Jumanne tarehe 6 Oktoba 2020
Leo ni Jumanne tarehe 18 Safar 1442 Hijria sawa na Oktoba 6 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1405 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, aliuawa shahidi Uways al Qarani, mmoja kati ya wafuasi waaminifu wa Mtume Mtukufu SAW na Imam Ali bin Abi Twalib (as) katika vita vya Siffin. Uways Qarani aliishi katika eneo la Qaran lililoko Yemen na alikuwa mchamungu mkubwa. Licha ya kuwa na mapenzi makubwa kwa Mtume Mtukufu SAW, Uways Qarani hakubahatika kumuona mtukufu huyo, kwa kuwa kipindi hicho alikuwa akimuuguza mama yake aliyekuwa mgonjwa. Baada ya Mtume Mtukufu SAW kufariki dunia, Uways Qarani alikuwa miongoni mwa wafuasi wa karibu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as). Hata hivyo Mtume Muhammad (saw) alimzungumzia Uways na kumsifu licha ya kwamba hakuwahi kuonana naye. Shakhsia huyo akiwa pamoja na wapiganaji wengine katika jeshi la Imam Ali (as), alishiriki kikamilifu kwenye vita vya Siffin kati ya jeshi la Imam Ali na lile la Muawiya bin Abi Sufiyan na akauawa shahidi katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 136 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Mir Hamid Hussein Mussawi Hindi. Alizaliwa mwaka 1246 Hijria nchini India na kupata elimu katika taaluma za fiqhi, Hadithi, teolojia na elimu nyingine za Kiislamu. Miir Hamid Hussein alitumia sehemu kubwa ya umri wake kufunza elimu za kidini na kuandika vitabu. Kitabu muhimu zaidi cha Allamah Miir Hussein Hindi ni A'baqaatul Anwar. Vitabu vingine vya msomi huyo wa Kiislamu ni pamoja na Asfarul Anwar na Sham'ul Majalis.
Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, alizaliwa mjini Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran malenga na mchoraji wa Kiirani wa zama hizi Sohrab Sepehri. Mwaka 1330 Hijiria Sepehri alisambaza majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akapata kusambaza tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana fani ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi viitwavyo "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1359 Hijiria na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita sawa na tarehe 6 Oktoba mwaka 1973, vilianza vita vya nne kati ya Waarabu na utawala ghasibu wa Kizayuni. Katika siku hiyo jeshi la Misri lilivishambulia vikosi vya utawala huo haramu katika oparesheni ya kushtukiza katika upande wa pili wa Mfereji wa Suez. Baada ya kuvunja mstari imara wa ulinzi wa Barlow vikosi hivyo vikafanikiwa kuingia katika jangwa la Sinai. Katika vita hivyo vikosi vya Misri na Syria viliyatia hasara kubwa majeshi ya utawala wa Israel na idadi kadhaa ya ndege za kivita za Wazayuni kusambaratishwa. Hata hivyo kutokana na hatua ya Marekani ya kuupatia silaha za kisasa utawala huo wa Kizayuni Waarabu walipoteza baadhi ya ushindi waliokuwa wameupata katika vita hivyo.
Na miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani mwaka 1981 maafisa kadhaa wa kundi la Kiislamu la "Al-Jihad" walishambulia na kumuua rais wa wakati huo wa Misri, Muhammad Anwar Sadat. Rais huyo aliuawa kwa sababu ya kutia saini makubaliano ya udhalilishaji ya Camp David mnamo mwaka 1978 na utawala ghasibu wa Kizayuni sambamba na kuutambua rasmi utawala huo haramu. Kufuatia hatua hiyo rais huyo alihesabiwa kuwa msaliti wa malengo matukufu ya Waislamu na Waarabu. Kwa upande mwingine hatua hiyo ilipelekea kutengwa Misri na nchi za Kiislamu. Ni kwa sababu hiyo ndipo makundi ya Kiislamu na wanamapambano wa Misri wakaamua kumuua Sadat, ambaye alionekana kuwa msaliti mkubwa kwa kuutambua rasmi utawala huo ghasibu unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kibla cha kwanza cha Waislamu. Aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa Khalid Islambuli, mmoja wa maafisa wa jeshi la Misri wakati huo.