Jumamosi, 15 Agosti, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 25 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1441 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 15 Agosti 2020 Miladia.
Tarehe 25 Dhulhija inasadifiana na siku ya kuteremshwa Suratu Dahr ambayo inawahusu Imam Ali bin Abi Twalib, mkewe Bibi Fatimatu Zahra na watoto wao Hassan na Hussein (as). Baada ya watukufu hao kuweka nadhiri ya kufunga swaumu siku tatu kwa ajili ya kukidhiwa haja zao na kuanza kutekeleza nadhiri hiyo, katika siku zote tatu za swaumu masikini, yatima na fakiri walikwenda nyumbani kwa Imam Ali (as) na kuomba chakula. Watukufu hao walitoa chakula chao kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya futari na kuwapa wahitaji hao kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu. Hali hiyo iliendelea kwa siku tatu za kutimiza nadhiri ya swaumu na wakati huo ndipo iliporetemshwa Suratu Dahr ikipongeza na kubakisha hai tukio hilo. ***

Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo mfereji wa Panama ulifunguliwa rasmi kufuatia kupita meli ya kwanza katika kanali hiyo. Ujenzi wa kanali hiyo ulianzishwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye serikali ya Marekani ilinunua kampuni ya Ufaransa iliyokuwa ikijenga mfereji huo na kukamilisha ujenzi wake. Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.***

Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita India ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza, baada ya miaka mingi ya mapambano ya kupigania uhuru. India ina historia kongwe na watawala mbalimbali wa ndani na nje wamewahi kutawala nchini humo. Mapambano ya wananchi wa India dhidi ya mkoloni Muingereza yalipamba moto zaidi baada ya kuasisiwa Chama cha Congress ya Kitaifa na kujiunga na chama hicho Mahatma Gandhi. ***
Miaka 72 iliyopita katika siku kakma ya leo, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea. Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini. ***
Miaka 67 iliyopita katika siku kama ya leo, Muhammad Reza Pahlavi, mfalme wa mwisho wa Iran alikimbilia Italia akiwa pamoja na mkewe. Kabla ya kuikimbia iran, Muhammad Reza Pahlavi alitia saini hukumu ya kuuzuliwa Wzairi Mkkuu Muhammad Musaddiq, na likimbia Italia baada ya kutambua kuwa, Waziri Mkuu huyo ana mpango wa kumpindua. ***
Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola. Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola. ***
Na miaka 15 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Agosti 2005 Miladia, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967, baada ya kutokea vita vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel. ***