Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani yafanyika Rwanda
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yamefanyika mjini Kigali, Rwanda ambapo wanaharakati na wadau wa Kiswahili wamezitaka nchi za jumuiya ya Afrika mashariki kuanzisha mabaraza ya Kiswahili kama mojawapo ya suluhu ya changamoto kubwa zinazokabili ukuaji wa Kiswahili kwenye jumuiya hiyo.
Haya ni maadhimisho ya nne tangu Shirika la Umoja wa Mataifa la Utamaduni,Sayansi na Elimu UNESCO lilipoitenga tarehe saba Julai kila mwaka kuwa ni siku ya maadhimisho ya kuienzi lugha ya Kiswahili.
Kongamano la Kiswahili Kigali limejumuisha matumbuizo na mijadala mbalimbali kuhusu jinsi waafrika hasa wananchi wa jumuiya ya Afrika mashariki wanavyoweza kuendelea kukitumia Kiswahili kama nyenzo ya kuwaunganisha katika Nyanja mbalimbali za maisha yao ya kila siku.
Maadhimisho ya Miaka Minne ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yalianza Jumapili mjini Kigali, yakiangazia jukumu la Kiswahili kama chachu ya mafungamano ya kikanda, elimu jumuishi na maendeleo endelevu.
Yakiandaliwa kwa pamoja na Rwanda na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, maadhimisho hayo ya siku mbili yalipewa kaulimbiu ya “Kiswahili, Elimu Jumuishi na Maendeleo Endelevu”, yakihusisha uchunguzi wa sera zinazofaa, mbinu bora na ushirikishwaji wa wadau.
Hafla hiyo iliwaleta pamoja zaidi ya washiriki 300, wakiwemo maafisa waandamizi wa serikali, wajumbe kutoka nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wasomi, wataalamu wa Kiswahili na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Akihutubia hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiyay Afrika Mashariki EAC Andrea Aguer Ariik Malueth alisema Kiswahili, zaidi ya kuwa lugha, ni chombo cha usawa, ufikiaji na uwezeshaji.
Naye Katibu mkuu mstaafu wa kamisheni ya Kiswahili Afrika mashariki Professor Inyani Simala ambaye sasa ni mkufunzi wa Kiswahili katika chuo kikuu cha Masinde Muliro huko Kenya anasema "Nafikiri tatizo kubwa ni kwamba kuna nia ya kuendelea Kiswahili ila hapajakauwepo sera za kuongoza namna ambavyo Kiswahili kinastahili kwenda."
Takwimu zilizotolewa nashirika la umoja wa mataifa la utamaduni na elimu UNESCO zimeonyesha kwamba Kiswahili sasa kinazungumzwa na watu zaidi ya milioni 200 duniani kote hali ambayo inakifanya kuwa na nafasi muhimu katika maisha ya waafrika kama lugha yao unganishi.