Jul 21, 2020 22:15 UTC
  • Jumatano tarehe 22 Julai mwaka 2020

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Dhulhija 1441 Hijria sawa na Julai 22 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita Binti wa Mtume Muhammad (saw) Fatima al Zahraa (as) alifunga ndoa na Imam Ali bin Abi Twalib (as)

Bibi Fatima alikuwa mwanamke mwema aliyejipamba kwa sifa zote nzuri ambaye alichumbiwa na shakhsia wakubwa na watu mashuhuri wa zama hizo. Hata hivyo Mtume (saw) alikuwa akiwaambia wachumbiaji hao kwamba suala la kuolewa Fatima liko mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Hatimaye Imam Ali bin Abi Twalib alikwenda kwa Mtume na kumchumbia Bibi Fatima na baada ya kushauriana na bintiye, Mtume alikubaliana na ombi la Ali na kuwafungisha ndoa. Baada ya kufunga ndoa, watukufu hao wawili waliishi maisha ya watu wa kawaida lakini yaliyojaa upendo, masuala ya kiroho na maadili ya Kiislamu. Watukufu hao wawili waliipa jamii ya mwanadamu watu adhimu na kamili kama Imam Hassan, Imam Hussein na Bibi Zainab (as). Watukufu hao walikuwa kigezo bora cha mwanadamu kamili.

Siku kama ya leo miaka 407 iliyopita, Mikhail Ramanov alikalia kiti cha utawala wa Russia na kwa utaratibu huo, utawala wa miaka 304 wa familia ya Ramanov ukawa umeanza nchini humo. Miaka mitatu baada ya mashambulio ya vikosi vya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi alifanikwa kuvishinda vikosi hivyo na kuudhibiti mji wa Moscow. Baada ya jeshi la Poland kufukuzwa nchini humo, Mikhail Ramanov akashika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa familia ya Ramanov, Russia ilipanuka lakini kwa upande wa uchumi haikupiga hatua kubwa.

Mikhail Ramanov

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, kulitokea vita vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo. Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo nchini Italia. Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia na Austria. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita hivyo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria.

Vita maarufu vya Isonzo

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuushambulia mji wa kihistoria wa Bizerte ulioko kaskazini mashariki mwa Tunisia. Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo. Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa.

Bizerte

Siku kama ya leo miaka 18 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel ukitumia ndege zake za kijeshi uliyashambulia maeneo ya Ukanda wa Gaza. Wapalestina 16 waliuawa shahidi katika mashambulio hayo ya kinyama yaliyofanywa usiku watu wakiwa wamelala. Salah Shahada kamanda wa Brigedi ya Izzu Diin Qassam Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alikuwa miongoni mwa watu waliouawa shahidi kufuatia mashambulio hayo. Aidha miongoni mwa waliouawa shahidi walikuwamo watoto wadogo 9. Kabla ya Salah Shahada kuuawa shahidi, mwanaharakati huyo aliwahi kukamatwa na utawala dhalimu wa Israel mara kadhaa na kutiwa jela.

Salah Shahada

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita wana wa dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein, Uday na Qusay waliuawa katika maeneo ya Mosul kaskazini mwa Iraq. Baada ya Marekani na Uingereza kuivamia Iraq April 2003, Uday na Qusay pamoja na viongozi kadhaa wa utawala wa zamani wa nchi hiyo, waliukimbia mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Kufuatia kufichuliwa na watu wao wa karibu nyumba walimokuwa, vikosi vya Marekani viliishambulia nyumba hiyo na kuwauwa. Uday aliyekuwa mtoto mkubwa wa Saddam na Qusay walikuwa wakishirikiana na baba yao kutekeleza mauaji dhidi ya raia wasio na hatia wa Iraq.

Uday na Qusay Saddam