Jul 23, 2020 21:52 UTC
  • Ijumaa tarehe 24 Julai mwaka 2020

Leo ni Ijumaa tarehe 3 Dhulhija 1441 Hijria sawa na tarehe 24 Julai mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 237 iliyopita Simón Bolívar mwanasiasa na mwanamapinduzi maarufu wa Amerika ya Kusini alizaliwa huko Caracas mji mkuu wa Venezuela. Simon Bolivar alikomboa ardhi kubwa ya Amerika ya Kusini kutoka katika makucha ya ukoloni wa Kihispania. Vilevile alikuwa na mchango mkubwa katika mapinduzi ya Caracas na kufanikiwa kuiteka Bogota huko katikati mwa Colombia.

Simón Bolívar

Simon Bolivar aliteuliwa kuwa Rais na Congress iliyokuwa imeundwa kwa shabaha ya kuasisi Colombia Kubwa na alifanikiwa kuzikomboa ardhi za Colombia, Venezuela na Panama. Mwaka 1822, mapambano ya ukombozi yaliyokuwa yakiongozwa na Bolivar yalienea pia hadi Ecuador na nchi hiyo ikajiunga na Colombia Kubwa, baada ya kupata uhuru.

Miaka 218 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, alizaliwa mwandishi maarufu wa Kifaransa Alexandre Dumas. Dumas aliandika riwaya nyingi kuhusiana na mapinduzi na historia ya Ufaransa kwa kustafidi na hadithi alizosimuliwa na baba yake ambaye alikuwa jenerali wa jeshi pamoja na kumbukumbu binafsi za wananchi kuhusu mapinduzi yalitokea nchini Ufaransa.

Alexandre Dumas

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita Jumuiya ya Mataifa iliipatia mamlaka rasmi serikali ya Uingereza ya kuzidhibiti Palestina, Iraq na eneo la mashariki mwa Jordan huku usimamizi wa Syria na Lebanon ukipewa serikali ya Ufaransa. Hata hivyo Paris na London ziliafikiana katika Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya hapo juu ya kugawana utawala wa kifalme wa Othmania na uamuzi huo wa Jumuiya ya Mataifa ulihalalisha suala hilo.

Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita kikosi cha anga cha jeshi la Uingereza kiliishambulia vikali bandari muhimu ya Hamburg huko kaskazini mwa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi ya anga ya Ujerumani na Uingereza yalianza mwanzoni mwa Vita vya Pili vya Dunia na kushadidi zaidi baadaye. Kwa kadiri kwamba raia wengi wa nchi mbili hizo waliuawa katika mashambulizi hayo. Makumi ya maelfu ya raia wa kawaida waliuawa kwa umati katika mashambulizi ya kikosi cha anga cha Uingereza dhidi ya bandari ya Hamburg mbali na kuangamizwa taasisi kadhaa za kijeshi na kiuchumi.

Bandari muhimu ya Hamburg ikipigwa mabomu

Na miaka 38 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani. Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadae alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na vya kisiasa. 

Dakta Hamid Inayat