Aug 15, 2020 22:07 UTC
  • Jumapili, 16 Agosti, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 26 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1441 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 16 Agosti 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 882 iliyopita alizaliwa huko katikati mwa Iraq Abul-Fadhail Amedi fakihi na mwanafasihi mahiri wa Kiislamu. Baada ya kusoma elimu za fiqhi, Usul Fiqhi, fasihi na hisabati katika mji wa Baghdad aliondokea kuwa mahiri katika elimu hizo. Abul Fadhail Amedi alikuwa na mashairi yenye kubeba maana kubwa. Amedi aliaga dunia akiwa katika eneo alilozaliwa akiwa na umri wa miaka 49. ***

Abul-Fadhail Amedi

 

Katika siku kama ya leo miaka 132 iliyopita,  alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu. Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence, alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu, ambapo sanjari na kujifunza lugha ya Kiarabu, alifahamu pia tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala, ili yaweze kujitenga mbali na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza. Aidha Thomas Edward Lawrence alikuwa na nafasi pi aya kuuingiza madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudia, suala ambalo lilipelekea kupata umashuhuri mkubwa nchini Saudia. ***

nchi

 

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa. Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterrania kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania. Lakini mwaka 1878, utawala wa  Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza. ***

Bendera ya Cyprus 

 

Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, kundi la kwanza mateka wa Kiirani waliokuwa wakishikiliwa katika magereza ya kutisha za Saddam Hussein liliwasili katika ardhi ya Iran. Kuachiwa huru mateka hao ilikuwa hatua muhimu ya kutekelezwa azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kati ya Iran na Iraq. Saddam Hussein ambaye wakati huo alikuwa chini ya mashinikizo kutokana na kuivamia Kuwait alikubali kuwaachia huru mateka hao wa Iran na kurejea katika mipaka inayokubalika kimataifa ya nchi mbili baada ya kukubali mkataba wa mpaka wa Algeria. ***

Mareka wa kiirani baada ya kuwasili katikka ardhi ya Iran 

 

Na miaka 17 iliyopita, inayosadifiana na 16 Agosti 2003, alifariki dunia dikteta wa zamani wa Uganda, Idi Amin Dada akiwa uhamishoni nchini Saudi Arabia. Idi Amin alilazwa katika hospitali ya Mfalme Feisal mjini Jeddah kwa wiki kadhaa kabla ya mauti kumkuta katika siku kama ya leo. Idi Amin aliingia madarakani mwaka 1971, baada ya kumpindua Milton Obote, na alibaki madarakani hadi mwaka 1979, pale alipoondoshwa madarakani na majeshi ya Tanzania. Idi Amin ambaye aliwahi kuwa bingwa wa masumbwi katika uzito wa juu nchini Uganda, aliwahi pia kuwa mkuu wa majeshi ya Uganda mwaka 1966, chini ya Rais Obote. Baada ya majeshi ya Uganda kupata kipigo mbele ya majeshi ya Tanzania, Amin alilazimika kuikimbia nchi hiyo na kukimbilia Libya, kisha Iraq na hatimaye Saudi Arabia. ***

Idi Amin Dada