Mshauri wa IRGC: Uwezo mkubwa wa ulinzi wa Iran bado haujaonyeshwa
(last modified Mon, 07 Jul 2025 06:33:19 GMT )
Jul 07, 2025 06:33 UTC
  • Mshauri wa IRGC: Uwezo mkubwa wa ulinzi wa Iran bado haujaonyeshwa

Mshauri mwandamizi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Brigedia Jenerali Ebrahim Jabbari amesema kuwa silaha, zana za kijeshi na vituo vingi vya ulinzi vya Iran bado havijaonyeshwa na kuwekwa paruwanja.

Akizungumza katika mahojiano na Shirika la Habari la Mehr, mshauri wa IRGC Brigedia Jenerali Ebrahim Jabbari amesema kuwa, vikosi vya jeshi vya Iran viko katika kilele cha utayarifu.

"Shahidi Hajizadeh aliwahi kusema kwamba, ikiwa kutakuwa na vita kati ya Iran na Israel na Marekani, hatutaishiwa na rasilimali ikiwa tutawavurumishia makombora kila siku kwa kipindi cha miaka miwili," Jabbari amesema.

Ameeleza bayana kuwa, hivi sasa, maghala ya chini ya ardhi, miji ya makombora, na hifadhi ya zana za kijeshi ni kubwa mno, na kwamba bado Iran haijaonyesha zana zake zote za ulinzi na makombora madhubuti ya nchi hii.

"Iwapo adui Mzayuni anataka kuendeleza vita na kuishambulia nchi yetu, itakuwa siku ya kustaajabisha kwa sababu jeshi letu, IRGC, vikosi vya ardhini na angani vitaingia katika medani ya vita kwa nguvu zao zote," ameongeza.

Akirejelea idadi kubwa ya miji ya chini ya ardhi ya Iran ya makombora na silaha za kisasa, mshauri wa IRGC Brigedia Jenerali Ebrahim Jabbari amesema kuwa, vituo vingi vya ulinzi vya Iran bado havijaonyeshwa.