Nov 01, 2016 06:59 UTC
  • Usekulari Katika Mizani ya Uislamu (27)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki, ambacho lengo lake ni kuuchambua Usekulari kwa kutumia mizani ya mafundisho ya Uislamu ili kuweza kuelewa kasoro, dosari na udhaifu wa fikra na nadharia hiyo ambayo chimbuko lake ni Ulimwengu wa Magharibi. Ni mategemeo yangu kuwa mtanufaika na kuelimika na yale mtakayoyasikia katika kipindi hiki. Endeleeni kuwa pamoja nami basi kuitegea sikio sehemu hii ya 27 ya mfululizo huu.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki, bila ya shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulizungumzia athari za Usekulari katika uga mmoja muhimu wa maisha ya mwanadamu, yaani akhlaqi na tukaashiria sifa maalumu za asili ya akhlaqi za Usekulari. Aidha tuliweza kufahamu kwamba sifa nyengine muhimu zaidi za akhlaqi za Usekulari ni kuwa kwake suala la kidunia tu, la mtu binafsi, lisilokuwa na uhusiano na dini pamoja na kutiliwa mkazo uhuru wa kiwango cha juu kabisa wa mtu binafsi.

Lakini mbali na hayo tulisema kwamba kilicho na nafasi kuu katika kuweka misingi ya akhlaqi za Usekulari, ni tafsiri waliyotoa Wasekulari kuhusu dini na akhlaqi. Wao wanaichukulia dini kuwa jambo la mtu binafsi na la batini, na ambayo haina mizizi na misingi inayotakiwa kwa ajili ya kuendesha maisha ya mtu na jamii. Akhlaqi nazo wanazichukulia ni jambo linalohusu mlahaka wa baina ya watu ambalo lengo lake ni kulinda na kudumisha nidhamu na uthabiti wa jamii na kujenga hisia za furaha na ridhaa katika nafsi za watu. Lakini tafsiri yao kuhusu dini haiendani na sifa za dini ya Uislamu, kwa sababu Uislamu una ratiba kamili ya uendeshaji maisha ya mtu binafsi na ya jamii nzima. Katika mtazamo wa Uislamu lengo la kuumbwa mwanadamu ni kujikurubisha kiumbe huyo kwa Mwenyezi Mungu na kufikia ukamilifu stahiki wa kiutu. Tafsiri unayotoa Uislamu kuhusu akhlaqi pia ina uhusiano mkubwa na lengo la kuumbwa mwanadamu. Katika kipindi chetu cha leo tunataka kuzungumzia zaidi uhusiano wa dini na akhlaqi na kuona kama madai ya Wasekulari kuhusu akhlaqi kutohitajia dini ni sahihi au la?

 

Kuhusiana na suala hili ni kwamba kulikuwa, na kungali kuna mitazamo tofauti kuhusu uhusiano baina ya dini na akhlaqi. Baadhi ya mitazamo hiyo haina uzito wa akili na mantiki; na inavyoonekana ni ya kufurutu na kupindukia mpaka. Uliofurutu mpaka zaidi kati ya mitazamo hiyo ni ule unaochukulia uzuri na ubaya wa tendo lolote kuwa unategemea amri na katazo la Mwenyezi Mungu tu juu ya jambo hilo. Kwa maana kwamba kabla ya tendo lolote kuamrishwa kutendwa au kukatazwa kufanywa na Mwenyezi Mungu, haliwi zuri wala haliwi baya, bali amri na katazo la Mola ndivyo vinavyolifanya tendo fulani kuwa jema au baya. Nadharia na mtazamo huu ambao ni maarufu kwa jina la mtazamo wa "amri ya kidini" au amri ya Mungu umekuwapo katika ulimwengu wa Ukristo na umepata uungaji mkono wa watu wachache katika baadhi ya makundi ya Waislamu.

Waungaji mkono wa mtazamo wa amri ya kidini wanaitakidi kuwa tendo lolote lile kwa nafsi yake si zuri wala si baya; na ni pale tu Mwenyezi Mungu anapokuwa ameamrisha lifanywe ndipo tunaweza kusema kuwa ni tendo zuri. Matokeo ya kuwa na mtazamo huu ni kutupasa tuseme, ikiwa Mwenyezi Mungu ataamrisha kufanywa tendo ambalo ni wazi kabisa ni ovu, mathalani kumtesa mtu asiye na hatia yoyote, tendo hilo litakuwa sahihi kabisa kiakhlaqi. Halikadhalika kama Mwenyezi Mungu atamchukua Mtume wake na kumtia kwenye moto wa Jahanamu hatokuwa amefanya jambo baya; kwa sababu zuri na jema ni lile analofanya Mwenyezi Mungu au analoamrisha lifanywe. Nadharia na mtazamo wa amri ya dini au ya Mungu umepingwa na kukataliwa na wanazuoni wengi wa akhlaqi, wa dini na wa Usekulari kutokana na masharti yake yasiyo na mantiki.

