El Fasher, Hadithi ya Kuanguka Mji
https://parstoday.ir/sw/news/event-i132914-el_fasher_hadithi_ya_kuanguka_mji
El Fasher sio jina la mji tu; bali ni jeraha lililowazi la dhamiri ya dunia. Katika kipindi chetu leo, tunasimulia mzingiro uliozuia mkate wa watu, na hujuma iliokata pumzi za watoto. Ni simulizi fupi lakini sahihi, inayotuhimiza sisi sote kuelekeza mazingatio yetu kwa maafa ya binadamu yanayotokea huko Sudan....
(last modified 2025-11-07T16:33:47+00:00 )
Nov 07, 2025 16:32 UTC
  • El Fasher, Hadithi ya Kuanguka Mji

El Fasher sio jina la mji tu; bali ni jeraha lililowazi la dhamiri ya dunia. Katika kipindi chetu leo, tunasimulia mzingiro uliozuia mkate wa watu, na hujuma iliokata pumzi za watoto. Ni simulizi fupi lakini sahihi, inayotuhimiza sisi sote kuelekeza mazingatio yetu kwa maafa ya binadamu yanayotokea huko Sudan....

Katika kipindi hiki, tunakupeleka kwenye kiini cha maafa ya El Fasher; mji uliloko Darfur Kaskazini nchini Sudan, ambao siku chache zilizopita ulishuhudia ukatili wa kutisha. Jina la mji huo sasa linaambatana na maneno kama vile kuzingirwa, njaa, kulazimishwa watu kuhama makazi yao na mauaji ya halaiki.

Mji wa El Fasher uliokumbwa na mauaji ya halaiki 

El Fasher, uliokuwa tumaini la mwisho la watu wa Darfur Kaskazini, hatimaye umeangukia mikononi mwa waasi baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu. Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyojumuisha wapiganaji wa mataifa kadhaa chini ya uongozi wa Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, viliingia katika mjii huo na kuvuka mipaka yote ya ubinadamu kwa kufanya ukatili usio na mfano na pia kusababisha umwagaji damu wa kutisha. Ripoti zinasema, baada ya kuudhibiiti kikamilifu mji wa El Fasher, vikosi vya Mohamed Hamdan Dagalo viliua raia wasiopungua elfu mbili, wakiwemo wanawake na watoto waliokimbia makazi yao, katika kipindi cha siku mbili tu.

Ili kupata sura walau isiyo kamili ya janga hilo, tunalazimika kurudi nyuma kidogo hadi takriban miezi 18 ya kuzingirwa mji huo ambayo iliutenga kabisa mji huo na  dunia nyingine. Barabara za mji zilifungwa, malori ya misaada ya kibinadamu yalisimamishwa, bei ya mkate ilipanda juu kupita kiasi na watoto wa mji, badala ya kucheza mitaani, walikuwa wakikariri orodha ya dalili za utapiamlo. Mashirika ya misaada ya kibinadamu, hasa UNICEF, yameonya mara kwa mara kwamba: "El Fasher imekuwa kitovu cha mateso ya watoto; na utapiamlo, magonjwa na ukatili vinachukua uhai wa watu kila siku." Hata hivyo, licha ya tahadhari hizo, mzingiro uliendelea na mji ukakata pumzi polepole.

Tunapozungumzia kuzingirwa kwa muda mrefu, hatuzungumzii tu uhaba wa chakula. Kuzingirwa kunasababisha uharibifu wa muundo wa miji, hospitali huzuiliwa kupata dawa, shule zinakosa walimu, maji ya kunywa na umeme vinakatwa na familia hupoteza matumaini. Katika hali kama hiyo, shambulio la ghafla linaweza kugeuka kuwa janga kubwa kwa wakazi wa mji au eneo linalozingirwa.

