Oct 19, 2020 23:07 UTC
  • Jumanne tarehe 20 Oktoba 2020

Leo ni Jumanne tarehe Tatu Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 1442 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Oktoba mwaka 2020.

Tarehe 3 Rabiul Awwal miaka 1001 iliyopita alifariki dunia mshairi na mwandishi mashuhuri wa Kiarabu Abul Alaa al Maarry. Alizaliwa mwaka 363 Hijria katika Syria ya sasa na baadaye alielekea Baghdad kwa ajili ya kukamilisha elimu ya juu. Licha ya kuwa kipofu tangu utotoni, lakini Abul Alaa alitokea kuwa mshairi mashuhuri na hodari wa zama zake.

Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri la "Risalatul Ghufran" na "al Aamali."

Abul Alaa al Maarry

Siku kama ya leo miaka 193 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean. Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita, yalishambulia meli za dola ya Othmania. Nchi hizo tatu za Ulaya zilifanikiwa kuziangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita.

Vita vya ghuba ya Navarone

Siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani. Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture" John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.

John Dewey

Miaka 68 iliyopita muwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya. Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza. Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo.

Mzee Jomo Kenyatta

Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita wafanyakazi wa sekta ya mafuta nchini Iran walianza mgomo wa nchi mzima katika harakati za kupinga utawala wa kidekta wa Shah. Mgomo huo ulipelekea kukatwa uuzaji nje bidhaa ya mafuta ya Iran na kumnyima Shah sehemu kubwa na muhimu zaidi la pato la utawala wake, na vilevile ulizidisha mashinikizo dhidi ya utawala huo. Mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya mafuta ya Iran pia ulipelekea kuongozeka bei ya bidhaa hiyo katika masoko ya kimataifa. Licha ya vitisho vya utawala kibaraka wa Shah mgomo huo ulioendelea hadi utawala huo ulipoondolewa madarakani.  

Mgomo wa wafanyakazi wa sekta ya mafuta Iran

Siku kama ya leo miaka 9 iliyopita, dikteta wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa. Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli. Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.

Muammar Gaddafi