Jumamosi, tarehe Mosi Agosti, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1441 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Agosti 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 111 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Mordad 1288 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi mjini Tehran Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri mwanachuoni mkubwa ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Qaajar hapa nchini Iran. Ayatullah Fadhlullah Nouri alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mapinduzi ya katiba na alisimama kidete kupinga sheria zilizopitishwa bungeni ambazo zilikuwa zikikinzana na miongozo na mafundisho ya Uislamu.***
Miaka 97 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 11 Mfunguo Tatu Dhul-Hijja alifariki dunia Ayatullah Mirza Jawad Malaki Tabrizi ustadhi mkubwa wa akhlaqi, msomi na arif. Alizaliwa katika mji wa Tabriz moja ya miji ya Iran na baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi na ya kati alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini cha Najaf nchini Iraq. Akiwa huko alihudhuria darsa za maustadhi mahiri katika zama hizo kama Haji Agha Reza Hamadani, Akhund Khorasani, Muhaddith Nuri na Akhund Hamedani. Mwanazuoni huyo mbali na kufundisha na kulea wanafunzi wengi hakuwa nyuma pia katika taaluma ya uandishi wa vitabu. Asraru Salat, al-Muraqabaat na A'amalu al Sunna ni baadhi tu ya vitabu vya Ayatullah Mirza Jawad Maliki Tabrizi.***
Katika siku kama ya leo mika 45 iliyopita, mkutano wa wakuu wa Urusi ya zamani, Marekani na Canada na nchi za Ulaya isipokuwa Albania ulianza huko Helsinki mji mkuu wa Finland. Mkutano huo ambao ulipewa jina la Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya ulifanyika kwa lengo la kuondoa mivutano kati ya nchi za kambi ya Mashariki chini ya uongozi wa Urusi ya zamani na kambi ya Magharibi chini ya uongozi wa Marekani. Hata hivyo mkutano huo wa usalama na ushirikiano haukuwa na mafanikio muhimu katika kuzikurubisha pamoja kambi mbili hizo hasa kufuatia uvamizi uliofanywa na Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani nchini Afghanistan mwaka 1979. ***

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala wa zamani wa Iraq ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutoa azimio lolote dhidi ya utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq ambao ulikuwa ukiungwa mkono na nchi za Magharibi, kwa kutumia silaha za kemikali. Masaa kadhaa baada ya kutolewa ripoti hizo, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia tena mji wa Ushnawiye kwa mabomu ya kemikali na kujeruhi watu 2400. ***
Miaka 15 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe Mosi Agosti mwaka 2005, Fahd bin Abdulaziz mfalme wa zamani wa Saudi Arabia alifariki dunia baada ya kuugua kwa miaka mingi. Mfalme Fahd alizaliwa mwaka 1921 huko Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia. Mwaka 1967, Fahd bin Abdulaziz alikuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo na miaka minane baadaye akawa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia. Alichukua hatamu za uongozi mwaka 1982 akiwa mfalme wa tano wa silsila ya Aal-Saud baada ya kufariki dunia kaka yake, Khalid bin Abdulaziz. Wakati wa vita vya kichokozi vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Mfalme Fahd alikuwa akimuunga mkono dikteta Saddam.***
Tarehe Mosi Agosti ni Siku ya Kimataifa ya Maziwa ya Mama. Utumiaji mkubwa wa maziwa ya kopo na vyakula vya watoto vilivyotengenezwa viwandani ulikithiri sana baada ya Vita vya Pili vya Dunia hususan katika nchi zilizostawi na suala hilo limezidisha wasiwasi wa jamii ya kimataifa. Hivyo suala la kunyonyesha watoto kwa maziwa ya mama na kuzidisha uelewa wa umma kuhusu faida kubwa na za aina yake za maziwa ya mama kwa mtoto na katika usalama na afya yake lilihitajia kuchukuliwa hatua kubwa na za kimsingi. Kwa msingi huo Shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) tarehe Mosi Agosti mwaka 1990 ziliitisha mkutano katika mji wa Florence nchini Italia na kutia saini taarifa iliyosisitiza udharura wa kudumishwa, kutangaza na kusisitiza suala la kuwalisha watoto wadogo kwa maziwa ya mama. Taarifa hiyo ilitilia mkazo umuhimu wa mtoto kunyonyeshwa maziwa ya mama katika kipindi cha miezi sita ya awali ya maisha yake na taathira yake kubwa kwa afya ya mtoto na mama.***