Simulizi za mashahidi zinasema, mji wa El Fasher uliangukia mikononi mwa waasi wa RSF baada tu ya kushambuliwa na wapiganaji wa kundi hilo. Mitaa ya mji ambayo hapo awali ilikuwa njia za kufikisha mkate na dawa kwa raia, iligeuka kuwa njia za vifo na mito ya damu. Hospitali hazikuwa salama; na kumetolewa ripoti za mauaji ya halaiki katika vituo vya matibabu ambavyo vilipaswa kuwa maeneo ya kuokoa maisha na uhai wa watu badala ya kuwa nyumba za mauaji na maangamizi. Vituo hivyo vya afya vilikuwa medani za mauaji ya kiholela, kupigwa risasi wagonjwa na wauguzi waliokuwa wakiomba msaada na miili iliyokuwa imerundikana ardhini katika ukimya wa vyombo vya habari na jamii ya kimataifa kwa ujumla.

Katika mikanda ya video zilizotoka nje ya mji wa El Fasher, ungeweza kuona nyuso za watu ambao hawakujua kabisa masuala ya siasa wala vita; kitu pekee walichokitaka ni kubakia hai na kupata kipande cha mkate. Jibu lilikuwa ukatili wa kutisha na kumiminiwa risasi na watu ambao wamerithi ukatili wa kundi la Janjaweed katika joho na vazi lililopewa jina na Vikosi vya Msaada wa Haraka, (RSF). 

Baada ya kurushwa hewani picha na simulizi za maafa ya El Fasher, kiongozi wa kundi la RSF, Mohamed Hamdan Dagalo, alitosheka kwa kueleza masikitiko yake yasiyo na maana na kujaribu kuhalalisha uhalifu huo kwa kudai kwamba "tumelazimishwa vita hivi." Lakini, katikati ya uharibifu huo, kulisikika ujumbe mwingine ambao ulikuwa kusambazwa kwa makusudi picha za kunyongwa watu viwanjani na mauaji ya kutisha ambavyo bila shaka vinaweza kuelezwa kwa maneno kama "uhalifu wa kivita," "maangamizi ya kikabila," na "uhalifu dhidi ya binadamu." Picha na video hizo hazikuwa tu kielelezo cha ukatili usio na mfano, kwani wachambuzi wengi wanaziona kama kitendo kilichopangwa kwa makusudi ili kuibua hofu na wahka katika jamii, na vita vya kisaikolojia kwa wakazi wa miji itakayolengwa baadaye, hasa eneo la Kordofan. Hii ni mbinu ya zamani inayogeuza hofu kuwa utangulizi wa kusonga mbele kwenye maeneo mengine na kufanya kifo na mauaji kuwa wenzo wa ushindi.

Manusurau wa mauaji ya halaiki katika mji wa El Fasher

Katika fasihi ya vita visivyo na ulinganifu, "ugaidi wa kisaikolojia" ni sehemu ya nyenzo za maendeleo ya haraka. Wakati mji unapotekwa na kudhibitiwa na picha za kutisha zikasambazwa haraka, ujumbe kwa miji inayofuata huwa uko wazi: "Usipinge wala kupambana, la sivyo gharama yake itakuwa kubwa zaidi." Inasikitisha kuona kwamba, huu ndio mtindo tunaoushuhudia katika baadhi ya migogoro ya dunia ya sasa.

Kwa hivyo, El Fasher haikuwa uwanja wa damu tu; bali pia ilikuwa uwanja wa simulizi. Katika siku za kutekwa kikamilifu mji huo, na wakati ulipoanza mchezo wa kukana habari za kufanyika uhalifu na kisha kukiri mbele ya picha za sateilaiti zilizoonyesha "mrundikano wa miili ya maiti za watu" "ardhi iliyobadilika kwa damu" na vilevile madimbwi ya damu na makaburi ya halaiki, ukweli ulikuwa wazi sana kiasi kwamba, kuukana kungekuwa kitendo kisicho cha kimaadili.

