Aug 03, 2020 03:07 UTC
  • Jumatatu tarehe 3 Agosti mwaka 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 13 Dhulhija 1441 Hijria sawa na na tarehe 3 Agosti mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 528 iliyopita baharia wa Kiitalia Christopher Columbus alianza safari kubwa zaidi ya kiuvumbuzi. Christopher Columbus alipewa jukumu la kuvumbua njia mpya inayoelekea India katika makubaliano yaliyofikiwa kati yake na mfalme na malkia wa Uhispania. Christopher Columbus aliondoka katika bandari ya Paulus huko Uhispania akiwa na meli tatu na mabaharia 120 na hatimaye walifika katika nchi kavu baada ya kuwa baharini kwa siku 33. Baharia huyo wa Kiitalia na wenzake walidhani kuwa wamefika India. Hata hivyo walikuwa wamefika katika kisiwa kilichojulikana kwa jina la Salvador katika bara la Amerika.

Christopher Columbus

Miaka 106 iliyopita katika siku kama hii ya leo Mfereji wa Panama ulifunguliwa baada ya meli ya kwanza kupita katika mfereji huo. Mfereji wa Panama ulianza kujengwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye ujenzi huo ukakamilishwa na Wamarekani. Mfereji wa Panana ulio na urefu wa kilomita 68 unaunganisha bahari mbili za Atlantic na Pacific. 

Mfereji wa Panama

Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran. Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapinduzi ya Waislamu dhidi ya Uingereza. Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatwa mashuhuri iliyopewa jina la fatwa ya kujilinda ambayo ilihalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni.

Katika siku kama ya leo miaka 90 iliyopita, alizaliwa katika mji wa Mash'had Iran Ayatullah Sayyid Ali Sistani fakihi, alimu na marjaa taqlidi wa Kishia.  Alianza kujifunza Qur'an akiwa na miaka 5 na akiwa na umri wa miaka 11 alianza kusoma masomo ya kidini ya utangulizi baada ya kutakiwa na baba yake kufanya hivyo. Baadaye alielekea katika mji wa Qum kwa ajili ya kujiendeleza zaidi kielimu. Baadaye Ayatullah Sistani alielekea katika Chuo Kikuu cha Kidini mjini Najaf Iraq. Hii leo Ayatullah Sistani si tu kwamba, anahesabiwa kuwa marjaa mkubwa zaidi nchini Iraq bali amekuwa pia na nafasi muhimu katika kuleta umoja, mshikamno na utulivu katika nchi hiyo ya Kiarabu. 

Ayatullah Sayyid Ali Sistani

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, mwafaka na tarehe 3 Agosti 1960, nchi ya Kiafrika ya Niger ilipata uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Niger ilikuwa chini ya himaya ya Ufaransa tangu karne ya 18 na mwaka 1922 ikawa koloni rasmi la Wafaransa baada ya nchi hiyo kujenga vituo vyake vya kijeshi nchini humo. Hata hivyo taratibu wananchi wa Niger walianzisha uasi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa na hatimaye nchi hiyo ilifanikiwa kupatia uhuru katika siku kama hii ya leo. Niger iko magharibi mwa Afrika na inapakana na Libya, Chad, Mali na Benin.

Tarehe 13 Dhulhija miaka 52 iliyopita alifafriki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.

Ayatullah Agha Bozorge Tehrani

Na miaka 42 iliyopita sawa na tarehe 3 Agosti 1978 utawala wa Kizayuni ulimuuwa kigaidi Izzudin Qalq, mwakilishi wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na naibu wake huko Paris, Ufaransa. Shirika la ujasusi la utawala wa kibaguzi wa Israel Mossad liliwauwa viongozi wengi wa PLO katika miongo miwili ya 1970 na 1980 lengo likiwa ni kudhoofisha mapambano ya ukombozi wa Palestina na kuwalazimisha wapigania uhuru kufikia makubaliano eti ya mapatano na utawala huo haramu.

Izzudin Qalq