Grossi: Uwezo wa nyuklia wa Iran hauwezi kuzimwa kwa mabavu
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati wa Atomiki IAEA amesema kuwa, mpango wa nyuklia wa Iran, nchi yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, kiviwanda na kiteknolojia hauwezi kuzimwa kwa hatua za kijeshi wala hatua zozote za mabavu.
Rafael Grossi amesisitiza kuwa, ushirikiano wa IAEA na nchi za Ulaya, Marekani, na China ndio unaweza kupelekea kupatikana suluhisho la kudumu na la kidiplomasia kwa suala hili.
Grossi ameeleza bayana kuwa, "Tulisisitiza katika ripoti kabla ya vita vya siku 12 kwamba, hatukuwa na ushahidi wa kuaminika kwamba Wairani wanamiliki silaha za nyuklia."
Kauli ya IAEA inakuja baada ya utawala wa Israel na muungaji mkono wake, Marekani, kuanzisha vita vya siku 12 dhidi ya Iran kwa kisingizio kwamba Iran inafanikisha bomu la nyuklia. Mashambulizi hayo yalipelekea kuuawa shahidi wananchi wasiopungua 1,000 wa Iran.
Matamshi hayo ya Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, yamekuja katika hali ambayo, kiwango cha Iran kutokuwa na imani na nchi za Magharibi kimefikia kilele chake.
Mashambulizi ya Israel na Marekani sio tu yamekuwa na athari za kibinadamu na kimazingira, bali pia yameharibu uaminifu wa mikataba ya kimataifa.