Hemedti, kamanda wa RSF ambaye alijaribu kupunguza mzigo wa kimaadili wa janga hilo kwa "kueleza masikitiko yake" baridi, amehalalisha ukatili huo kwa kudai kuwa ni vita vya "kulazimishwa." Lakini ukweli na hali halisi vimefichua mfumo wa vitisho na kueneza hofu, kuanzia usambazaji wa makusudi wa picha za kunyongwa watu na mauaji ili kuvunja ari na moyo wa mapambano wa wakazi wa miji inayofuata, hasa Kordofan. Na katika upeo mpana zaidi, hali hiyo inaakisi dunia ambayo taasisi zake zimeonekana kuwa dhaifu zaidi katika mtihani wa kulinda uhai wa raia wa kawaida.

kiongozi wa kundi la RSF, Mohamed Hamdan Dagalo

Mwandishi wa habari aliyekuweko huko El Fasher anaripoti kuwa: “Kandokando ya kambi ya wakimbizi za Tawila, nilizungumza na bibi ambaye ndio kwanza alikuwa amewasili eneo hilo. Alisema: "Hatukuwa na maji, hatukuwa na mkate, hatukuwa na dawa. (Waasi wa RSF) walipokuja, walikuwa wakipiga risasi kutoka juu ya paa za nyumba. Walivunja milango ya nyumba. Tulikuwa tukikimbia ovyo… tulikuwa tukikimbia tu…” Katika upande wa pili, baba mmoja alikuwa ameshika kipande cha karatasi mkononi mwake. Karatasi hiyo ilikuwa na maagizo ya dawa yaliyoandikwa na daktari lakini bila ya kuwa na dawa. Alisema: "Mwanangu alikuwa na homa, nilimpeleka hospitalini, lakini...lakini..." Babu alikatiza maneno yake, si kutokana na uhaba wa maneno, la hasha, bali kutokana na uchungu wa kumbukumbu hiyo....

Nchi ya Sudan imekuwa ikikodolewa macho kutokana na eneo lake maalumu la kijiografia na kisiasa; kuanzia pwani ya Bahari Nyekundu hadi kuungana kwake na Pembe ya Afrika na kadhaiika. Katika ulimwengu wa leo, ambapo miundo ya kikanda na kimataifa imenaswa katika maslahi yanayoingiliana au imepoteza nguvu zake za kujilinda, nyayo za baadhi ya wachezaji wakubwa wa kikanda zinaonekana zaidi katika simulizi za kiuchambuzi. Kwa mfano, kwa mujibu wa imani ya baadhi ya wachambuzi, kutokana na mtazamo wa mafundisho na sera ya usalama ya utawala wa Kizayuni wa Israel, kudhoofishwa kwa nchi za kandokando yako ni mojawapo ya njia za kudhibiti vitisho vinavyoweza kutokea. Kwa msingi huo, katika mlingano kama huo, msukosuko wowote nchini Sudan huwa sehemu ya fumbo kubwa linalosukwa na wachezaji wengine,  moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Katika muktadha huo, jina la moja ya nchi ndogo za Kiarabu kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi linaonekana zaidi katika kusababisha mgogoro nchini Sudan. Ingawa nchi hiyo inazitaja shughuli zake nyingi kuwa ni za "kibinadamu na upatanishi", lakini kwa muda mrefu imekuwa ikifanya kazi nchini Sudan kwa ajili ya "kupata ushawishi wa kijiografia-kistratijia katika Bahari Nyekundu," "kudhibiti eneo hilo na kupata faida zinazotokana na biashara ya dhahabu," "kuwadhibiti wapinzani wa kiaidiolojia na wa kikanda" na kuimarisha "mradi wa bandari na vifaa vya kilojestiki." Vilevile tangu mwanzo wa vita vya ndani vya Sudan (2023), safari nyingi za ndege za mizigo zimerekodiwa kutoka nchi hiyo ndogo za Kiarabu kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi hadi ukanda wa mpaka wa Chad (uwanja wa ndege/njia zinazozunguka mji wa Amdjarass), ambazo baadhi, kama wanavyosema wanadiplomasia na wataalamu, zimefanyika kwa ajili ya kupeleka silaha na zana za kivita kwa waasi wa RSF.

