ya mtu au sehemu ya maisha yake ihusishe mambo yanayogusa hisia, hamu na utashi au imani binafsi za mtu ili kuyafanya maisha yawe na maana maalumu. Baadhi ya Wasekulari wengine wanasema maisha ya mwanadamu huwa yana maana pale yeye anapokipenda kitu.  Wakosoaji wa rai na fikra hii wanasema, kuwa na maana maisha hakuwezi kufungamanika na hisia, hamu na matashi tu ya binafsi, kwa sababu katika hali hiyo, kama mtu atapata hisia nzuri kwa mambo yenye umuhimu finyu kama mathalani, kula aiskrimu au kukusanya vifuniko vya chupa na akatumia muda wake mwingi katika mambo hayo, kulingana na vigezo vilivyotajwa hapo juu atakuwa na maisha yenye maana; ilhali kwa mtazamo wa akthari ya watu maisha ya aina hiyo ni upuuzi na yasiyo na maana yoyote.

 

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 29 ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa nikitumai kuwa mumenufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi hiki. Katika kipindi kijacho tutakuja kuendelea kuizungumzia maudhui hii ili kuweza kujua mitazamo ya Wasekulari wengine kuhusu maana ya maisha, na mtazamo wa Uislamu juu ya suala hilo. Basi hadi wakati huo inshallah nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags