May 18, 2025 02:28 UTC
  • Jumapili, 18 Mei 2025

Leo ni Jumapili 20 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1446 Hijria ambayo inasadifiana na 18 Mei 2025 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1007 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya kauli za kihistoria alizaliwa Omar Khayyam msomi, malenga na Aarif mashuhuri wa Kiirani. Abul-Fat'h Omar bin Ibrahim Khayyam Neishabouri alikuwa mwanafalsafa, mwanahisabati, tabibu, malenga na mwandishi mkubwa wa Kiirani aliyeishi mwishoni mwa karne ya tano na mwanzoni mwa karne ya sita Hijria. Omar Khayyam aliondokea kuwa mashuhuri zaidi kutokana na kubobea katika elimu za tiba, nujumu na hisabati. Hata hivyo mwishoni mwa umri wake alijulikana zaidi kutokana na mashairi yake. Siku hii huadhimishwa nchini Iran kama siku ya kumbukumbu ya Omar Khayyam.

Kaburi la Omar Khayyam

 

Miaka 990 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 20 Dhulqaada mwaka 456 alifariki dunia Abu Ali Qirawani, mshairi, mwanafasihi na mkosoaji wa fasihi wa Morocco. Abu Ali alijifunza mashairi, fasihi na elimu nyingi za kipindi hicho akiwa bado mdogo na baada ya hapo alielekea katika mji wa Qirawan nchini Tunisia kwa shabaha ya kushiriki katika vikao na majlisi za wasomi wakubwa. Kipindi hicho mji wa Qirawan ulikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu huko kaskazini mwa Afrika na Andalusia na wasomi wa Kiislamu na wanazuoni wengi mashuhuri walikuwa wakiishi katika mji huo. Mashairi mengi ya malenga huyo yanaakisi vipindi mbalimbali vya maisha yake ya kijamii. Mshairi huyo aligundua mbinu mpya ya kukosoa kazi za fasihi na kuacha athari nyingi katika uwanja huo.

 

Siku kama ya leo miaka 221 iliyopita, Baraza la Seneti la Ufaransa lilimpasisha Napoleon Bonaparte kuwa mfalme wa Ufaransa na kwa utaratibu huo kwa mara nyingine tena mfumo wa kidikteta ukatawala nchi hiyo ikiwa ni miaka 15 imepita baada ya ushindi wa Mapinduzi makubwa ya nchi hiyo ya bara Ulaya. Hata hivyo, mfumo wa kifalme ulifikia mwisho miaka kumi baadaye, sawa na tarehe 11 Aprili mwaka 1814, baada ya Napoleone kushindwa katika vita vyake na nchi za Ulaya na kubaidishwa. ***

 

Miaka 195 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza operesheni ya jeshi la Ufaransa kwa shabaha ya kuikalia kwa mabavu Algeria. Kisingizio cha Charles wa Kumi mfalme dikteta wa wakati huo wa Ufaransa cha kutoa amri ya kufanywa mashambulio hayo, ni eti vitisho vilivyokuwa vimetolewa miaka mitatu kabla na mtawala wa wakati huo wa Algeria akiitaka Ufaransa ilipe deni la nchi hiyo la Franc milioni saba. Hata hivyo, kinyume na ilivyodhania Paris, wananchi wa Algeria walisimama kidete katika kukabiliana na mashambulio hayo. Ijapokuwa Ufaransa ilifanikiwa kuikalia kwa mabavu Algeria na kupora maliasili na utajiri wa nchi hiyo, hatimaye nchi hiyo ya Kiafrika ilijipatia uhuru wake mwaka 1962. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 153 iliyopita, alizaliwa Bertrand Russell mwanafalsafa na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Russell alijiunga na Chuo Kikuu cha Cambridge mjini London baada ya kumaliza masomo yake ya awali. Alikuwa mpinzani mkubwa wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam, na hata kufikia hatua ya kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wa Marekani ambayo yaliyopewa jina lake la Russell. Mwaka 1950 msomi huyo alitunukiwa tuzo ya fasihi ya Nobel na alifariki dunia  mwaka 1970. ***

 

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, sawa na tarehe 18 Mei 1974, India ilifanya jaribio la kwanza la kombora lake la nyuklia katika jangwa la Rajasthan, karibu na mpaka na Pakistan. Kwa utaratibu huo baada ya nchi za Marekani, Russia, Uingereza, China na Ufaransa, India inakuwa nchi ya sita kwa kuwa na nguvu za nyuklia duniani. Miaka 24 baadaye yaani mwaka 1998 India ilifanya majaribio mengine matano ya nyuklia na kufanikiwa kutengeneza silaha za atomiki. ***

 

Na katika siku kama ya leo miaka 48 iliyopita, kwa mujibu wa azimio la Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza Kuu la Kamati ya Kimataifa ya Makumbusho, siku hii iliainishwa na kutangazwa kuwa "Siku ya Makumbusho Duniani." Moja ya malengo muhimu ya baraza hilo lilikuwa kupanuliwa makumbusho katika kona mbalimbali duniani, kuweko ushirikiano wa kila upande wa majumba ya makumbusho ulimwenguni kwa malengo ya kiutamaduni na wakati huo huo kuzuia kuangamizwa athari za kale za kiutamaduni. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, lengo  la kuanzishwa sehemu kwa jina la makumbusho ni kuhifadhi athari za kale za vizazi vilivyopita kwa ajili ya vizazi vijavyo. ***