Oct 26, 2020 02:37 UTC
  • Jumatatu tarehe 26 Oktoba 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 9 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na Oktoba 26 mwaka 2020.

Siku kama ya leo tarehe 9 Rabiul Awwal miaka 1182 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, baada ya kuuawa shahidi Imam Hassan Askari (AS) kilianza rasmi kipindi cha uongozi wa Imam wa Zama, Imam Mahdi (AF). Imam Mahdi ni mwana wa Imam Hassan Askari (AS) na miongoni mwa wajukuu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Imam Mahdi yuko ghaiba kwa amri ya Mwenyezi Mungu (SW) na hadi mwaka 328 Hijria alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi wake maalumu. Kipindi hicho kilipewa jina la "Ghaiba Ndogo". Baada ya hapo kilianza kipindi cha Ghaiba Kubwa ambapo Imam wa Zama hakuainisha mwakilishi makhsusi na mafakihi wenye ujuzi wa dini ya Kiislamu, wacha-Mungu na watambuzi wa masuala ya zama ndio wawakilishi wa mtukufu huyo katika Umma. Imam Mahdi (AF) atadhihiri tena kwa ajili ya kueneza haki na uadilifu.

Miaka 73 iliyopita katika siku kama hii ya leo eneo la kiistratejia la Jammu na Kashimir liliunganishwa na India baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza na Pakistan kujitenga na India. Ilipangwa kuwa, eneo la Jammu na Kashmir lenye wakazi wengi Waislamu litajiunga na Pakistan lakini mtawala wa eneo hilo akichochewa na India na Uingereza, aliamua kuliunganisha na India na kupuuza matakwa ya wananchi. Baada ya kutangazwa habari hiyo Pakistan ililishambulia eneo hilo na kutwaa sehemu ya Jammu na Kashmir. Tangu wakati huo hadi sasa India na Pakistan zimepigana vita mara mbili juu ya umiliki wa eneo la Jammu na Kashmir na hitilafu za pande hizo mbili zingali zinaendelea.

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita maajenti wa shirika la ujasusi la Israel Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Katibu mkuu wa zamani wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Dakta Fathi Shiqaqi, akiwa huko Malta. Shiqaqi alizaliwa mwaka 1951 katika kambi ya wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza. Alihitimu masomo ya udaktari na kufanya kazi katika hospitali moja ya Baitul Muqaddas. Alianzisha harakati za mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel akiwa bado kijana. Mwaka 1979 Dakta Shiqaqi alikamatwa na kusweka jela nchini Misri kwa sababu ya kuandika kitabu kuhusu harakati za Imam Ruhullah Khomeini na ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Dakta Shuqaqi aliitangaza Siku ya Kimataifa ya Quds iliyoainishwa na Imam Khomeini, kuwa ni siku ya kuhuisha Uislamu na mapambano ya jihadi dhidi ya Wazayuni huko Palestina.

Dakta Fathi Shiqaqi

Na tarehe 26 Oktoba miaka 26 iliyopita mfalme wa zamani wa Jordan Hussein na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Yitzhak Rabin walitia saini makubaliano eti ya amani. Mkataba huo ulishinikizwa na Marekani kwa ajili ya kile kilichotajwa na jitihada za kuanzisha mapatano kati ya Waarabu na Israel.

Tags