Oct 28, 2020 11:28 UTC
  • Jumanne tarehe 27 Oktoba 2020

Leo ni Jumanne tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka 1442 Hijria sawa na Oktoba 27 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 1487 iliyopita alifariki dunia babu yake Mtume Muhammad (saw), Bwana Abdul Muttalib katika mji wa Makka. Mtukufu huyo alikuwa miongoni mwa wakuu wa kabila la Kuraish kabla ya kudhihiri Uislamu na alikuwa hodari mno katika fasihi ya lugha ya Kiarabu. Bwana Abdul Muttalib alikuwa msimamizi na mshika ufunguo wa nyumba tukufu ya al-Kaaba. Vilevile babu huyo wa Mtume alikuwa akitayarisha chakula na maji kwa ajili ya watu wanaozuru nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu na kazi hiyo aliirithi kutoka kwa baba yake. Aliheshimu mno mikataba na ahadi zake na kwa sababu hiyo alikuwa na ushawishi mkubwa baina ya watu. Miongoni mwa watoto wa mtukufu huyo ni Abdullah, baba yake Mtume wetu Muhammad (saw) na Abu Twalib, baba yake Imam Ali bin Abi Twalib (as).

Tarehe 10 Rabiul Awwal miaka 1470 iliyopita, yaani miaka 28 kabla ya Hijra, Mtukufu Mtume Muhammad (saw) alimuoa Bibi Khadija binti Khuwailid (as). Bibi Khadija alikuwa mwanamke sharifu, mwenye imani na maarufu kwa ukarimu wake katika zama za ujahilia na alikuwa maarufu kwa lakabu ya "Twahira" kwa maana ya msafi na mtoharifu. Baada ya kufunga ndoa na Nabii Muhammad (saw) Bibi Khadija alikuwa msaidizi mkubwa na mwenzi wa mtukufu huyo katika hatua zote za maisha yake. Alisabilia kila kitu kwa ajili ya Uislamu na Mtume Muhammad (saw). Aidha Bibi Khadija (as) aliishi pamoja na Mtume kipindi cha miaka 25 na daima alikuwa mke mwema na mwenye kujitolea kwa mumewe Mtume Muhammad (saw) mbora wa walimwengu.

Siku kama ya leo miaka 115 iliyopita nchi ya Norway ilivunja muungano wake na Sweden na kujitangazia uhuru. Kabla ya karne ya 14 Norway ilikuwa nchi yenye ushawishi na moja ya madola vamizi. Hata hivyo mnamo mwaka 1380 ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Denmark na kuendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo kwa muda wa karne 4.

Bendera ya Norway

Miaka 110 iliyopita katika siku kama leo, baada ya Japan kupigana vita na nchi mbili za China na Russia kwa miaka kadhaa na kupata ushindi katika vita hivyo, iliunganisha rasmi ardhi ya Korea na ardhi yake. Korea iliendelea kuwa chini ya udhibiti wa Japan hadi mwaka 1945 wakati Japan iliposhindwa katika Vita vya Pili vya Dunia.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita Imam Ruhullah Khomeini alipinga vikali mpango wa mfalme wa zamani wa Saudi Arabia, Fahad bin Abdul Aziz kuhusu mapatano ya Palestina na Israel. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na baada ya kutiwa saini mkataba wa Camp David baina ya serikali ya Misri na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani, tawala vibara za Kiarabu zilifuata nyayo za utawala wa Misri katika suala hilo. Wakati huo Fahad bin Abdul Aziz aliyekuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, alitoa pendekezo la kutambuliwa rasmi utawala wa vamizi wa Israel, suala ambalo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Waislamu kote duniani. Kwa msingi huo katika siku kama hii ya leo Imam Ruhullah Khomeini alitoa hotuba akisema: "Ni wajibu kwetu sisi na kwa kila Mwislamu kupinga mipango kama ule uliopendekezwa na Fahad. Tunawajibika kulaani mipango kama hii isiyokuwa na faida kwa watu wanaodhulumiwa. Jambo hatari sana kwa sasa ni makubaliano ya Camp David na mpango wa Fahad ambayo inaimarisha zaidi Israel na kudumisha jiani zake." Upinzani huo wa wazi wa Imam Khomeini na uungaji mkono wa Waislamu kote dunia kwa misimamo hiyo ya Imam ilikuwa sababu ya kukataliwa na kupingwa pendekezo hilo katika nchi nyingine. 

Imam Ruhullah Khomeini