Sambamba na kudhibitiwa kikamiliifu mji wa El-Fasher, kumetolewa ripoti za kuwepo "msaada wa kigeni" kwa waasi wa RSF, sambamba na simulizi la uhalifu unaofanywa na kundi hilo; ingawa kiwango cha ushiriki wa moja kwa moja wa kila mhusika unatofautiana kulingana na ripoti tofauti.

Kwa vyovyote vile, katika mtazamo wa kimkakati, El Fasher ni kiunganishi muhimu huko kaskazini mwa Darfur, kitovu cha njia za misaada na kituo cha makumi ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao. Kwa hivyo kudhibitiwa kikamilifu mji huo si kubadilishwa bendera kwenye jengo la vagana wa mji pekee; bali ni fursa kwa wavamizi kushiriki katika "uhandisi wa idadi ya watu," kwa ajili ya kufukuza kundi moja na kuliwe kundi jingine mahali pake. Uzoefu huo mchungu ulishuhudiwa pia Darfur miongo miwili iliyopita. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana waangalizi wanayataja yanayojiri hivi sasa katika eneo hilo kuwa ni "mauaji ya kimbari" au "maangamizi ya kikaumu."

Ukweli ni kuwa, El Fasher sio kesi ya kupelekwa mahakama tu, bali pia ni kioo kinachoakisi hali ya dunia yetu ya sasa. Kurudi tena wanadamu wa karne hii ya 21 kwenye mbinu za kikatili za karne zilizopita ni ishara ya kuhuzunisha ya kuyumba na kudhoofika mfumo wa kimaadili na kisheria wa dunia ambao baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulipaswa kuwa chini ya utawala wa sheria na uadilifu.     

Tunapozungumzia mauaji ya watu elfu mbili katika siku mbili, lazima tukumbuke kwamba takwimu zinaweza kuwa kubwa zaidi. Kwa sababu El Fasher imezama katika giza la kutokuwa na mawasiliano; simu zilikatwa, ripoti zilifika kwa kuchelewa na takwimu kamili za idadi ya watu waliouawa zimepotea katika sauti za milipuko ya mabomu na risasi. Hata hivyo, kuna mwafaka kwamba: "Idadi ya waliouawa ni kubwa; mamia wameuawa wakiwa hospitalini na mitaani; na maelfu katika mji mzima wa El Fasher." Makadirio haya, ingawa si kamili, lakini yanatoa picha ya ukubwa wa uhalifu uliofanyika.

Wasikilizaji wapendwa! El Fasher ni jina ambalo linapaswa kubaki katika kumbukumbu walimwengu, sawa kabisa na majina ya Gaza, Sarajevo, Rohingya na kadhalika. Mashirika ya kutetea haki za binadamu na yale ya Umoja wa Mataifa yamezungumzia mengi kuhusu "mauaji ya viwanjani," "mashambulizi dhidi ya hospitali," na "maangamizi ya kikabila." Vyombo vya habari vya kuaminika vimeripoti idadi ya kutisha ya watu waliouawa, na picha za setilaiti zimethibitisha suala hilo. Lakini leo, kazi yetu si kuomboleza tu; Lazima tugeuze huzuni yetu kuwa vitendo: kuwa harakati za kupigania amani, kuwa vuguvugu la kuimarisha utulivu, na kuwa azma ya kutoa msaada kwa wanadamu wenzetu wanaosumbuliwa na maafa...   

Unaweza kusikilizai tena kipindi hiiki katika mtandao wetu wa parstoday.ir/sw.