 

Kati ya rai na mitazamo tofauti kuhusu akhlaqi za kidini kuna nadharia nyengine yenye kutoa mguso, ambayo inaweza kuzivuka vizuri changamoto za kifalsafa na kimantiki kuhusu namna ulivyo uhusiano baina ya dini na akhlaqi na badala yake unaanika na kuweka wazi kasoro za akhlaqi za Usekulari. Wenye mtazamo huu kuhusu akhlaqi za kidini wanasema uzuri na ubaya wa amali na tendo fulani unahusiana na dhati ya tendo na amali yenyewe bila kujali amri na katazo la Mwenyezi Mungu. Ukweli ni kwamba Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya tendo fulani kwa sababu kwa dhati yake, tendo hilo ni zuri, na anakataza tendo kwa sababu tendo hilo kwa dhati yake ni baya na ovu. Nadharia na mtazamo huu unapingana na mtazamo unaoamini kwamba tendo fulani ni zuri kwa sababu Mwenyezi Mungu ameamrisha lifanywe. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 28 ya Suratul A'raf kwamba:" Na wanapo fanya mambo machafu husema: Tumewakuta nayo baba zetu, na Mwenyezi Mungu ametuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi mambo machafu."

Kulingana na mtazamo huu, thamani za kiakhlaqi zinaitangulia amri ya kidini na zinajitegemea bila ya kuwa na utegemezi nayo. Japokuwa itikadi na mtazamo huu haumaanishi kukana nafasi muhimu ya dini katika akhlaqi, lakini Wasekulari wameitumia maudhui hii kutoa hitimisho lisilo na mantiki ambalo ni kuzifanya akhlaqi kuwa ni kitu kisichoihitajia dini. Watetezi wa mtazamo huu wanasema nafasi yenye umuhimu mkubwa mno ya dini katika akhlaqi, kwanza kabisa ni ya maarifa ya utambuzi wa mambo, kwa maana kwamba bila ya amri na katazo la Mwenyezi Mungu, mtu hawezi kuielewa mwenyewe mifano yote halisi ya kheri na shari na dhulma na uadilifu.

Hakika ni kwamba ni kwa kupitia akili na fitra aliyopewa na Mwenyezi Mungu, ndipo mwanadamu huweza kudiriki na kutambua uzuri wa uadilifu na ubaya wa dhulma; bali huweza hata katika mambo mengi kutambua mifano halisi ya uadilifu na dhulma. Kwa mfano kila mtu anajua kuwa "kumnyanyasa mtoto" ni kitendo kiovu kiakhlaqi. Lakini si mambo yote yako wazi na wadhiha kufahamika na akili na fitra ya mwanadamu kwamba ni maovu kiakhlaqi kama ilivyo kumnyanyasa mtoto. Tuchukulie mfano suala la mgonjwa kujiua wakati madaktari wanapokuwa hawana matumaini tena ya yeye kupata afueni, na kuendelea kuishi kwa mgonjwa mwenyewe likawa ni jambo thakili. Kwa maulama wa akhlaqi, hili lingali ni moja ya mambo yanayowawiya vigumu kuyatolea hukumu na uamuzi. Vilevile kuhusu "kutoa mimba" wakati uja uzito unapokuwa hauhatarishi maisha ya mzazi wala kiumbe kilichomo tumboni mwake, ni mfano mwengine mgumu na ambao unaendelea kuzusha makelele na majadiliano.

 

Tukumbuke pia kuwa kuna mambo mengi katika tabia, hulka na silka za watu ambazo katika jamii au nchi fulani yanaonekana kuwa ni mazuri na mema kiakhlaqi, lakini yanachukuliwa kuwa mabaya na maovu kiakhlaqi katika jamii na nchi nyengine.

Masuala yanayohusu akhlaqi za mambo ya kunga na ngono ni mfano mmoja wa wazi kabisa wa masuala hayo. Hitilafu hizi za mitazamo hazitokei baina ya watu wa kawaida tu, bali zimekuwepo pia hata baina ya wanafikra na wanahekima wa kaumu na jamii, waliokuwa wakiishi katika zama moja na zenye mazingira yanayofanana. Wote hao wamekuwa na fikra na rai zinazogongana kuhusu matendo mengi ya watu kwa kuyahukumu kama ni mazuri au mabaya kiakhlaqi. Hii inaonesha, kwa kutegemea akili na uwezo wake wa utambuzi tu, mwanadamu hawezi kutambua kwa usahihi kabisa mifano hai na halisi ya kheri na shari; na kwa sababu hiyo ndio maana baadhi ya wakati hunasa kwenye mtego wa kuzifanya akhlaqi kuwa si kitu mutlaki cha uzuri na ubaya na kuonesha kuwa haiwezekani  kuwa na usuli na misingi thabiti ya kiakhlaqi. Wakosoaji wa hilo wanasema matokeo ya kuzifanya akhlaqi kuwa ni kitu kisicho kizuri au kibaya mutlaki ni kuporomosha kikamilifu misingi ya akhlaqi.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 27 ya kipindi cha Usekulari Katika Mizani ya Uislamu imemalizika. Hivyo tusite hapa kwa leo hadi juma lijalo inshaallah tutakapoendelea na sehemu ya 28 ya kipindi hiki. Nakushukuruni kwa kunisikiliza, na nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Tags