Jumanne tarehe 11 Agosti mwaka 2020
Leo ni Jumanne tarehe 21 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 11 mwaka 2020.
Tarehe 11 Oktoba miaka 491 iliyopita Martin Luther alitangaza rasmi madhehebu ya Protestant. Uprotestanti ulianzishwa na Martin Luther kama harakati ya kidini katika karne ya 16 kwenye ulimwengu wa Kikristo kwa lengo la kufanya mageuzi ya kidini. Harakati hiyo ilianza dhidi ya kanisa Katoliki na udikteta wa viongozi wa madhehebu hiyo kuhusu suala la msamaha wa dhambi unaotolewa makasisi na Papa. Martin Luther aliyekuwa Mjerumani alianza harakati hiyo ya uasi ndani ya kanisa Katoliki baada ya kufasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani tofauti kabisa na amri ya Papa kwa lengo la kuvunjilia mbali taasubu za kimadhehebu za Kikatoliki.
Miaka 112 iliyopita katika siku kama ya leo, sawa na tarehe 21 Dhulhija mwaka 1329 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Akhund Mulla Muhammad Kadhim Khorasani, mmoja wa mafakihi wakubwa wa Kiislamu wa Iran. Baada ya kuhitimu elimu yake ya mwanzo mwanazuoni huyo alisoma katika vyuo mashuhuri vya kidini vya Iran na Iraq kupata umashuhuri mkubwa katika elimu za fiqhi na usuli. Akhund Khorasani alifundisha na kulea wanazuoni wakubwa na mashuhuri kama Sayyid Abul Hassan Isfahani, Sayyid Abul Qasim Kashani, Sayyid Muhammad Taqi Khansari, Sayyin Hassan Mudarris, Sheikh Abdul Kariim Hairi, Mirza Hussein Naini na wengine wengi. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo mashuhuri ni 'Kifayatul Usul' ambacho hadi sasa ni kati ya vitabu vyenye hadhi kubwa katika somo la usulul fiqhi na kinafundishwa kwenye vyuo mbalimbali vya kidini.
Siku kama ya leo miaka 68 iliyopita Haile Selassie, aliyekuwa mfalme wa Ethiopia alitia saini azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililokuwa na lengo la kuiunganisha Eritrea na Ethiopia. Ardhi ya Waislamu ya Eritrea ambayo hapo kabla ilikuwa ikikoloniwa na Italia, katika Vita vya Pili vya Dunia ilikaliwa kwa mabavu na Uingereza. Mwezi Disemba 1950 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliidhinisha Eritrea kuongozwa kwa mfumo wa shirikisho sambamba na kuunganishwa na Ethiopia. Hata hivyo kutokana na kwamba wananchi wengi wa Eritrea hawakuridhishwa na hatua hiyo pamoja na kupuuzwa haki zao na utawala wa Ethiopia, walizidisha upinzani dhidi ya utawala wa Addis Ababa na hatimaye kuanzisha harakati ya kupigania uhuru wa nchi yao mnamo mwaka 1960. Mwaka 1993 mapambano ya wananchi wa Eritrea yalizaa matunda ambapo walishiriki katika kura ya maoni na kupiga kura ya kujitenga na Ethiopia.
Na siku kama ya leo miaka 60 iliyopita nchi ya Chad ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa na siku hii hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 wakoloni wa Ufaransa waliishambulia Chad na katika kipindi cha miaka mitatu wakaidhiiti ardhi yote ya nchi hiyo. Mwaka 1958 Ufaransa iliipa Chad hiari ya kujiongoza na miaka miwili baadaye na katika siku kama ya leo nchi hiyo ikapata uhuru kamili na kuchagua mfumo wa uongozi wa jamhuri. Nchi ya Chad inapakana na nchi za Libya, Cameroon, Sudan, Afrika ya Kati, Nigeria na Niger.