Aug 21, 2020 22:29 UTC
  • Jumamosi, 22 Agosti, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe Pili Mfunguo Nne Muharram 1442 Hijria mwafaka na tarehe 22 Agosti 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita yaani tarehe Pili Muharram mwaka 61 Hijria Imam Hussein (AS) mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) akiwa pamoja na familia yake waliwasili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo. Miezi kadhaa kabla ya hapo, Imam Hussein AS aliondoka katika mji mtakatifu wa Madina na kuelekea Makka akilalamikia utawala wa kimabavu wa Yazid bin Muawiya na baadaye akaelekea katika mji wa Kufa huko Iraq. Japokuwa watu wa Kufa mwanzoni waliunga mkono mapambano ya Imam Hussein na kumwalika katika mji huo, lakini waliacha kumuunga mkono mjukuu huyo wa Mtume kutokana na hofu na vitisho vya utawala wa Yazid bin Muawiya. Jeshi la Yazidi mlaaniwa liliuzuia msafara wa mjukuu huyo wa Mtume (saw) kuingia katika mji wa Kufa na kuuzingira katika jangwa na Karbala.***

Harakati ya Imam Hussein (as)

 

Katika siku kama ya leo miaka 393 iliyopita vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle. ***

Vita vya Rochelle

 

Miaka 322 iliyopita katika siku kama ya leo, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Sharel XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Sharel XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.  Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda. ***

Sharel XII, mfalme kijana wa Sweden

 

Siku kama ya leo miaka 160 iliyopita Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine. ***

Paul Gottlieb Nipkow

 

Miaka 156 iliyopita katika siku kama hiii ya leo, mkataba wa kihistoria wa Geneva ulitiwa saini baina ya nchi kadhaa za Ulaya, Asia na Amerika. Lengo la mkataba huo lilikuwa ni kuwasaidia majeruhi katika medani za vita.  Kwa mujibu wa mkataba huo, timu za madaktari, watoaji misaada na zana zao zinapaswa kutoegemea upande wowote na zisishambuliwe bali zibakie katika amani wakati wa vita. Mbunifu wa mkataba huo alikuwa Henry Dunant raia wa Uswisi. ***

Henry Dunant

 

Na siku hii ya tarehe Mosi Shahrivar kwa kalenda ya mwaka wa Hijria Shamsia ni siku ya kumuenzi mwanafalsafa, tabibu na msomi mkubwa wa Kiislamu na Kiirani Hussein bin Abdullah maarufu kwa jina la Ibn Sina. Ibn Sina alihifadhi Qur'ani yote alipokuwa na umri wa miaka 10. alijifunza utabibu baada ya kupata elimu za mantiki, hisabati, nujumu, falsafa pamoja na elimu nyinginezo. Alianza kuandika vitabu akiwa na umri wa miaka 21 na miongoni mwa vitabu vyake maarufu ni Qanun, Shifaa na al Isharaat. Siku hii huenziwa hapa nchini Iran kama Siku ya Daktari. ***

Abu Ali Sina