Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu (13) +SAUTI
Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo hususan huko nyumbani Afrika Mashariki. Karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Mchango wa Maulamaa wa Kishia Katika Uislamu ambacho huwatambulisha na kuwazungumzia Maulamaa wakubwa wa Kishia, mchango wao katika Uislamu pamoja na vitabu na athari zao.
Kipindi chetu kilichopita kilimzungumzia Ali bin Hussein bin Mussa maarufu kwa jina la Sayyid Murtadha, Sharif Murtadha au Alamul Huda ambaye ni mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kishia aliyekuwa amebobea mno katika elimu za fiqihi na teolojia na alihesabiwa kuwa, miongoni mwa shakhsia wa Kishia waliokuwa na ushawishi mkubwa wa kijamii. Tulisema kuwa, Sayyid Murtadha ambaye ni kaka yake Sharif Radhii aliishi katika karne ya 4 na ya 5. Sehemu ya 13 ya mfululizo huu juma hili itazungumzia japo kwa mukhtasari historia na maisha ya Sheikh Tusi. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Abu Ja’far Muhammad bin Hassan Tusi mashuhuri kwa jina la Sheikh at-Taifah au Sheikh Tusi ni fakihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mahiri na mashuhuri wa Kishia wa elimu ya teolojia ambaye aliishi katika karne ya tano Hijria. Alizaliwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka 385 Hijria katika mji wa Tous, moja ya miji ya Iran. Sheikh Tusi alikuwa moja ya nyota zinazong’ara katika ulimwengu wa Kiislamu na Kishia ambaye ameacha athari nyingi na zenye thamani za vitabu katika elimu za fiqih, usul, hadithi, tafsiri, teolojia na kadhalika. Alikuwa mwanafunzi bora wa Sheikh Mufid na Sayyid Murtadha.
Sheikh Tusi ndiye mwandishi na mtunzi wa vitabu viwili kati ya vitabu vinne muhimu vya hadithi vya Waislamu wa Kishia vinavyojulikana kama Kutub al-Arbaa. Aidha Sheikh Tusi ndiye muasisi wa Chuo Kikuu cha Kidini (Hawza) cha Najaf al-Ashraf.
Hakuna nyaraka nyingi sana zinazoeleza maisha ya Sheikh Tusi katika kipindi cha miaka 23 ya awali. Hata hivyo hivyo kuna uwezekano mkubwa kwamba, katika kipindi hiki cha hadi kufikia umri wa miaka 23 Sheikh Tusi alikuwa akijishughulisha na kusoma elimu mbalimbali katika mji aliozaliwa wa Tous nchini Iran. Katika zama hizo, Tous ulikuwa moja ya miji minne mashuhuri ya Khorasan. Katika zama alizoishi Sheikh Mufid katika mji huo, watawala wa ukoo wa Ghazni ndio waliokuwa wakiudhibiti mji huo na Mashia waliokuwa wakiishi katika mji wa Tous walikuwa chini ya mashinikizo makubwa na hawakuwa na utulivu hata kidogo kutokana na kuandamwa na njama mbalimbali.
Kwa upande wa utamaduni mji wa Tous ulikuwa moja ya miji iliyokuwa imenawiri katika uwanja huo. Waliondokea katika mji huo malenga na wana mashairi kama Ferdowsi na wasomi kama Nasirudeen Tousi. Familia ya Sheikh Tusi kwa vizazi kadhaa wote walikuwa ni wanazuoni wa fiqihi na maulamaa wakubwa na wa kutegemewa na jamii. Mtoto wa Sheikh Tusi, alikuwa alimu na msomi mkubwa wa fiqih ambapo kutokana na nafasi yake kubwa kijamii na yenye taathira kwa hawza na chuo cha kidini, aliondokewa kutambuliwa kama Mufid Thani yaani Mufid wa Pili. Aidha mabinti wa Sheikh Mufid walikuwa wasomi na wanazuoni wakubwa wa elimu ya fiqihi. Fauka ya hayo, mjukuu wake pia baada ya baba yake, naye alikuwa kiongozi wa Chuo Kikuu cha Kidini. Kwa hakika Sheikh Tousi kutokana na kujipamba kwake kwa taqwa, elimu na uchaji Mungu aliondokea kufahamika kama mmoja wa wasomi, wanazuoni, shakhsia wakubwa na marajii waliokuwa na taathira katika zama zake.
