Jumatano tarehe 7 Oktoba mwaka 2020
Leo ni Jumatano tarehe 19 Safar 1442 Hijria sawa na Oktoba 7 mwaka 2020.
siku kama ya leo miaka 1271 iliyopita yaani tarehe 19 Safar mwaka 171 Hijria alizaliwa Abu Ma'ashar Balkhi mmoja kati ya wanajimu na wasomi wakubwa wa elimu ya nujumu wa Kiirani. Alielekea Baghdad na kuanza kusoma elimu ya nujumu. Abu Ma'ashar Balkhi alitumia vyanzo vya lugha za Kiarabu, Kihindi, Kigiriki na Kisiriani kwa ajili ya kupata elimu ya nujumu na kuwa miongoni mwa wanajimu wakubwa katika zama zake. Kazi zake katika taaluma hiyo zilitumiwa kwa karne kadhaa katika ulimwengu wa Kiislamu na Kimagharibi hata baada ya kufariki kwake dunia. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo wa Kiislamu ni al-Madkhal al-Kabir na al-Mawalidul al Saghirah.

Miaka 92 iliyopita katika siku kama ya leo muwafaka na tarehe 16 Mehr mwaka 1307 Hijiria Shamsia kufuatia upinzani wa mara kwa mara wa Sayyid Hassan Mudarres dhidi ya utawala wa kidikteta wa Ridhakhan Pahlawi, mtawala huyo aliviamuuru vikosi vyake kuvamia nyumba ya Ayatullah Muddares na kumpiga na kisha kumjeruhi. Baadaye mwanazuoni huyo alihamishiwa nje ya mji wa Tehran. Mwishowe Ayatullah Mudarres alipelekwa uhamishoni katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran na kuuawa shahidi na askari wa Ridhakhan mwaka 1316 Hijiria Shamsia akiwa katika mji huo.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita utawala wa Baath nchini Iraq ulishambulia mji wa Soumar nchini Iran kwa silaha za kemikali. Raia wengi waliuawa shahidi katika mahambulizi hayo ya silaha za kemikali. Katika kipindi chote cha miaka 8 ya vita vya kutwishwa, utawala wa Saddam Hussein ulitumia silaha za kemikali mara kadhaa dhidi ya maeneo ya raia na vituo vya kijeshi. Mashambulizi hayo yaliua shahidi na kujeruhhi raia na wanajeshi karibu laki moja wa Iran. Baadhi ya majeruhi wa silaha hizo hadi sasa bado wanaishi kwa mashaka na taabu sana kutokana na athari mbaya ya gesi ya kemikali ya silaha zilizotuumiwa na Saddam Hussein dhidi ya maeneo mbalimbali ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 19 iliyopita yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington walihusika na tukio la Septemba 11 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo mazito ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi. Hata hivyo pamoja na Marekani kusaidiwa na muungano wa vikosi vya kaskazini mwa Afghanistan na kufanikiwa kuuangusha utawala wa Taliban, hadi leo haijaweza kuwatia nguvuni baadhi ya viongozi wa kundi hilo la Taliban.