Jumapili tarehe 23 Agosti 2020
Leo ni Jumapili tarehe 3 Mfunguo Nne Muharram mwaka 1442 Hijria unayosadifiana na Agosti 23 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1435 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW aliwatumia barua wafalme wa tawala mbalimbali duniani na kwa hatua hiyo akawa ameanza rasmi kuwalingania watu Uislamu kimataifa. Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume Muhammad SAW alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa duniani bila wasi wasi. Wanahistoria wanasema kuwa, Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine makubwa katika zama hizo ambapo kila mmoja kati ya watawala hao alionesha radimalia yake. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilionesha wazi kuwa dini ya Kiislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.
Miaka 1381 iliyopita yaani tarehe 3 Muharram mwaka 61 Hijria, jeshi la Omar bin Saad liliwasili katika ardhi ya Karbala. Baada ya Hurr bin Yazid kumzingira Imam Hussein AS na maswahaba zake katika ardhi ya Karbala na kuwazuia wasisonge mbele, Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa kibaraka wa Yazid huko Kufa akakabidhi jukumu la ukamanda wa jeshi la Yazid kwa Omar bin Saad.

Siku kama ya leo, miaka 76 iliyopia, mji wa Paris ulikombolewa kutoka kwenye uvamizi wa Ujerumani. Miezi 15 baada ya kushtadi moto wa Vita vya Pili vya Dunia na katika kuendeleza njama zake za kutaka kujitanua, dikteta Adolph Hitler aliyaamuru majeshi ya nchi hiyo kuushambulia mji wa Paris kwa lengo la kutaka kuudhibiti mji huo. Tarehe tano Juni mwaka 1940, Hitler alitoa amri ya kuharibiwa kikamilifu muundo wa majeshi ya Ufaransa na siku tatu baadaye yaani tarehe nane Juni mwaka 1940, vikosi vya Wanazi vilikishinda kikosi cha ulinzi cha Ufaransa katika eneo la kaskazini mashariki mwa taifa hilo, na hivyo kutoa mwanya kwa jeshi la Ujerumani kuingia nchini Ufaransa.
Miaka 42 iliyopita katika siku kama hii ya leo Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Andarzgu aliuawa shahidi na vibaraka wa utawala wa Shah. Shahidi Andarzgu alianza harakati za mapambano akiwa na umri wa miaka 19 na kufahamiana kwa karibu shahidi Nawab Safawi, kiongozi wa kundi la Waislamu wanamapinduzi. Baada ya hapo Shahid Andarzgu alijiunga na harakati ya Muutalifeye Eslami na alikuwa miongoni mwa waliotekeleza mauaji ya kimapinduzi dhidi ya Waziri Mkuu wa wakati huo wa Shah, Hussein Ali Mansour. Shahid Andarzgu aliendesha mapambano ya siri dhidi ya utawala wa Shah kwa kipindi cha miaka 13 na hatimaye aliawa shahidi shahidi na vibaraka wa Shah katika siku kama hii ya leo katika mapambano ya silaha.
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 23 Agosti 2003, alifariki dunia Michael Kijana Wamalwa, Makamu wa Rais wa Kenya. Wamalwa alizaliwa 25 Novemba 1944 katika kijiji cha Sosio karibu na Kimilili, wilayani Bungoma. Michael Kijana Wamalwa alikuwa mtoto wa mwanasiasa na mbunge machachari William Wamalwa. Mwaka 2002, Wamalwa akiwa pamoja na wanasiasa wengine mashuhuri nchini Kenya, wakiongozwa na Mwai Kibaki wa chama cha National Rainbow Coalition NARC, walifanikiwa kuung'oa madarakani utawala wa chama cha KANU uliotawala nchi hiyo kwa zaidi ya miongo minne. Kijana Wamalwa alizikwa kwenye shamba lake lililoko Kitale.