Rwanda yatumia roboti kukabiliana na janga la COVID-19
Rwanda yatumia roboti kukabiliana na janga la COVID-19
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangaia baadhi ya mafanikio katika nyuga za sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika na niliyokuandalieni kwa leo.
@@@
Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu wa Iran amesema, wakati mripuko wa virusi vya corona ulipozuka nchini kulikuwepo na uhaba fulani wa vifaa vya afya, lakini kwa kutegemea uwezo wake wa ndani, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliweza ndani ya muda wa chini ya miezi miwili kubadilika na kuwa msafirishaji na muuzaji badala ya kuagiza bidhaa za tiba kutoka nje.
Saeed Namaki aliyasema hayo hivi karibuni katika hafla ya uzinduzi wa mavazi ya kinga kwa ajili ya timu ya utabibu yaliyotengezwa hapa nchini na akakumbusha kwamba: Wakati nchi ilipokuwa ikikabiliwa na uhaba wa barakoa na mavazi hayo, hakuna daktari wala muuguzi hata mmoja wa Kiirani aliyewapuuza wananchi kwa sababu ya uhaba wa suhula hizo.
Namaki ameongeza kuwa, katika kipindi hiki cha corona, katika baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani watu wengi wametaabika na kutangatanga nje ya mahospitali huku wazee wakongwe wanawake kwa wanaume wakiachwa bila kushughulikiwa, lakini nchini Iran hakujatokea mtu hata asiye na mahali pa kudumu pa kulala aliyeachwa nje ya hospitali.
Katika wiki na miezi ya hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata mafanikio makubwa na muhimu katika uwanja wa kudhibiti maradhi ya COVID-19. Akizungumzia suala hilo mwezi Mei pambizoni mwa kikao cha 73 cha Shirika la Afya Duniani WHO na ambacho kilifanyika kwa njia ya mawasiliano ya video, Christoph Hamelmann, Mwakilishi wa WHO nchini Iran alisisitiza kwamba hakuna tatizo lolote nchini Iran katika uwanja huo na kwamba wagonjwa wote wanapata huduma maalumu na za dharura katika kukabiliana na maradhi hayo. Hamelmann ameashiria msaada wa Umoja wa Mataifa na mashirika yaliyo chini ya umoja huo ikiwemo WHO kwa Iran na kusema: Hivi sasa Iran imeongeza kiwango cha uzalishaji wa nguo za kujikinga na vijidudumaradhi, maski na vifaa vingine vya kiafya na kitiba zikiwemo mashine za kuwasaidia wagonjwa kupumua (ventilator) na hata kuuza nje vifaa vya kutambua walioathirika na ugonjwa wa corona.
@@@
Shirika la Afya Duniani, WHO, limesitisha kwa muda majaribio ya dawa inayotumika kutibu Malaria hydroxychloroquine kama tiba ya ugonjwa wa COVID-19 au corona.
Katika taarifa, WHO imesema: “Majaribio yanayofanyiwa dawa ya ugonjwa wa malaria Hydroxychloroquine ili kuona iwapo inaweza kutibu COVID-19 yamesitishwa kutokana na hofu ya usalama wake. “
Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema utumizi wa hydroxychloroquine una madhara kwa watumizi ikiwa ni pamoja na matatizo ya moyo.
Wiki iliopita, utafiti uliofanywa na jarida la tiba duniani Lancet ulibaini kwamba hakuna faida yoyote inayopatikana katika matumizi ya dawa ya Hydroxychloroquine na kwamba utumizi wake unaweza kuongeza idadi ya vifo miongoni mwa wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na maambukizi ya Corona.
Hydrochloroquine ni dawa salama ya kutibu ugonjwa wa malaria lakini hakuna majaribio yoyote ambayo yamependekeza matumizi yake katika kutibu COVID-19.
Hivi karibuni Rais wa Marekani Donald Trump alisema kuwa anatumia dawa hiyo na kuwa inaweza kuzuia virusi vya Corona.
Hata hivyo watafiti wanasema kwamba wagonjwa wa COVID-19 hawapasi kutumia hydroxychloroquine.
