Aug 31, 2020 21:54 UTC
  • Jumanne, Septemba 01, 2020

Leo ni Jumanne tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 1442 Hijria sawa na Tarehe Mosi Septemba mwaka 2020 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Muharram mwaka 61 Hijria msafara wa mateka wa Karbala uliokuwa na wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Bibi Zainab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as) pamoja na Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as). Imam Sajjad na Bibi Zaynab (as) walitekeleza majukumu yao kwa kufikisha ujumbe wa Imam Hussein kwa jamii ya Waislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtukufu wa mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein AS ilizikwa ikiwa ni siku mbili baada ya kuuawa shahidi na kuachwa jangwani. Mashahidi wa Karbala walizikwa na watu wa kabila la Bani Asad. Mwili wa Imam Hussein na mashahidi wote wa Karbala ilibakia kwa siku mbili bila ya kuzikwa kwani hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzika miili hiyo kutokana na hofu ya utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo wanawake wa kabila la Bani Asad waliwahamasisha wanaume wao kuzika miili hiyo mitakatifu ya wajukuu wa Mtume na masahaba wa Imam Hussein (as).

Makaburi ya Mashahidi wa Karbala

Siku kama ya leo miaka 1347 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.

Siku kama ya leo miaka 846 iliyopita, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kuitundika saa juu ya mnara huo, hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda katika masafa ya karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la"Mnara Uliopinda wa Pisa." Hadi kufikia sasa mnara huo umeweza kufanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali.

Mnara wa Pisa

Katika siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioambatana na uharibifu mkubwa na kuua idadi kubwa ya watu, ulitokea nchini Japan. Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 8.3 kwa kipimo cha Rishta iliua watu zaidi ya laki moja na 40 elfu. Mtetemeko huo uliyakumba hata baadhi ya maeneo ya miji ya Tokyo na Yokohama. Mbali na hasara kubwa zilizosababishwa na mtetemeko huo, idadi kubwa ya Wajapani pia walikosa makazi yao na nyumba nyingi ziliteketea kwa moto.

Siku kama leo miaka 59 iliyopita, yaani sawa na tarehe Mosi Septemba mwaka 1961, ulifanyika mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya Isiyofungamana na Upande Wowote NAM huko Belgrade mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani kwa kuhudhuriwa na viongozi wa nchi 25 duniani. Jumuiya ya NAM iliasisiwa lengo kuu likiwa ni kuziunga mkono nchi za ulimwengu wa tatu mkabala na kambi za Mashariki na Magharibi. Masharti makuu ya kujiunga na jumuiya hiyo, ni kutokuwa mwanachama rasmi katika muungano unaofungamana na madola makubwa ya Mashariki na Magharibi.

Na miaka 51 iliyopita katika siku kama ya leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomfikisha madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa Mfalme Idris wa Kwanza. Wakati mfalme Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi ya kijeshi na kumvua madaraka mfalme huyo sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Hata hivyo katika miaka ya kukaribia kupinduliwa na kuuliwa, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi. Muammar Gaddafi aliondolewa madarakani na kuuawa kufuatia mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011.

Muammar Gaddafi