Alkhamisi tarehe 25 Juni mwaka 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 3 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Juni 25 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita kundi la watumwa wa Marekani wenye asili ya Afrika ambao waliachiwa huru na wamiliki wao wazungu wa nchi hiyo, walirejea Afrika na kuanzisha makazi katika ardhi ambayo leo hii inajulikana kama Liberia. Raia hao weusi wa Marekani walianzisha harakati ya ukombozi mwanzoni mwa karne ya 19 kwa lengo la kujiondoa utumwani na kuunda nchi yao. Kwa sababu hiyo kundi la Wamarekani weusi wenye asili ya Afrika lilihamia Magharibi mwa Afrika na kuasisi nchi ya Liberia kwa kusaidiwa na taasisi ya wahamiaji, baada ya kuwa utumwani kwa miaka mingi huko Marekani. Awali Liberia ilikuwa ikiendeshwa kama moja ya majimbo ya Marekani, lakini mwaka 1847 nchi hiyo iliasisi mfumo wa jamhuri na rais wake wa kwanza akawa Joseph Roberts, mtumwa kutoka jimbo la Virginia.
Katika siku kama hii ya leo miaka 125 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Fesharaki Isfahani, faqihi, mchamungu na mwanazuoni mkubwa wa zama zake. Sayyid Fesharaki Isfahani alizaliwa mwaka 1253 Hijria Qamaria katika kijiji cha Fesharak karibu na Isfahan na alianza kusoma Qur'ani na elimu ya msingi akiwa na umri wa miaka 6. Alielekea Karbala na baadaye Najaf huko Iraq akiwa pamoja na kaka yake wakati alipokuwa na umri wa miaka 11 na huko alipata elimu kwa wanazuoni wakubwa na kukwea haraka daraja za juu za kiroho na uchamungu. Ayatullah Fesharaki alikataa kuwa kiongozi wa juu ya kidini wa Waislamu wa madhehebu ya Shia kutokana na uchamungu wake mkubwa na akakhitari kuendelea kutoa darsa na kulea vizazi vya wanazuoni na maulamaa.
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita, yaani tarehe 25 Juni mwaka 1975, Msumbiji ilipata uhuru. Mwishoni mwa karne ya 15 kundi moja la mabaharia wa Kireno likiongozwa na mvumbuzi mashuhuri Vasco da Gama lilifika Msumbiji na kuanzia hapo mabaharia hao wakaanza kuikoloni nchi hiyo, ukoloni ambao uliendelea kwa karne tano. Wareno walianza kupora maliasili na utajiri wa Msumbiji na makumi ya maelfu ya wananchi wapigania ukombozi wa Msumbiji waliuawa wakitetea nchi yao.
Siku kama ya leo miaka 70 iliyopita, kufuatia harakati za kichokozi za Marekani katika eneo la Peninsula ya Korea, Korea Kaskazini iliishambulia Korea Kusini na kusonga mbele haraka upande wa nchi hiyo hasimu. Hata hivyo kupasishwa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi nyingine 15 zilituma askari wao kwa ajili ya kukabiliana na kuzuia kusonga mbele zaidi Korea Kaskazini sambamba na kuisaidia Korea Kusini. Hatimaye majeshi hayo ya kigeni kwa kushirikiana na Korea Kusini yaliweza kuizuia kusonga mbele Korea Kaskazini. Hata hivyo hatua ya China ya kuingilia kati vita hivyo kwa maslahi ya Pyongyang, kulifanya uvamizi wa Marekani na vikosi vya kigeni kufikia tamati katika eneo hilo. Ni baada ya hapo ndipo kukaanza mchakato wa mazungumzo ambapo mwaka 1953 kulitiwa saini makubaliano ya usitishaji vita hivyo. Hata hivyo hadi sasa mkataba rasmi wa amani baina ya Korea mbili bado haujatiwa saini na daima hali ya ushindani imeendelea kushuhudiwa baina yao, huku Marekani ikiendeleza siasa zake za uchochezi katika eneo hilo.