@@@
Rwanda imeagiza roboti kutoka Ubelgiji ili kuzitumia katika vita dhidi ya janga la COVID-19 ili kupunguza muingiliano kati ya madaktari na wagonjwa. Hatua hiyo pia inatarajiwa kupunguza hatari ya kuambukizwa wahudumu wa afya na virusi hivyo.
Roboti hizo zimezinduliwa kwa ushirikiano wa wizara ya afya na shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo UNDP katika hospitali ya Kanyinya inayotibu COVID-19.
Roboti hizo zitaweza kupima hali joto, kukusanya data za wagonjwa, kuwatambua watu wasiovalia mask au barakoa, na kuwapa wagonjwa chakula na dawa. Roboti hizo zimepewa majina ya Kinyarwanda ambayo ni Akazuba, Ikirezi, Mwiza, Ngabo, and Urumuri. Wizara ya Afya ya Rwanda inasema roboti hizo zina uwezo wa kuwachunguza watu 50 hadi 150 kwa dakika moja na zina uwezo wa kupeleka chakuka na dawa katika vyumba vya wagonjwa.
@@@
Nchi mbali mbali duniani zinatumia aplikesheni za simu za mkononi kuwafuatilia wagonjwa wanaoshukiwa kuambukizwa ugonjwa wa COVID-19 au corona.
Serikali ya Kenya inatumia simu za mkononi kuwafuatilia wagonjwa wanaoshukiwa kuambukizwa COVID-19. Aplikeshini hiyo imetengenezwa na Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta na inaweza kuwafuatilia wale walioambukizwa COVID-19 na kubainisha waliko pamoja na watu waliokaribiana nao. Hatua hizo vilevile zinatumiwa katika nchi nyingine mbalimbali katika kufuatilia mlipuko wa virusi hivyo, zikiwemo Singapore, Australia, Korea Kusini, China na Iran.
Pamoja na kuwa aplikesheni kama hizo zinatoa msaada mkubwa katika kukabiliana na COVID-19 lakini Marekani imechukua hatua ya kuwawekea vikwazo Wairani wasiweze kunufaika na aplikesheni hiyo.
Mwezi Mei, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano katika Wizara ya Afya ya Iran alitangaza kuwa aplikesheni ya Kiirani ya kupambana na COVID-19 inayojulikana kama Mask imefutwa katika aplikesheni ya Google Play kutokana na vikwazo vilivyo dhidi ya binadamu vya Marekani. Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano katika Wizara ya Afya ya Iran aliyasema hayo katika ujumbe wa Twitter na kuongeza kuwa: "Aplikesheni ya Mask imefutwa katika jukwaa la Google Play kutokana na vikwazo vilivyo dhidi ya binadamu vya madola ya kinyama ya Magharibi."
Aplikesheni ya Mask inatumiwa na Wizara ya Afya ya Iran kubaini miji na maeneo yenye corona, hali ya karibuni kabisa ya maambukizi katika kila hatua na umbali wa maaeno yaliyo na maradhi hayo.
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba aliyotoa hivi karibu aliashiria matamshi ya seneta mmoja wa nchi ya Magharibi ambaye alisema 'Magharibi ya Kinyama imehuishwa' na kuongeza kuwa sisi tunasema Wamagharibi wana moyo wa kinyama kinyume na dhahiri yao yenye kung'ara kwa suti na uturi, wao wanakana lakini hivi karibuni mmoja wao alikiri wazi kuhusu ukweli huu."
Vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu vya Magharibi na baadhi ya nchi za Ulaya dhidi ya Iran ambavyo vinajumuisha hata dawa na masuala ya tiba vimewasababishia matatizo makubwa watu wa Iran hasa wagonjwa wa COVID-19. Kutokana na kutabiri ukatili wa Marekani Iran imechukua hatua kadhaa kukabiliana na vikwazo hivyo vya Marekani. Kwa msingi huo hata baada ya Marekani kufuta aplikesheni hiyo ya Mask katika jukwaa la Google Play, Wairani sasa wanaweza kuipakua aplikesheni hiyo katika majukwaaa kadhaa ya ndani ya nchi ikiwa ni pamoja na jukwa la Bazaar ambalo hutumiwa na aghalabu ya aplikesheni za Kiirani.
@@@
Na hadi hapo wapenzi wasikilizaji ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya Sayansi na Teknolojia kwa leo.