Jumanne tarehe 29 Septemba 2020
Leo ni Jumanne tarehe 11 Safar 1442 Hijria sawa na tarehe 29 Septemba 2020.
Siku kama ya leo miaka 941 iliyopita Jaafar bin Hussein bin Ahmad mashuhuri kwa jina la Siraj, alifariki dunia katika mji wa Sur (Tyre) kusini mwa Lebanon. Jaafar bin Hussein bin Ahmad alikuwa miongoni mwa mafaqihi, wapokeaji hadithi na maqarii wakubwa wa karne ya sita. Siraj alizaliwa mwaka 419 Hijria na kupata elimu mbalimbali kama hadithi, qiraa na fasihi ya lugha. Aidha alisafiri katika nchi mbalimbali kama Misri na eneo la Sham kwa ajili ya kuzidisha elimu na maarifa. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu mbalimbali na miongoni mwake ni kile alichokipa jina la Nidhamul Manasik.
Miaka 119 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa mwanafizikia mashuhuri wa Italia Enrico Fermi katika mji wa Roma. Baada ya kukamilisha masomo ya Chuo Kikuu aliweza kuvumbua kanuni ya Mwendo wa Molekuli ya Gesi. Fermi alifanya uchunguzi kuhusu mabadiliko ya atomu na akafanikiwa kutengeneza betri ya atomu kwa kuipasua na kutoa nje nishati yake. Mwanafizikia huyo wa Italia alifariki dunia mwaka 1954.
Siku kama ya leo miaka 118 iliyopita, alifariki dunia mwandishi wa Kifaransa, Emile Zola. Zola alizaliwa mjini Paris mwaka 1840. Emile Zola alindika vitabu vingi katika elimu tofauti. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwandishi huyo wa Ufaransa ni "Therese Raquin” "Nana", "The Belly of Paris na "Germinal."
Na siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, ulifanyika uchaguzi huru wa kwanza nchini Angola. Katika uchaguzi huo chama cha MPLA kilichokuwa kikiongoza nchi hiyo tangu mwaka 1976 kilipata ushindi na kiongozi wake José Eduardo dos Santos akachaguliwa tena kuingoza nchi hiyo. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Angola ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mreno hapo mwaka 1975. Vita vya ndani nchini humo vilihitimishwa rasmi mwaka 2002 baada ya kuuawa kiongozi wa chama cha upinzani cha UNITA Jonas Savimbi aliyekuwa akiungwa mkono na Marekani.