Aug 26, 2020 03:47 UTC
  • Jumatano tarehe 26 Agosti mwaka 2020

Jumatano tarehe 6 Muharram 1442 Hijria sawa na tarehe 26 Agosti mwaka 2020.

Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1381 iliyopita mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) Imam Hussein (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa wa mjini Madina. Barua hiyo ilisema: "Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nasi atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga nasi hatapata ushindi." Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba Imam Hussein alikuwa akijua kuwa atauawa shahidi yeye na masahaba zake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala kwamba wote watauawa shahidi na kwamba mtu mwenye malengo mengine bora arejee Madina.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita, Habib bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.” Imam Hussein alimruhusu Habib bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.” 

Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kujua kwamba jeshi la Omar Bin Sa’ad lilitambua nia yao; hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwata illa Billah.”

Kaburti la Habib bin Madhahir

Siku kama ya leo miaka 1036 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu. Aalim huyo pia alifahamika kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za Fiqhi, tafsiri ya Qur'ani Tukufu na elimu nyingine ya Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur'ani, historia na fasihii ya Kiarabu. Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as).

Kaburi la Sayyid Radhi

Siku kama ya leo miaka 674 iliyopita mzinga mkubwa ulitumika kwa mara ya kwanza katika historia. Siku hiyo jeshi la Uingereza lilitumia silaha ya mzinga dhidi ya askari wa Ufaransa. Katika vita hivyo Mfalme Philip wa Sita wa Ufaransa alishindwa vibaya na jeshi la Uingereza licha ya kwamba jeshi la Ufaransa lililokuwa limekaribia kupata ushindi, lilikuwa na idadi kubwa ya askari na wapiganaji. Ushindi wa jeshi la Uingereza katika vita hivyo ulitokana na utumiaji wa silaha ya mzinga.

Mfano wa mizinga ya zamani

Siku kama ya leo miaka 124 iliyopita askari wa utawala wa Kiothmani walianza kufanya mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia. Waturuki wa Kiothmani walifanya mauaji hayo kwa kisingizio kwamba Waarmenia waliwasaidia Wagiriki katika ghasia zilizofanyika dhidi ya utawala wa Kiothamani. Maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wadogo wa Kiarmenia waliuawa kwa umati katika mauaji hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha siku tano.

Mauaji ya umati dhidi ya Waarmenia

Tarehe tano Shahrivar miaka 42 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, mwanzo wa kalenda ya Iran ulirejeshwa tena katika mwaka wa Hijria Shamsia kutoka mwanzo wa tarehe ya Kifalme. Katika miaka ya kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu utawala wa kidikteta wa Pahlavi ambao ulitambua mafundisho ya Uislamu kuwa ni kinyume na maslahi yake, ulikuwa ukifanya njama za kukabiliana na Uislamu kwa kutumia utajiri na turathi ya kihistoria ya Iran. Katika mkondo huo bunge la kimaonyesho la utawala wa Kipahlavi lilipasisha sheria iliyobadilisha mwanzo wa kalenda ya Iran kutoka mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) na kuifanya kuwa tarehe ya kuvikwa taji la Mfalme Kurosh wa silsila ya Khahamaneshi. Hatua hiyo lilikabiliwa na hasira na malalamiko makubwa ya Imam Ruhullah Khomeini na wananchi Waislamu wa Iran. Kubadilishwa huko kwa mwaka wa Hijria na kufuata mwaka wa Kifalme nchini hakukudumu kwa zaidi ya kipindi cha miaka miwili na nusu na utawala wa Shah uliokuwa ukikabiliwa na harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ulilazimika kutambua tena mwaka wa Hijra ya Mtume (saw) kutoka Makka kwenda Madina kuwa ndiyo mwanzo wa kalenda nchini Iran. 

Siku hii ya leo tarehe 5 Shahrivar ni siku ya kumuenzi Muhammad bin Zakaria Razi, msomi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu. Ibn Zakaria Razi alizaliwa mwaka 251 hijria katika mji wa Rei nchini Iran na alianza kujifunza kemia na fizikia akiwa bado kijana. Tabibu na mkemia Muhammad bin Zakaria Razi alijifunza pia elimu nyingine kama vile tiba, mantiki na falsafa. Baadaye Razi alifanikiwa kutengeneza asidi ya sulfuriki kwa kustafidi na mada asilia. Msomi huyo wa Kiislamu Muirani alikuwa shakhsia wa kwanza kuvumbua alkoholi. Muhammad bin Zakaria Razi ameandika vitabu 56 vya tiba, 33 vya sayansi ya asili, 17 vya falsafa, 14 vya teolojia, 22 vya kemia na makumi ya vitabu vingine katika nyanja mbalimbali. Msomi huyo wa Kiislamu alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 60 na alizikwa katika mji wa Rei ambao hii leo uko kusini mwa Tehran.

Muhammad bin Zakaria Razi

Miaka 30 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo alifariki dunia Ali Akbar Kaveh, mwalimu mkubwa wa sanaa ya kaligrafia ya hati za Kifarsi. Mtaalamu huyu alizaliwa mwaka 1271 Hijria mjini Shiraz, moja ya miji ya kusini mwa Iran na kuanza kujihusisha na masuala ya karigrafia. Baada ya hapo Ali Akbar Kaveh alipata kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo kama vile Mirza Twahir Katib, Homayun Hamedani na Imad Al Katib Seifi Qazvini na hatimaye akawa hodari mkubwa katika sanaa ya kaligrafia.

Ali Akbar Kaveh