Jul 31, 2020 22:25 UTC
  • Jumatatu tarehe 27 Julai mwaka 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 6 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Julai 27 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1183 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Dhul-Hijja mwaka 258 Hijiria, alizaliwa Abu Ali Muhammad ibn Hammam, mmoja wa maulama mashuhuri wa Iran. Ibn Hammam alikuwa akiishi mjini Baghdad, Iraq ambapo alifanikiwa kusoma elimu ya hadithi kutoka kwa maulama wakubwa wa enzi zake. Aidha msomi huyo alikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walijifunza toka kwake elimu ya hadithi na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo ameacha vitabu kadhaa katika uga wa hadithi.

Miaka 248 iliyopita, katika siku kama ya leo ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prussia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapa kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti.

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, alizaliwa mtoto wa Alexandre Dumas, (Fils), mwandishi wa vitabu na mtaalamu wa fasihi wa Kifaransa. Fils alikuwa mwana wa Alexandre Duma, Jenerali wa jeshi na mwandishi wa Kifaransa. Kipindi cha utotoni cha Fils kilikuwa cha mashaka na taabu nyingi, masaibu ambayo ameyataja pia katika athari zake zote za uandishi.

Alexandre Dumas

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, mamia ya mahujaji wa Iran na wengine kutoka nchi tofauti waliokuwa wameenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu mjini Makka na wakiwa katika hali ya kutekeleza ibada ya faradhi ya kujitenga na mushrikina, waliuawa shahidi na askari wa utawala wa Saudi Arabia. Ni vyema kukumbusha kuwa, mahujaji wa Iran kwa miaka yote huwa wanatekeleza ibada hiyo kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu na Qur'ani Tukufu, ambapo mbali na kuwasisitizia Waislamu kuungana, hutangaza kujitenga na maadui wa Uislamu hususan Marekani na utawala haramu wa Israel. Ibada hiyo ambayo hufanyika kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu, huwa na taathira kubwa katika msimu wa Hija. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Imam Khomeini mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akasisitiza sana umuhimu wa ibada ya kujitenga na mushrikina na maadui wa dini ya Kiislamu.

Mauaji ya mamia ya Mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu

Na miaka 31 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Mordad 1368 Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki kwenye kura ya maoni ambapo walipiga kura za ndio na kupasisha marekebisho yaliyofanywa katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imam Khomeini (MA) aliagiza kufanyiwa marekebisho katiba ya Iran na kuundwa majlisi kwa ajili ya kutekeleza suala hilo muda mfupi kabla ya kufariki dunia. Miongoni mwa mabadiliko hayo, ni kuondoa kipengee cha Umarjaa la kuwa sharti la kuchukua wadhifa wa uongozi wa juu nchini, kuogezwa nguvu za rais na kuondoa wadhifa wa Uwaziri Mkuu.