Alkhamisi, Oktoba 8, 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Mfunguo Tano Safar mwaka 1442 Hijria sawa na Oktoba 8 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu, ilifanyika majlisi ya kwanza ya siku ya Arubaini tangu kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW) Imam Hussein bin Ali (AS) na watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume ambao waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria. Majlisi ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka baada ya kupita siku Arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume na masahaba zake watiifu ambao walijisabilia roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika ardhi ya Karbala. Katika siku hii ya Arubaini pia msafara wa mateka wa Ahlul-Baiti wa Mtume uliokuwa umepelekwa Sham kwa mtawala dhalimu Yazid bin Muawiyah uliwasili Karbala ukiwa na kichwa cha Imam Hussein na kukutana hapo na Sahaba wa Mtume, Jabir bin Abdillah al Ansari na wafuasi wengine wa Imam waliokwenda hapo kufanya ziara. Siku hiyo kichwa cha Imam Hussein kilizikwa pamoja na mwili wake.

Siku kama ya leo miaka 127 iliyopita, alizaliwa Ayatullah al-Udhma Mar’ashi Najafi mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu katika mji wa Najaf nchini Iraq. Baba yake ni Sayyid Shamsuddin Mahmoud Mar’ashi aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na mafaqihi wakubwa katika zama zake. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na ya Kiislamu huko Najaf, Mar’ashi Najafi alianza kuhudhuria darsa na masomo ya Usul kwa Agha Dhiyau Iraqi na Sheikh Ahmad Kashif al-Ghitaa. Ayatullah Mar’ashi Najafi alipata daraja ya juu ya elimu yya Ij’tihad akiwa na umri wa miaka 27.
Katika siku kama ya leo miaka 109 iliyopita, vita vya Balkan vilianza kwa ushiriki wa Bulgaria, Serbia na Ugiriki dhidi ya Utawala wa Othmania. Ufalme wa Othmania kwa miaka kadhaa mtawalia ulikuwa umefanikiwa kuyafanya maeneo mengi ya magharibi mwa Asia, kaskazini mwa Afrika na mashariki mwa Ulaya kuwa chini ya udhibiti wake na hivyo ukawa umetanua utawala wake. Vuguvugu la kulitaka kujitenga nchi zilizokuwa chini ya utawala huo lilikuwa likipelekea kutokea vurugu mara kwa mara na vita vya Balkan ni moja ya harakati hizo.
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita sawa na tarehe 8 Oktoba 1990, kwa mara nyingine tena utawala haramu wa Israel ulifanya jinai ya kinyama kwa kuwashambulia waumini wa Kipalestina waliokuwa wakiswali ndani ya Msikiti mtukufu wa al-Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wapalestina 20 waliuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa. Mauaji ya Wapalestina yaliyofanywa na utawala ghasibu wa Israel tena ndani ya Msikiti wa al-Aqsa, kwa mara nyingine tena yalilipua ghadhabu za fikra za walio wengi duniani dhidi ya utawala huo katili. Hata hivyo kama kawaida uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ulizuia kuchukuliwa hatua yoyote ya kivitendo dhidi ya utawala huo.
Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo cha rishta uliyakumba maeneo ya kaskazini mashariki mwa Pakistan. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa katika mji wa Muzaffarabad. Watu karibu 90,000 walipoteza maisha yao na wengine 3,300,000 kubaki bila makazi.
