Jeshi la Yemen lajibu mapigo kwa kushambulia maeneo kadhaa ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128028-jeshi_la_yemen_lajibu_mapigo_kwa_kushambulia_maeneo_kadhaa_ya_israel
Jeshi la Yemen limefanya mashambulizi mapya ya makombora katika maeneo mbali mbali ya Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ili kulipiza kisasi cha mashambulizi ya anga ya utawala huo pandikizi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2025-07-07T06:33:08+00:00 )
Jul 07, 2025 06:19 UTC
  • Jeshi la Yemen lajibu mapigo kwa kushambulia maeneo kadhaa ya Israel

Jeshi la Yemen limefanya mashambulizi mapya ya makombora katika maeneo mbali mbali ya Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ili kulipiza kisasi cha mashambulizi ya anga ya utawala huo pandikizi dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Ndege za kivita za Israel usiku wa kuamkia leo, zimefanya mashambulizi 20 ya anga dhidi ya mji bandari wa Hudeidah, magharibi mwa Yemen.

Jeshi la Yemen limesema katika taarifa jana Jumapili kwamba, kikosi chake cha anga kimekabiliana na uvamizi wa Israel dhidi ya Yemen. "Vikosi vya Jeshi la Yemen vinawahakikishia watu wetu na watu huru wa taifa letu kwamba wamejiandaa kwa hali ya juu na, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, wana uwezo wa kukabiliana na wavamizi, na kwamba hujuma hizi hazitawaathiri wao au uwezo wao wa kijeshi.

Taarifa ya Jeshi la Yemen imesisitiza kuwa, kuunga mkono operesheni za Gaza na Palestina zitaendelea kwa kasi kubwa, na kwamba Wayemen watailinda nchi yao, na taifa lao kwa nguvu zote inshaAllah.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa, angalau kombora moja la balistiki la Yemen lilifanikiwa kupenya angani huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Shambulio hilo lilisababisha ving'ora vya tahadhari kuhinikiza kwenye vitongoji kadhaa vya walowezi wa Kizayuni, yakiwemo maeneo ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Al-Quds.

Kabla ya hapo, uwanja mkuu wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv ulisimamisha safari zote za ndege kutokana na hofu ya kutokea kwa mashambulizi zaidi ya makombora.

Shambulio hilo la vikosi vya Yemen vimejiri kujibu mashambulizi ya anga ya Israel jana Jumapili kwenye bandari kadhaa muhimu za nchi hiyo ya Kiarabu.