Jul 20, 2020 21:49 UTC
  • Jumanne, Julai 21, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 29 Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai 21 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita John Boyd Dunlop raia wa Uingereza, alikuwa mvumbuzi wa kwanza wa gurudumu. Dunlop alifikia hatua ya kuvumbua gurudumu la magari baada ya utafiti wa miaka kadhaa. Alifariki dunia 1921.

John Boyd Dunlop

Katika siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, yaani sawa na tarehe 21 Julai mwaka 1899, alizaliwa mwandishi mtajika wa Kimarekani kwa jina la Ernest Hemingway. Kwa muda fulani Hemingway alikuwa mwandishi huko Uingereza na Ufaransa. Hemingway alianzisha mbinu ya kuandika riwaya na tungo fupi fupi na alikuwa akitumia lugha nyepesi na inayoeleweka kwa wepesi. Mwaka 1954 mwandishi Ernest Hemingway alitunukukiwa tuzo ya Nobel katika medani ya fasihi. Hemingway alipendelea sana kuwinda na alitumia muda mwingi katika shughuki hiyo. Alifariki dunia tarehe pili Julai 1961 baada ya kujipiga risasi na bunduki yake mwenyewe ya kuwindia, wakati akiisafisha. Hivyo, mkasa wa kifo cha baba yake ukawa umejirudia kwake baada ya kupita miaka 23. Miongoni mwa vitabu maarufu vya Hemingway ni pamoja na kitabu cha "The Old Man and The Sea", "A Farewell to Arms" na "For Whom The Bell Tolls".

Ernest Hemingway

Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Mahakama ya Kimataifa ya Hague ilitupilia mbali mashtaka ya serikali ya Uingereza dhidi ya Iran baada ya hatua ya Tehran kutaifisha sekta ya mafuta hapa nchini iliyokuwa chini ya udhibiti wa makampuni ya Kiingereza. Tarehe 29 mwezi Esfand mwaka 1329 (20 Machi 1951) Bunge la Taifa la Iran lilitangaza habari ya kutaifishwa sekta ya mafuta na kukata mikono ya Uingereza katika sekta hiyo nchini Iran. Uingereza ilikuwa ikipata fedha nyingi kutokana na kupora utajiri huo na hivyo iliamua kufungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Hague. Uamuzi uliotoewa na mahakama hiyo kwa maslahi ya Iran ulizikasirisha Uingereza na Marekani ambazo mwaka mmoja baadaye ziliongoza mapinduzi na kuiondoa madarakani serikali ya Muhammad Musaddiq nchini Iran kwa shabaha ya kutwaa tena sekta hiyo ya mafuta ya Iran.  

Mahakama ya Kimataifa ya Hague

Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Julai 1954 ulitiwa saini mkataba wa kuacha vita kati ya Ufaransa na Vietnam na kukomesha ukoloni wa Ufaransa huko India na China mwishoni mwa mkutano wa Geneva. Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kuanguka ngome imara ya Wafaransa iliyojulikana kwa jina la Dien Bien Phu nchini Vietnam Mei mwaka 1954. Makubaliano ya mkutano wa kimataifa wa Geneva, yalihudhuriwa na wawakilishi wa ngazi za juu kutoka Ufaransa, Marekani, Uingereza, China, Vietnam na Urusi ya zamani. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, vikosi vya kigeni vilipaswa kuondoka Vietnam, lakini Marekani kinyume na makubaliano ya Geneva, ikaamua kutuma majeshi katika eneo hilo kwa lengo la kuzuia kuungana maeneo mawili ya Vietnam ya kaskazini na ya kusini.

Vita vya Dien Bien Phu

Na katika siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, meli ya kwanza ya biashara ya nyuklia iliyopewa jina la NS Savannah iliwekwa majini huko Marekani. Baada ya kugunduliwa atomu na wasomi kutambua nguvu kubwa na nishati ya atomiki ilijitokeza fikra ya kutumia nishati hiyo katika masuala mbalimabali. Hata hivyo inasikitisha kwamba, nishati hiyo ilitumiwa kwa mara ya kwanza kielimu katika kutengeneza mabomu ya nyuklia. Suala hilo lilichochea mashindano ya kutengeneza silaha na mabomu ya nyuklia kati ya madola makubwa duniani na kuiweka dunia katika ncha ya vita vya nyuklia. Meli ya NS Savannah ilikuwa matokeo ya jitihada za wasomi za kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani na katika siku kama hii ya leo yaani tarehe 21 Julai mwaka 1958 meli hiyo ya kibiashara iliyokuwa ikitumia nishati hiyo iliwekwa majini na kuanza kufanya kazi. NS Savannah ilikuwa meli ya kwanza iliyotumia nishati ya nyuklia kuvuka habari ya Atlantic.

Meli ya NS Savannah