Mwaka 408 wakati Sheikh Tusi akiwa na umri wa miaka 23 alihajiri na kuelekea Baghdad Iraq kwa lengo la kujiendeleza zaidi kielimu na kuhudhuria darsa za wasomi na walimu wakubwa na kubakia huko hadi mwishoni mwa umri wake. Sheikh Tusi alihudhuria darsa za Sheikh Mufid kwa muda wa miaka 5 na baada ya kufariki dunia mwalimu wake huyo kwa miaka mingi alihudhuria darsa za Sayyid Murtadha. Miaka 12 baada ya kuaga dunia mwalimu yaani Sayyid Murtadha, Sheikh Tusi alibakia mjini Baghdad na kubeba bendera ya uongozi wa Ushia. Historia inaonyesha kuwa, nyumba yake ilikuwa kimbilio na mahala pa matumaini ya Waislamu.
Wasomi na maulamaa wengi waliokuwawakitoka katika maeneo mbali ya ardhi za Waislamu walikuwa wakielekea Baghdad na kwenda kusoma kwa mwanazuoni huyo. Historia inaonyesha kuwa, idadi ya wanafunzi wake walikuwa zaidi ya 300 na wote walikuwa ni mafakihi na Mamujitahidi wa Kishia. Aidha walikuwemo pia mamia ya maulamaa wa Kisuni waliokuwa wanafunzi wa Sheikh Tusi.
Sheikh Tousi alibakia mjini Baghdad kwa takribani miaka 40 akijishughulisha na kazi ya kufundisha hadi mtawala wa wakati huo wa ukoo wa Seljuki aliyekuwa na chuki na upinzani mkali dhidi ya Mashia aliposhambulia maeneo ya Mashia katika mji huo na kufanya mauaji na uporaji mkubwa. Nyumba ya Sheikh Tusi nayo haikusalimika na shambulio hilo. Washambuliaji waliivamia nyumba ya Sheikh Tusi kwa lengo la kumuua. Hata hivyo baada ya kumkosa, walichoma moto vitabu pamoja na vifaa vingine vya Sheikh Tusi. Tukio hilo linadhihirisha hali ngumu na mazingira ya kutisha waliokuwa wakikabiliwa nayo wanazuoni wa Kishia katika zama hizo. Baada ya tukio hilo, Sheikh Tusi alihamia katika mji wa Najaf. Katika zama hizo, mji wa Najaf ulikuwa na mitaa kumi tu midogo ambapo idadi ndogo tu ya Mashia walikuwa wakiishi jirani na Haram tukufu ya Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Baada ya kupata utulivu kidogo, Sheikh Tusi akaanzisha Hawza ya Najaf ambayo baadaye iliondokea kuwa Chuo Kikuu kikubwa zaidi cha kidini baina ya Mashia. Hawza ya Najaf imekuwa ikiendesha harakati zake kwa zaidi ya karne kumi bila kusita na katika kipindi chote hiki, imeweza kulea na kutoa maelfu ya mafaqihi na Mamujitahidi wakubwa wa Kishia.
Kwa hakika fikra na maktaba ya Sheikh Tusi ilikuwa ni kamlisho la maktaba ya Sheikh Mufid na Sayyid Murtadh. Fikra na mitazamo yake ilitegemea hoja za kiakili na nakili. Katika karne ya 4 na ya tano kulishuhudiwa kunawiri midahalo, mijadala, makongamano ya kielimu pamoja uandishi na usambazaji wa vitabu vya tafsiri na teolojia. Sheikh Tusi naye kutokana na daraja ya juu ya kielimu aliyokuwa nayo aliteuliwa na mtawala wa wakati huo kuwa kiongozi wa kiti cha elimu ya teolojia. Sheikh Tusi ana zaidi ya vitabu 15 katika elimu ya teolojia ingawa kitabu chake muhimu zaidi katika uwanja huo kinajulikana kwa jina la Talkhis al-Shafii.
Kutokana na muda wetu kumalizika kwa leo, sina budi kukomea hapa. Tukutane tena katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wiki ijayo ambapo tutaendelea kumzungumzia mwanazuoni huyu yaani Abu Ja’far Muhammad bin Hassan Tusi mashuhuri kwa jina la Sheikh Tusi.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….