Ijumaa tarehe 30 Oktoba mwaka 2020
Leo ni tarehe 13 Rabiul Awwal 1442 Hijria sawa na tarehe 30 oktoba mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 110 iliyopita yaani tarehe 30 Oktoba 1910 alifariki dunia Henri Dunant, mwasisi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Dunant alizaliwa Geneva na mwaka 1828, aliamua kuanzisha Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa shabaha ya kuokoa maisha ya majeruhi wa vita. Kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu, Henri Dunant alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1901, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.
Siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, yaani tarehe 9 Aban 1304 Hijria Shamsia, Bunge la Ushauri la Taifa la Iran lilichukua uamuzi wa kumuuzulu Ahmad Shah, mfalme wa mwisho wa silsila ya Qajar na kutangaza kuufuta kikamilifu utawala wa kizazi hicho nchini Iran kilichobaki madarakani kwa kipindi cha miaka 135. Baada ya kuondoshwa utawala wa silsila ya Qajar, Uingereza ilifanya njama za kuingilia kati na kuuweka madarakani utawala wa muda nchini ulioongozwa na Reza Khan. Reza Khan alijitangaza kuwa mfalme na kuanzisha silsila ya utawala wa Kipahlavi. Utawala huo wa Kipahlavi uliandaa mazingira ya kuporwa zaidi utajiri wa taifa na kukandamizwa wananchi wa Iran kulikofanywa na madola ya Uingereza na Marekani.
Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio nambari 540 baada ya utawala wa Baathi wa Iraq kushambulia meli za kibiashara katika Ghuba ya Uajemi. Azimio hilo lilitolewa kufuatia mashambulizi ya utawala wa Iraq dhidi ya meli za kibiashara katika kipindi cha vita vyake vya kichokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hujuma ambazo zilikuwa na lengo la kuchafua usalama wa eneo hilo. Azimio hilo lilisisitiza haki ya meli zote za kibiashara kufanya safari kwa uhuru katika maji ya kimataifa na lilizitaka nchi zote kuheshimu suala hilo. Azimio nambari 540 la Baraza la Usalama pia lilizitaka pande mbili hasimu kukomesha mapigano katika Ghuba ya Uajemi na kuheshimu ardhi ya nchi za eneo hilo. Inafaa kuashiria kuwa, azimio hilo lilitolewa huku utawala wa Saddam Hussein ukizidisha mashambulizi yake dhidi ya meli za mafuta za Iran.
Tarehe 31 Oktoba miaka 34 iliyopita, alifariki dunia malenga wa zama hizi wa Iran, Salman Harati. Harati ambaye jina lake la asili ni Salman Qanbar Harati, alizaliwa katika kijiji cha Marz Dasht cha mji wa Tonekabon nchini Iran. Alikuwa malenga mwanamapinduzi na shakhsia wa kidini. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na ‘Asman Sabz’ na ‘Dari be Khoneh Khorshid’ kadhalika aliandika kitabu cha ‘Azin Setareh ta Ansetareh’ ambacho hufundishwa mashuleni. Alijitahidi kutumia lugha nyepesi katika mashairi yake ili kumuwia rahisi msomaji kuelewa.