Jumanne tarehe 18 Agosti 2020
Leo ni Jumanne tarehe 28 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 18 mwaka 2020
Tarehe 28 Dhulhija siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita, yaani miaka miwili baada ya harakati na mapambano ya mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) katika ardhi ya Karbala hapo mwaka 61 Hijria, kulijiri tukio la Harrah. Mwaka huo watu wa mji mtukufu wa Madina waliokuwa wamechoshwa na dhulma na ukatili wa mtawala Yazid bin Muawiya, walimfukuza gavana wake mjini humo Marwan bin Hakam. Baada ya tukio hilo Yazid alituma jeshi likiongozwa na mtumishi wake mmwaga damu na mtenda dhulma Muslim bin Uqbah katika mji mtakatifu wa Madina na kuliamuru kufanya mauaji makubwa mjini humo na kupora mali. Mauaji kama hayo hayakuwahi kushuhudiwa katika historia ya zama za awali za Uislamu na wanahistoria wamesema kuwa Waislamu zaidi ya elfu kumi wakiwemo maswahaba wa Mtume, waliuawa katika shambulizi hilo. Vitabu vya historia pia vinasema utawala wa Yazid bin Muawiya ulihalalisha mji wa Madina kwa askari wake kwa muda wa siku tatu na kwamba wasichana na wanawake wa maswahaba walinajisiwa katika tukio hilo.

Siku kama ya leo miaka 1367 iliyopita, vilitokea vita vya Ajnadeen katika eneo la Ajnadeen huko Palestina kati ya Waislamu na Warumi. Katika vita hivyo ambavyo havikuwa na mlingano hasa kwa kuzingatia kuwa, askari wa Kirumi walikuwa wengi mara kadhaa kuliko Waislamu, jeshi la Waislamu liliibuka na ushindi mkubwa kutokana na wapiganaji wake kuwa na irada na imani thabiti. Baada ya Warumi kushindwa vibaya na Waislamu waliamua kurejea nyuma hadi katika mpaka wa Palestina na Syria sambamba na kupoteza maeneo mengi yaliyokuwa chini ya udhibiti wao.
Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, alifariki dunia Hadi Sabzavari au Hajj Mulla Hadi Sabzavari, mmoja wa maulama na wanafalsafa wakubwa wa karne ya 13 Hijiria. Mulla Hadi Sabzavari alizaliwa mwaka 1212 Hijiria ambapo umri wake ulijaa baraka, huku mwishoni mwa maisha yake akijawa na izza ya nafsi, zuhdi na ucha-Mungu. Athari za Mulla Hadi Sabzavari zinaonyesha kwamba, alimu huyo mkubwa wa Waislamu mbali na kwamba alikuwa mmoja wa wanafalsafa wakubwa, pia alitabahari katika uwanja wa elimu ya sheria za Kiislamu (fiq'hi), tafsiri ya Qur'an, mantiki, hisabati, fasihi na elimu ya tiba. Aidha Mulla Hadi Sabzavari mbali na kufikia daraja za juu za kielimu, alikuwa pia malenga. Katika uwanja huo, alikuwa akisoma mashairi ambayo yalifungamana na nukta za kifalsafa na elimu ya irfani. Allamah Iqbal Lahore, malenga na mwanafalsafa mkubwa wa Pakistan, alimzungumzia Mulla Hadi Sabzavari kuwa, mwanafikra mkubwa wa Iran ambaye falsafa yake alijifunza kupitia dini ya Kiislamu. Miongoni mwa athari za mwazuoni huyo ni pamoja na 'Mandhumah' katika uwanja wa elimu ya mantiki, 'Asraarul-Hikami' na 'al-Jabru wal-Ikhtiyaar.'
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, kulifanyika mapinduzi ya Kimarekani dhidi ya serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq nchini Iran na baadaye kidogo Shah Reza Pahlavi akatwaa tena madaraka ya nchi. Mapinduzi hayo ambayo yalipangwa na shirika la ujasusi la Marekani CIA kwa ushirikiano wa Uingereza, yaliiondoa madarakani serikali ya Musaddiq kupitia njia ya kuzusha hitilafu na mifarakano kati ya wanaharakati wa kisiasa na wananchi na kueneza anga ya ghasia na machafuko nchini. Vilevile yalimrejesha Iran Shah Pahlavi ambaye siku tatu kabla alikuwa amekimbilia nchini Italia. Kabla ya tukio hilo la kusikitisha, wananchi Waislamu wa Iran walikuwa wamefanikiwa kukata mkono wa Uingereza hapa nchini na kutaifisha sekta ya mafuta iliyokuwa ikidhibitiwa na wakoloni hao.

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 28 Mordad 1357, Hijria Shamsia, vibaraka wa utawala wa Shah walifanya maafa ya kutisha ya kuchoma moto jumba la sinema la Rex katika mji wa Abadan kusini mwa Iran. Katika tukio hilo la kinyama la kuchomwa moto Jumba la Sinema la Rex, watu wasio na hatia 377 wakiwemo watoto na wanawake walipoteza maisha yao. Jinai hiyo ilifanywa na maajenti shirika hatari la ujasusi la Savak na vibaraka wa utawala wa Shah. Watu karibu 700 waliokuwa wakitazama sinema katika jumba hilo walifungiwa ndani baada ya moto kuzuka na mamia miongoni mwao wakateketea. Tukio hilo lilizusha hasira kubwa baina ya wananchi. Utawala wa Shah ulifanya maafa hayo na kisha kuwatuhumu wanamapinduzi kuwa ndio waliotekeleza shambulizi hilo la kutisha kwa shabaha ya kuchafua sura la harakati za Mapinduzi ya Kiislamu mbele ya wananchi. Hata hivyo njama hizo za Shah zilifeli.
Na katika siku kama ya leo miaka 36 iliyopita alifariki dunia Dakta Azar Andami mwanafizikia, mhakiki na mtaalamu mahiri wa bakteria wa Kiirani. Alizaliowa katika eneo la Rasht katika mkoa wa Gilan huko kaskazini mwa Iran. Alikuwa na kipaji kikubwa cha masomo. Azar Andami alihitimu masomo ya PhD katika Chuo Kikuu cha Tehran.