Alkhamisi tarehe 13 Agosti mwaka 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 13 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilijikomboa na kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Ilikuwa katikati ya karne ya 19 wakati nchi hiyo iliyokuwa ikijulikana hapo kabla kwa jina la Ubangi-Shari, ilipounganishwa na makoloni ya Ufaransa barani Afrika. Hata hivyo mwaka 1958, Jamhuri ya Afrika ya Kati ilipatia mamlaka ya ndani na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1960, ikajikomboa na kupata uhuru kamili.
Siku kama ya leo miaka 82 iliyopita aliaga dunia Ayatullah Sheikh Abbas Qummi, aalim na mpokeaji hadithi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa mwaka 1294 Hijria katika mji mtakatifu wa Qum huko kusini mwa Tehran. Sheikh Abbas Qummi alianza kusoma elimu ya dini akiwa huko huko Qum na baadaye alielekea katika chuo kikuu cha kidini katika mji wa Najaf nchini Iraq ili kukamilisha masomo yake. Akiwa mjini Najaf, Ayatullah Sheikh Abbas Qummi alipata elimu kutoka kwa maulamaa watajika wa hauza hiyo ya kielimu. Sheikh Abbas Qummi alirejea Iran baada ya muda ambapo alitumia muda wake wote kuandika vitabu na kufuatilia masuala ya kidini. Miongoni mwa vitabu muhimu vya mwanazuoni huyo ni Mafatiihul Jinan na Manazilul Akherah.
Tarehe 13 Agosti miaka 121 iliyopita alizaliwa Alfred Hitchcock mtengeneza filamu mashuhuri wa Kiingereza. Alionesha kazi yake ya kwanza mwaka 1920 na baadaye akaanza kujihusisha na uongozaji filamu. Filamu zake za kuogopesha na za kusisimua zilikuwa mashuhuri mno katika zama hizo. Filamu hizo zilimfanya awe mashuhuri kwa jina la the Master of Suspense. Miongoni mwa filamu zake ni The Man Who Knew Too Much na Young and Innocent. Alfred Hitchcock aliaga dunia tarehe 28 Aprili 1980.
Katika siku kama ya leo miaka 157 iliyopita aliaga dunia Frederick Eugene Delacroix, mchoraji maarufu wa Ufaransa. Eugene Delacroix alirithi kipaji cha sanaa ya uchoraji kutoka kwa mama yake. Baada ya kupoteza wazazi wake wawili akiwa kijana mdogo na kujikuta akiishi maisha magumu sana ya umasikini, aliamua kufanya juhudi kubwa katika kujiendeleza na fani yake uchoraji. Baadaye alianza kufanya maonyesho ya sanaa hiyo katika ukumbi wa jiji la Paris. Katika kipindi hicho baadhi ya watu walikuwa wakimfanyia maskhara na kumkebehi, hata hivyo hakuvunjika moyo na hatimaye kazi zake zilikuwa na taathira. Alipata umashuhuri katika kipindi kifupi na kazi zake zikapokewa sana katika jamii.
Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita, aliaga dunia Florence Nightingale, mwanzilishi wa uuguzi wa kisasa huko nchini Italia, akiwa na umri wa miaka 90. Nightingale alizaliwa tarehe 12 Mei 1820 nchini Italia. Aliishi kipindi kirefu cha ujana wake nchini Uingereza. Akiwa kijana alifanya juhudi kubwa katika kuwasaidia watu, suala ambalo alilipa umuhimu mkubwa kuliko kitu kingine chochote na hatimaye alisabilia maisha yake kwa amjili ya kuuguza wagonjwa. Bi, Florence Nightingale alikuwa muuguzi na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Alipewa lakabu ya ''Mwanamke Mwenye Taa Mkononi' kutokana na uvumilivu wake mkubwa na kujinyima usingizi kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa nyakati za usiku. Alifanya juhudi kubwa pia kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika hospitali nyingi nchini Uingereza. Kazi hiyo aliyoifanya kwa miaka mingi bila kuchoka ilimdhoofisha sana kimwili kwa kadiri kwamba alikuwa kipofu mwishoni mwa umri wake na hatimaye aliaga dunia tarehe 13 Agosti 1910.