Aug 13, 2020 22:21 UTC
  • Ijumaa tarehe 14 Agosti mwaka 2020

Leo ni ijumaa tarehe 24 Dhulhija 1441 sawa na Aggosti 14 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1432 kwa mujibu wa nukuu mashuhuri ya kihistoria Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na binti yake Bibi Fatima (AS), Ali bin Abi Twalib (AS) , na wajukuu wake wawili Hassan na Hussain (AS) waliondoka mjini Madina kwenda kufanya mdahalo na viongozi wa Wakristo wa eneo la Najran juu ya dini ya kweli. Tukio hilo linaelezwa na Mwenyezi Mungu SW katika aya za 60 na 61 za sura ya Aal Imran. Wakati viongozi wa Najran walipoona Mtume amekuja katika mdahalo huo akiwa na watu wanne tu wa Nyumba yake tukufu walipigwa na mshangao na kuelewa kwamba, dua ya mtukufu huyo ya laana kwa atakayesema urongo itakubaliwa. Katika hali hiyo askofu wa Najran alisema: "Ninaziona nyuso ambazo iwapo zitamuomba Mwenyezi Mungu aung'oe mlima mkubwa zaidi mahala pake basi dua yao itajibiwa papo hapo. Kwa msingi huo si sahihi kufanya mdahalo na watu hawa watakatifu kwani yumkini kizazi chetu chote kikaangamia." Baada ya hapo askofu huyo wa Najran alimuomba Mtume (SAW) kufanya suluhu na kusamehe. Tukio hilo la kihistoria lilidhihirisha haki na ukweli wa dini tukufu ya Kiislamu na utukufu na nafasi aali ya Ahlubait wa Mtume Muhammad (SAW).

Tarehe 14 Agosti miaka 75 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti mwaka 1945 Japan ilisalimu amri mbele ya vikosi vya Waitifaki. Kwa utaratibu huo vita vilivyokuwa vimeanza mwaka 1939 kwa mashambulizi ya Ujerumani dhidi ya Poland vikafikia kikomo. Japan na Marekani ziliingia katika vita vikali Disemba mwaka 1941. Vita hivyo vilimalizika baada ya Marekani kushambulia miji ya Hiroshima na Nagasaki kwa mabomu ya nyuklia ambayo yaliua karibu watu laki mbili. Kusalimu amri huko kwa Japan kwa hakika kulihitimisha Vita vya Pili vya Dunia.

Askari wa Japan wakisalimu amri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, nchi ya Pakistan ilijitenga rasmi na India na kujitangazia uhuru wake. Dini tukufu ya Kiislamu iliingia Bara Hindi katika karne ya 8 na sehemu ya ardhi hiyo ambayo leo inajulikana kwa jina la Pakistan ilikuwa mikononi mwa Waislamu hadi wakati ilipokaliwa kwa mabavu na Waingereza mwishoni mwa karne ya 18. Chama cha Muslim League kikiongozwa na Muhammad Ali Jennah kilianzishwa mwaka 1906 kwa lengo la kuunda serikali ya Kiislamu baada ya kuanza harakati za wananchi wa India dhidi ya mkoloni Mwingereza. Chama hicho kilifanikiwa kuwashawishi Waislamu wa India na hatimaye kiliunda nchi ya Pakistan.

Katika siku kama ya leo miaka miaka 64 iliyopita yaani tarehe 14 Agosti 1954, aliaga dunia malenga na mwandishi wa Kijerumani aliyejulikana kwa jina la Bertolt Brecht. Brecht alizaliwa mwaka 1898 Miladia katika jimbo la Ugsbourg nchini Ujerumani. Malenga na mwandishi huyo wa Kijerumani alihitimu elimu ya juu katika taaluma ya sayansi asilia (bayolojia, kemia na fikikia). Malenga huyo wa Kijerumani ameacha vitabu na picha ambazo nyingi zinaeleza kuhusu utawala wa Manazi na udhalimu waliokuwa wakiutenda. 

Na siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 14 Agosti 2006, yalimalizika mapigano kati ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikubaliwa na pande hizo mbili. Mapigano hayo yaliyoanzishwa na utawala haramu wa Israel tarehe 12 Juni 2006, yalikuwa na lengo la kuidhoofisha na hata kuisambaratisha harakati ya Hizbullah. Kusimama kidete kwa wapiganaji wa Hizbullah dhidi ya majeshi ya Israel, kulimfanya Katibu Mkuu wake Sayyid Hassan Nasrullah apate uungaji mkono mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kukabiliwa na mapambano makali ya wapiganaji shupavu wa Hizbullah askari wa Kizayuni ambao awali walikataa mpango wa kusitisha vita walilazimika kuukubali mpango huo na kurudi nyuma bila ya mafanikio yoyote.