Alkhamisi tarehe 22 Oktoba 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 5 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa Oktoba 22 mwaka 2020.
Tarehe 5 Mfunguo Sita miaka 174 iliyopita kilifunguliwa chuo kikuu cha kwanza nchini katika muundo na sura ya kisasa. Chuo hicho kilichojulikana kwa jina la 'Darul Funuun' kilianza kutoa mafunzo katika zama za ufalme wa Nasiruddin Shah Qajar kwa hima ya Amir Kabiir. Lengo la kuanzishwa chuo hicho lilikuwa kufunza sayansi mpya na kuiwezesha Iran kupata viwanda na teknolojia ya kisasa. Miongoni mwa taaluma zilizokuwa zikitolewa katika chuo hicho ni masuala ya tiba, upasuaji, utaalamu wa madini na utengenezaji dawa. Kuanzishwa chuo hicho kulifungua ukurasa mpya katika historia ya elimu nchini Iran.
Tarehe 22 Oktoba miaka 45 iliyopita aliaga dunia mwanahistoria mashuhuri wa Uingereza, Arnold Toynbee. Msomi huyo alizaliwa mwaka 1889. Alifundisha somo la historia ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha London. Arnold Toynbee ameandika vitabu vingi katika taaluma ya historia, na muhimu zaidi ni kile cha A Study of History kinachochunguza staarabu za kale za kihistoria.
Miaka 43 iliyopita katika siku kama hii ya leo, Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini, mtoto wa Imam Ruhullah Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa shahidi kufuatia njama ilizofanywa na askari usalama wa utawala wa Shah akiwa nyumbani kwake huko Najaf, moja kati ya miji mitukufu ya Iraq. Al Haj Mustafa Khomeini alizaliwa mwaka 1309 Hijria Shamsiya katika mji mtakatifu wa Qum na baadaye akajiunga na chuo cha elimu ya dini cha mji huo kwa ajili ya masomo ya juu baada ya kuhitimu elimu ya msingi. Alikuwa hodari mno na alifikia daraja ya juu ya kielimu ya Ijtihadi akiwa na umri wa miaka 27. Ayatullah Mustafa Khomeini alikuwa pamoja na baba yake Imam Khomeini katika kipindi chote cha mapambano dhidi ya utawala wa Shah.
Tarehe 22 Oktoba ni siku ya kitaifa ya Vatican, inayohesabiwa kuwa nchi ndogo zaidi duniani.
Vatican ina ukubwa wa chini ya nusu kilomita mraba, na jamii ya watu karibu elfu moja huko kusini mwa Ulaya. Nchi hiyo iko eneo la magharibi ndani ya mji mkuu wa Italia, Roma. Lugha rasmi ya Vatican ni Kitaliano. Wakazi wa Vatican ni wafuasi wa madhehebu ya Katoliki na wanatumia sarafu ya Yuro. Nchi hiyo ndogo ya Vatican inatawaliwa na serikali ya kidini ambayo inaongozwa na Papa wa Kanisa Katoliki. Vatican inatajwa kuwa kituo kikuu cha kupanga mikakati ya madhehebu ya Katoliki katika maeneo mbalimbali duniani. Nchi ya Vatican ilijitenga na Italia mwaka 1929 na tarehe 22 Oktoba ya kila mwaka ambayo kwa hakika ni siku ya kuchaguliwa Papa John Paul wa Pili hapo mwaka 1978, imetangazwa kuwa ni Siku ya Kitaifa ya Vatican.