Jumamosi, 31 Oktoba, 2020
Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1442 Hijria mwafaka na tarehe 31 Oktoba 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1378 iliyopita Yazid bin Muawiya aliangamia. Yazid alikuwa mtawala dhalimu na fasiki na alitawala kwa muda wa miaka mitatu na miezi tisa. Katika kipindi cha utawala wake Yazid mwana wa Muawiya alifanya jinai kubwa na za kutisha. Miongoni mwa jinai hizo ni kumuua shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW yaani Imam Hussein bin Ali AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala huko Iraq mwaka 61 Hijria, kushambulia kinyama miji mitakatifu ya Makka na Madina, kubomoa nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba na kuhalalisha mji wa Madina siku tatu ambapo askari wake waliwabaka na kuwanajisi wake na mabinti wa maswahaba wa Mtume Muhammad (saw). ***
Miaka 106 iliyopita katika siku kama ya leo, serikali ya wakati huo ya Iran ilitangaza kutofungamana na upande wowote katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Hata hivyo udhaifu wa kisiasa wa watawala wa wakati huo, matatizo ya ndani, matatizo ya kivita na kupenda kujitanua kwa nchi zilizokuwa zikipigana katika vita hivyo ni mambo yaliyopelekea nchi hii kwenda kinyume na ahadi yake ya kutofungamana na upande wowote katika vita hivyo. Ni kutokana na hali hiyo, ndipo Iran ikajikuta katika hujuma na mashambulizi ya majeshi ya Uingereza, Urusi ya zamani na jeshi la Othmania na kuisababishia hasara kubwa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Aban 1359 Hijria Shamsia, alikamatwa mateka Mhandisi Muhammad Jawad Tondguyan Waziri wa Mafuta wa wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na maafisa kadhaa wa wizara hiyo. Operesheni hiyo ilifanywa na majeshi ya Iraq mwezi mmoja tu baada ya majeshi ya Iraq kushambulia ardhi ya Iran. Mhandisi Tondguyan alikwenda kusini mwa Iran kwa shabaha ya kukagua visima na viwanda vya mafuta katika eneo hilo. ***
Tarehe 31 Oktoba 1984 yaani siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, aliuawa Bi. Indira Gandhi, Waziri Mkuu wa wakati huo wa India. Mauaji hayo yalifanywa na walinzi wawili wa kiongozi huyo ambao walikuwa Masingasinga. Masingasinga hao walifanya mauaji hayo baada ya Gandhi kutoa amri ya kushambuliwa hekalu la dhahabu lililoko katika jimbo la Punjab, ambalo lilihesabiwa na masingasinga kuwa ni eneo takatifu. Masingasinga ambao wanaunda asilimia mbili ya watu wa India na wengi wao wanaishi katika jimbo la Punjab, walikusanya silaha zao kwenye hekalu hilo kwa shabaha ya kufanya uasi na kutaka kujitenga jimbo hilo. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 27 iliyopita, aliaga dunia Federico Fellini mtengenezaji filamu maarufu wa Kiitalia. Fellini ni miongoni mwa watengenezaji na waongozaji filamu wakubwa wa karne ya ishirini. Fellini alianza kazi ya kuandika filamu tangu mwaka 1938 na baadaye akajiingiza katika utengenezaji filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945, Federico Fellini akiwa msaidizi wa mtengeneza filamu aliyejulikana kwa jina la Roberto Rossellini walitengeneza filamu iliyojulikana kwa jina la "Rome Open City". Mwaka 1993, yaani miezi sita kabla ya kifo chake, Fellini alitunukizwa tuzo ya Oscar kutokana na kazi zake za thamani katika ulimwengu wa filamu.***